2016-03-14 12:03:00

Hata kwenye bonde la uvuli wa mauti, Mungu yu pamoja na watu wake!


Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican anasema, hata leo hii mwanadamu anaendelea kutembea katika bonde la uvuli wa mauti: kuna watu wanaokufa kutokana na baridi mjini Roma, watawa wa Mama Theresa wa Calcutta waliouwawa huko Yemen, kuna watu wanaendelea kupoteza maisha kutokana na uchafuzi wa mazingira nchini Italia na kwingineko duniani. Katika shida na mahangaiko yote haya, waamini wanapaswa kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu. Hata pale ambapo kifo kiko usoni, watu wajifunze kujiaminisha mbele ya  Mungu.

Baba Mtakatifu anasema, Suzana anayesimuliwa kwenye Liturujia ya Neno la Mungu anachafuliwa sifa na wema wake kutokana na tamaa ya mwili waliyokuwa nayo wale wazee wa Baraza, lakini akaonesha ujasiri mkuu kwa kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu, ili afe akiwa mwaminifu kuliko kumsaliti Muumba wake kwa kitendo cha zinaa. Hivi ndivyo Nabii Danieli anavyompamba Suzana kutokana na uaminifu wake kwa kukaza kwamba, hata kama waamini watatembea katika bonde la mauti, hawana haja ya kuogopa, kwani Bwana ni mchungaji wao daima!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Mwenyezi Mungu daima anatembea na watu wake; anawatakia mema na kamwe hawezi kuwaacha katika utupu na upweke! Kuna mamillioni ya watu wanaotembea katika bonde na uvuli wa mauti kama vile watoto walemavu; watoto wenye magonjwa adimu; watu wanaoendelea kupoteza maisha yao kutokana na ugonjwa Saratani unaosababishwa na uchafuzi wa mazingira! Watu wanapoangalia changamoto zote hizi wanajiuliza maswali yasiyokuwa na majibu, Je, Mungu yuko wapi?

Watawa wa Mama Theresa wameuwawa kwa chuki za kidini huku wakitoa huduma ya mapendo! Kuna nchi ambazo zinaendelea kufunga mipaka yake ili kuwazuia wakimbizi na wahamiaji wasipate nafasi ya kuingia huko! Watu wanaendelea kufa kwa baridi, kiasi cha kujiuliza, Je, Mungu yuko wapi? Katika changamoto zote hizi, Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu kwani hapa hakuna majibu ya mkato na kwamba, mambo mengi yatabaki kuwa ni fumbo mbele ya mwanadamu.

Baba Mtakatifu anawakumbusha waamini kwamba, hata Yesu mwenyewe pale Bustanini Getsemani alimwomba Baba yake, ikiwa kama inawezekana asikinywee kikombe cha mateso, lakini si kama anavyotaka Yeye, bali mapenzi ya Baba yake wa mbinguni yatimizwe! Hapa Yesu akajiaminisha mikononi mwa Baba yake wa mbinguni na alipokuwa pale juu Msalabani kabla ya kuyamimina maisha yake kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu akasema, Baba mikononi mwako naiweka roho yangu! Hivi ndivyo Mwenyezi Mungu anavyoendelea kutembea na waja wake na Kanisa kama kielelezo cha imani!

Kwa mwamini anayejiaminisha na kumtegemea Kristo hata kama atapita kwenye bonde la uvuli wa mauti, hatatendwa mabaya, kwani Mungu yuko pamoja naye anamwongoza na kumkinga na hatari zote za maisha. Hii ndiyo neema ambayo waamini wanapaswa kumwomba Mwenyezi Mungu, hata pale wanapokiona kifo mbele ya macho yao! Hata bila kufahamu, bado wanathubutu kujiaminisha mbele ya Mungu. Hii ni sala ambayo daima inapaswa kuwa mioyoni na midomoni mwa waamini!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahii ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.