2016-03-14 07:57:00

Matendo ya huruma na toba ya kweli!


Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika ujumbe wake wa Kwaresima kwa Mwaka 2016 linatafakari kwa kina na mapana kuhusu huruma ya Mungu; ufunuo wa huruma ya Mungu kwa mwanadamu; Kanisa na huruma ya Mungu. Leo katika Makala ya Hazina Yetu, Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican inaendelea kukushirikisha kuhusu matendo ya huruma: kiroho na kimwili; umuhimu wa toba ya kweli, Bikira Maria Mwenyehuruma na hatimaye, hitimisho la Ujumbe wa Kwaresima kutoka kwa Maaskofu Katoliki Tanzania.

Matendo ya huruma

“Iweni na huruma, kama Baba yenu alivyo na huruma”. Kristo Bwana wetu anatufundisha na kututaka kuwatendea wanadamu wote kwa mapendo na huruma. “Kama Baba yenu”. Hiki ndicho kipimo. Mungu ndiye kipimo cha upendo na huruma ambao wanadamu wanaalikwa kuudhihirisha katika maisha yako. Tunapowatendea wenzetu matendo ya huruma tunamtendea Kristo mwenyewe anayetueleza uwepo wake kwao. “Kadiri mlivyomtendea mmojawapo wa hao ndugu zangu walio wadogo, mlinitenda mimi (Rej. Mt 25:40). Mapendo na huruma yakikristo si ya vionjo bali ya hitaji. Mungu anatupenda sisi si kwa sababu tunavutia, bali tunavutia kwa sababu anatupenda na kutuhurumia daima (Rej. Kum 6:5, Law 19:8). Hivi tunapopendana kuhurumia jirani zetu, tunawafanya wavutie na kupendeza na tunaufanya uumbaji uvikwe kwa sura yake ya uhalisia wa awali inayovutia.

Mapendo kwa jirani yana msingi wake katika kumpenda Mungu. Ndiyo maana Yesu anasisitiza kuwa, kumpenda Mungu kuende sambamba na kumpenda jirani (Rej. Mt 22:39). Jirani ni mtu yeyote, mhitaji. Mfano wa Msamaria mwema unasisitiza fundisho hilo (Rej. Lk 10:25-37). Na sheria yote na manabii inategemea amri hiyo ya Mapendo (Rej. Mt 22:40). Kumpenda Mungu ina maana pia kupenda vyote vinavyopendwa na Mungu. “Kwahiyo, huruma kwa masikini na wagonjwa, vilevile matendo ya huruma ya ujima, yenye lengo la kupunguza kila aina ya dhiki za wanadamu, yanaheshimiwa na Kanisa kwa namna ya pekee… Utendaji wa huruma leo waweza kuwaelekea watu wote kabisa na mahitaji yao, na lazima uwe wa namna hiyo. Kila mahali wapo watu wenye kukosa chakula, na kinywaji, mavazi, makao, madawa, kazi na elimu, na vifaa vinavyohitajika ili kuweza kuishi maisha yaliyo kweli ya kiutu. Wapo wanaohangaika katika dhiki au kwa sababu ya kukosa afya, wanaoteseka mbali na makwao au walio kifungoni, na hapo mapendo ya Kikristo lazima yawatafute na kuwapata, kuwaliwaza kwa uangalizi mkarimu na kuwainua kwa kuwapatia msaada.” 

Tunapenda basi kuwakumbusha tena mafundisho ya Kanisa letu juu ya matendo ya huruma ya mwili na ya roho. Mapokeo ya Kanisa letu yanatufundisha juu ya matendo saba ya mwili, ambayo Kanisa limechota toka Maandiko Matakatifu (Rej. Mt 25:36; Tobit 1:17).

(i) Kuwalisha wenye njaa

(ii) Kuwanywesha wenye kiu

(iii) Kuwavika wasio na nguo

(iv) Kuwakaribisha wasio na makazi

(v) Kuwatembelea wagonjwa

(vi) Kuwatembelea wafungwa

(vii) Kuwazika wafu.

