2016-03-12 15:15:00

Papa Francisko kuwasha moto wa huruma ya Mungu Poland!


Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani, huko Jimbo kuu la Cracovia, Poland kuanzia tarehe 27 – 31 Julai 2016. Hii itakuwa ni hija ya kitume nchini humo. Taarifa zinasema kwamba, Baba Mtakatifu Francisko amekubali mwaliko uliotolewa kwake na Serikali pamoja na Baraza la Maaskofu Katoliki Poland.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Siku ya XXXI ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2016 sanjari na maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu anasema, vijana wanatarajiwa kuwasha moto wa huruma ya Mungu huko Cracovia, Poland, mwezi Julai, 2016. Hii itakuwa ni Siku ya Jubilei ya Vijana Duniani; muda uliokubalika wa kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani. Jubilei ni kipindi cha kuimarisha mahusiano mema na Mungu, jirani na viumbe sanjari na kufanya matendo ya huruma. Kwa mara ya kwanza Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani yanafanyika Jimbo kuu la Cracovia, tangu Mama Kanisa kumtangaza Papa Yohane Paulo II kuwa Mtakatifu. Hii ni mara ya tatu maadhimisho haya yanafanyika sanjari na Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.