2016-03-12 06:48:00

Msaada kwa familia zinazokumbana na magumu katika maisha!


Baba Mtakatifu Francisko katika nia zake za jumla kwa Mwezi Machi, 2016 anasema familia ni kati ya kito cha thamani kubwa katika maisha ya mwanadamu, lakini ni kati ya taasisi ambazo zinakabiliwa na changamoto kubwa kwa nyakati hizi. Ujumbe wa Baba Mtakatifu ambao umetolewa kwa njia ya video katika lugha mbali mbali unaendelea kubainisha umuhimu wa familia katika maisha na utume wa Kanisa, lakini kwa namna ya pekee, anapenda kuonesha mshikamano wake wa dhati na familia ambazo zinapambana na changamoto mbali mbali katika maisha.

Kati ya changamoto hizi ni hali ngumu ya kiuchumi, magonjwa yanayoziandama familia pamoja na magumu mengine ya maisha yanayoendelea kuwa ni siri ya wanafamilia wenyewe! Katika mazingira kama haya anakaza kusema Baba Mtakatifu, watoto katika familia wanakua katika hali na mazingira magumu. Hawa ni watoto ambao wanalelewa pengine hata na familia ambazo ni tenge, kiasi hata cha kukosa uwiano makini wa makuzi yanayotolewa kati ya baba na mama! Familia nyingi za namna hii, ni zile ambazo zinasimamiwa na kuhudumiwa na wanawake peke yao. Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha ujumbe wake kwa kuwaambia wanafamilia kwamba, anapenda kuwashirikisha matumaini yake na yale ya Yesu, ili kweli watoto waweze kupata msaada makini na mazingira bora zaidi katika malezi na makuzi yao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.