Tukifanya hivyo, huruma ya Mungu itakuwa wazi kwetu na kwao. “Katika parokia zetu, jumuiya zetu, vyama vyetu vya Kitume na vikundi, katika maana kwamba popote alipo Mkristo; kila mmoja apate chemchemi ya huruma.” Kusoma, kutafakari na kusikiliza Neno la Mungu ni msaada mkubwa katika kutembea kwenye njia ya huruma. Pamoja na matendo hayo ya huruma ya mwili mapokeo ya Kanisa yanatufundisha pia kutenda matendo ya huruma ya roho yanayotupeleka kuwajibika katika:

(i) Kuwashauri wenye mashaka

(ii) Kuwafundisha wasiojua

(iii) Kuwafariji wenye huzuni

(iv) Kuonya wakosefu

(v) Kusamehe makosa

(vi) Kuvumilia wasumbufu

(vii) Kuombea wazima na wafu

Jamii yetu inajumuisha watu wenye uwezo mkubwa na wenye uwezo mdogo. Wengine ni wazee, watoto, wagonjwa na walemavu, n.k. Tunawahimiza walio na uwezo kuwasaidia wasio na uwezo. Haya ni makundi ya watu wanaotuzunguka kila siku na huu ni uhalisia wa maisha. Tujifunze kumwona Yesu katika wahitaji hawa na tutambue kuwa kila tunapowahudumia tunakuwa tunaliboresha hekalu la Roho Mtakatifu. Tukitumie kipindi cha Kwaresima mwaka huu kama fursa ya kujikumbusha mapokeo haya ya Kanisa na kiwe kipindi cha kuadhimisha na kung’amua huruma ya Mungu. Tukiyatenda matendo haya ya huruma tutakuwa tunadhihirisha huruma na upendo wa Mungu unaoendelezwa katika maisha yetu ya kila siku kupitia ukarimu wa kikristo. Huruma na upendo huenda pamoja.

Toba ya kweli

Mungu wetu ni mwingi wa huruma na mtakatifu. Ingawa anachukia dhambi, hamchukii mkosefu. Anatupokea kila tunaporudi kwake na kutubu. Tunawahimiza kuikimbilia Sakramenti ya Kitubio ili kila mkosefu anayetubu ajipatanishe na Mungu na Kanisa. Sakramenti ya Kitubio inatuwezesha kuugusa utukufu wa huruma ya Mungu. Toba ya kweli inatudai kujirekebisha na kubadilika, kuacha dhambi na kuepuka nafasi ya dhambi. Ili kupokelewa katika ufalme wa Mungu, mwanadamu ni lazima ageuke na kuachana na njia zake mbaya na kushikamana na tangazo la Yesu la ufalme wa Mungu. Hivyo toba ni dai la kwanza la Yesu kwa wale wanaotaka kushiriki katika utawala wa Mungu (Rej. Mt 21:28 – 32).

Toba ni nafasi ya kubadili hali na misimamo yetu mibovu; kama vile dhuluma, uonevu kwa wanyonge, mauaji na rushwa inayopoteza matumaini ya wanyonge. Tusikilize sauti za wanyonge na maisha yao, kwa haki na upendo. Tujue kuwa dhambi zetu hata zile nyepesi zinatuletea shida. Dhambi nyepesi zinadhoofi sha mapendo na kuzuia maendeleo ya kiroho katika zoezi la fadhila na maisha mema.Tuziungame nazo hizo pia! Tendo la upendo wenye huruma linakuwa na huruma kweli kweli, pale tunapojiridhisha na kujiaminisha kwamba wakati tunalitenda, vilevile, tunapokea huruma kutoka kwa watu wale tunaowatendea. Kama sifa hii ya kutoa na kupokea haipo,matendo yetu yatakuwa hayajastahili kuitwa matendo ya huruma; wala ule wongofu ambao Kristo alituonyesha kwa maneno na maisha yake, hata kufa msalabani, utakuwa haujakamilika; wala tutakuwa hatujashiriki katika chanzo cha ajabu cha upendo wenye huruma ambao yeye alitufunulia.”

