2016-03-12 17:04:00

Kituo cha Hija Kiabakari: Mahali huruma ya Mungu inapomwilishwa katika huduma


Padre Wojciech Adam Koscielniak, mmissionari wa huruma ya Mungu katika mahojiano maalum na Radio Vatican anabainisha jinsi ambavyo cheche za huruma ya Mungu zimegusa maisha yake, leo hii anataka kuwa kweli ni shuhuda na chombo cha huruma ya Mungu inayomwilishwa katika huduma ya upendo; kiroho na kimwili, katika Kituo cha Hija Kiabakari, Jimbo Katoliki la Musoma.

Kituo cha hija Kiabakari ni matunda ya huruma ya Mungu katika maisha ya Padre Wojciech ambaye amekuwepo nchini Tanzania kwa takribani miaka 26 na ushehee sasa! Anasema, anapenda kuona Kituo cha Hija Kiabakari kinakuwa ni mhimili wa huruma ya Mungu kwa njia ya Sakramenti za Kanisa hususan Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na Sakramenti ya Kitubio inayomwonjesha mwamini huruma na upendo wa Mungu, tayari kuanza tena safari ya maisha ya kiroho. Hiki ni kituo cha hija za kiroho, ambapo waamini wanaweza kujichotea tena nguvu na neema ya kusonga mbele katika maisha yao ya kiroho! Hiki ni kisima cha huruma ya Mungu!

Ili kweli huruma ya Mungu iweze kuwagusa na kuwaambata watu, Kituo cha Hija cha Kiabakari kimefanikiwa kujenga shule ya awali, msingi na sasa kinajenga shule ya Sekondari na hatimaye, Chuo cha Ufundi, ili kuwasaidia vijana kutambua, kukuza na kuendeleza vipaji vyao kwa ajili ya ujenzi wa Familia ya Mungu inayowazunguka. Ni kituo ambacho kinataka pia kuwaonjesha wagonjwa na wale wanaoteseka kimwili, huruma ya Mungu kwa kujenga kituo cha afya! Hapa wahudumu wanapaswa kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu!

Padre Wojciech katika mahojiano na Radio Vatican anagusia kwa ufupi historia ya ujenzi wa Kituo cha Hija cha Kiabakari Jimbo Katoliki Musoma, mchakato ambao ulianza kunako mwaka 1991 Hayati Justin Samba alipompatia kibali cha kuanza ujenzi wa Parokia ya Kiabakari uliohitimishwa hapo tarehe 3 Oktoba 1991. Mwaka 1992, ujenzi wa nyumba ya Mapadre ukakamilika. Kuanzia mwaka 1994 hadi mwaka 1997 Ujenzi wa Kanisa la Parokia ukakamilika na kutabarukiwa na Askofu mkuu Anthony Mayala wa Jimbo kuu la Mwanza hapo tarehe 3 Julai 1997.

Kunako tarehe 17 Agosti 2001 Askofu mkuu Luigi Pezzuto, aliyekuwa Balozi wa Vatican nchini Tanzania akatangaza Parokia ya Kiabakari Jimbo Katoliki la Musoma ni Kituo cha Hija ngazi ya Kijimbo. Kunako mwaka 2002 Padre Wojciech akahamishiwa Parokia ya Musoma mjini kwa ajili ya maandalizi ya Jubilei ya Miaka 50 ya Parokia ya Musoma mjini, Kanisa kuu la Jimbo. Hapa Padre Wojciech hakulala, akachapa kazi usiku na mchana leo hii Kanisa kuu la Jimbo Katoliki Musoma lina mwelekeo mpya kabisa. Zote hizi ni jotihada za huruma ya Mungu inayomwilishwa katika matendo yanayogusa watu kwa uwepo endelevu wa Mungu katika maisha yao!

Kunako mwaka 2006, Askofu Justin Samba wa Jimbo Katoliki Musoma, akafariki dunia na Baba Mtakatifu Benedikto XVI akamteua Askofu mkuu Athony Mayala kuwa Msimamizi wa Kitume wa Jimbo Katoliki Musoma, akamwomba Padre Wojciech Adam Koscielniak, mmissionari wa huruma ya Mungu kurejea kwenye Kituo cha Hija cha Kiabakari, ili kukiendeleza zaidi! Huu ukawa ni mwanzo wa ukurasa mpya wa Kituo cha Hija Kiabakari. Baada ya Maaskofu wa Kanda ya Ziwa kuridhika na huduma ya kiroho inayotolewa na Kituo cha Hija Kibakari, kwa sasa kuna mchakato ambao umewasilishwa kwenye Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania ili Kituo hiki kiweze kuwa ni Kituo cha Hija Kitaifa, mahali ambapo Wakleri kutoka Majimbo mbali mbali ya Tanzania wataweza kufundwa kuhusu huruma ya Mungu, tayari kuineza kwa familia ya Mungu ndani na nje ya Tanzania.

Hapa patakuwa ni mahali pa waamini kujichotea ufahamu wa kina kuhusu huruma ya Mungu! Familia ya Mungu Parokia ya Kiabakari, Jimbo Katoliki Musoma, inasubiri kwa hamu kusikia maamuzi ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania! Hapana shaka hii itakuwa ni Habari Njema ya Injili ya huruma ya Mungu nchini Tanzania, hasa wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu! Kwa ufupi hii ndiyo safari ya ufahamu wa Ibada ya huruma ya Mungu ambayo kwa sasa imeenea sehemu nyingi nchini Tanzania.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.