2016-03-12 15:31:00

Mh. Padre Anaclet Mwumvaneza ateuliwa kuwa Askofu wa Jimbo la Nyundo!


Baba Mtakatifu Francisko amemteua Mheshimiwa Padre Anaclet Mwumvaneza kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki Nyundo, nchini Rwanda. Askofu mteule alizaliwa tarehe 4 Desemba 1956, Jimbo kuu la Kigali, Rwanda. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, akapadrishwa kunako tarehe 25 Julai 1991. Tangu wakati huo amefanya kazi na utume mbali mbali kama: Paroko msaidizi huko Kibuye, Paroko wa Parokia ya Familia Takatifu. Kuanzia mwaka 1993 ni mjumbe wa Baraza la Washauri, Jimbo kuu la Kigali, Rwanda.

Kati ya mwaka 2000 hadi mwaka 2004 alipelekwa Roma kwa masomo ya juu na kujipatia  Shahada ya uzamivu katika Sheria za Kanisa kutoka Chuo Kikuu cha Kipapa cha Gregorian. Baada ya kurejea tena nchini Rwanda kati ya mwaka 2004 hadi mwaka 2005 amekuwa ni Jaalim wa Sheria za Kanisa Seminari ya Nyakibanda. Wakati huo huo, akateuliwa kuwa ni Mkurugenzi wa Caritas Jimbo na Mwenyekiti wa Tume ya Haki na Amani, Jimbo kuu la Kigali, utume alioutekeleza hadi kufikia mwaka 2013. Kunako mwaka 2013 akateuliwa kuwa ni Hakimu kwenye Mahakama ya Kanisa Katoliki Rwanda na Katibu mkuu wa Caritas nchini Rwanda.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.