SURA YA NNE: BIKIRA MARIA MAMA MWENYEHURUMA

Mapokeo ya Kanisa letu yanatupatia sala ya “Salamu Malkia” inatutafakarisha huruma ya Mungu kwa kumuangalia Mama yetu Bikira Maria, aliye tulizo katika mahangaiko yetu. Yeye aliepushwa na kila doa la dhambi; alikuwa wa kwanza kati ya wote na kwa namna ya pekee alifaidi ushindi ulioletwa na Kristo juu ya dhambi: alikingiwa kila doa la dhambi ya asili, na katika maisha yake yote ya hapa duniani, kwa neema ya pekee ya Mungu, hakutenda dhambi yoyote. Mama huyu alitumia vizuri uhuru wake akakubali kuwa Mama wa Mwana pekee wa Mungu, Yesu Kristo Bwana wetu. Kwa maisha yake amemwimbia Mungu sifa daima. Anatukumbusha pia kuwa huruma ya Mungu kwetu sisi wanadamu “hudumu kizazi hata kizazi” (Lk 1:50).

Mama Maria ameshiriki mpango wa ukombozi kwa kutustahilia uzima mpya wa Roho zetu. Maana “Bwana mwenyewe amekuja kumkomboa binadamu na kumtia nguvu akimwumba upya ndani yake na kumfukuza mkuu wa ulimwengu huu, aliyekuwa amemfunga katika utumwa wa dhambi.” Tunawahimizeni nyote kwa maombezi ya mama Bikira Maria kujibidisha kutenda mema ili kujijengea fadhila na kujipatia majina yenye sifa njema katika maisha. Tumuombe mama Bikira

Maria mwenye huruma awe msaada na mwombezi wetu katika juhudi zetu. Tujue kuwa Mama Bikira Maria ni mfano wetu wa namna ya kuwa mfuasi mwaminifu wa Kristo. Tuombe msaada wa maombezi ya Mama Bikira Maria ili tuweze kuwa wafuasi waaminifu wa kuonesha huruma ya Mungu kwa watu wote. Mtakatifu Bernardo anatuasa kumkimbilia Mama huyu akisema; “Ikiwa tunahofu kuikimbilia huruma ya Baba, tumgeukie Yesu Kristo aliyetwaa mwili wetu na Kaka yetu Mwenye Huruma. Na ikiwa kwa Yesu tunahofi a ukuu wa enzi ya Umungu wake, tunaweza kumkimbilia Maria Mama yetu na mtetezi wetu mwenye huruma, awasikilizae wanae kama Baba amsikilizavyo Mwana.”

HITIMISHO

Wapendwa Taifa la Mungu, kipindi cha Kwaresima ni cha kuitayarisha mioyo yetu kwa toba, kufunga, kusali, kutoa sadaka, na kutenda matendo mema ili kujiandaa kukumbuka Fumbo la Pasaka: yaani, mateso, kifo, na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo.Tukumbuke pia kwa kushiriki msalaba wake, na kwa neema yake tutashirikishwa pia utukufu wa ufufuko wake. Ni kipindi cha kutafakari zaidi zawadi ya fumbo la ukombozi wetu na namna tunavyoshiriki upendo wa Kristo katika suala zima la ukombozi, kwa mjibu wa ubatizo wetu. Tuombe neema ili tujivike fadhila ya unyenyekevu tuweze kutenda vema na kiaminifu katika utumishi wetu. Yafaa tumwombe Mungu atujalie fadhila ya unyenyekevu ambayo inatusaidia kujitambua kuwa tu wadhambi na tukishajitambua hivyo yatupasa tufanye toba mara.Tunahitaji msaada wa Kristo aliye Bwana wetu mwenye huruma tukimkimbilia atusaidie. Tukaze nia ya kuishi kama watumishi wenye huruma.

Na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania.








All the contents on this site are copyrighted ©.