2016-03-11 10:33:00

Ambateni huruma ya Mungu kushinda utandawazi usiojali!


Baba Mtakatifu Francisko katika mahojiano na mwandishi wa kitabu Jina la Mungu ni huruma anabainisha sababu za kuitisha maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu; umuhimu wa waamini kujitambua kwamba, ni wadhambi hivyo wanapaswa kukimbilia huruma ya Mungu ambayo haina mipaka ni kwa ajili ya wote pasi na ubaguzi kwani Kanisa linalaani dhambi lakini linamkumbatia mdhambi. Waamini wawe tayari kupata tiba ya magonjwa yao ya kiroho, ili kuambata huruma na upendo wa Mungu. Sasa unaweza kuendelea zaidi!

Katika Sura ya Saba, Baba Mtakatifu anasema, Mdhambi anaweza kuvumiliwa lakini fisadi na mla rushwa, hawa ni watu hatari kwani wanatenda dhambi lakini si wepesi kuungama dhambi zao, tayari kujipatanisha na Mungu. Mafisadi na wala rushwa ni watu wanaowatesa na kudhalilisha wananchi wengine; ni wanafiki. Katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, Baba Mtakatifu Francisko anawaalika mafisadi na wala rushwa kutubu na kumwongokea Mungu, ili kuanza ukurasa mpya wa maisha yao. Wamwombe Mungu neema ya kuona aibu kwa dhambi walizotenda.

Huruma ni chachu muhimu sana inayoweza kudumisha umoja na udugu kati ya watu na kwamba, haki peke yake haitoshi, bali inapaswa kukamilishwa na fadhila ya huruma na mapendo, kwani Mungu anavuka haki na kwamba, hakuna haki pasi na msamaha. Msamaha ni msingi wa maisha ya jamii inayojikita katika haki na mshikamano na kwamba, huruma inapaswa kumwilishwa katika maisha ya binadamu. Baba Mtakatifu anakaza kusema, ndiyo maana Kanisa linapinga adhabu ya kifo.

Familia ni shule ya kwanza ya huruma ya Mungu na kwamba hapa wanafamilia wanajifunza kupenda na kupendwa, kusamehe na kusamehewa. Si matarajio yake kuona malango ya magereza yanafunguliwa na wafungwa wote kuachiwa huru hata wale waliotenda makosa makubwa ya jinai. Hapa Baba Mtakatifu anakaza kusema, wafungwa wasaidiwe kutubu, kuongoka na kuanza tena kuandika ukurasa mpya wa maisha yao, wakiwa ni watu wema zaidi kuliko walivyoingia magerezani.

Katika sura ya nane, Baba Mtakatifu anawakumbusha walimwengu kwamba, Mwenyezi Mungu anawapenda upeo na anataka kuwaonjesha huruma yake isiyokuwa na mipaka. Mwenyezi Mungu kwanza kabisa anaonesha uso wa binadamu na pili uso wa Kimungu. Yesu anamwangalia mwanadamu kutoka katika undani wa maisha yake na wala si kama mpiga picha anayeangalia mambo ya nje. Mwenyezi Mungu anamshirikisha mwanadamu katika maisha na mipango yake, mwaliko kwa walimwengu kuambata huruma ya Mungu ili kushinda kishawishi cha utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine.

Sura ya tisa ambayo ni hitimisho la maswali 40 ambayo Baba Mtakatifu Francisko amejitahidi kuyajibu kwa ufasaha mkubwa, inajikita katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili; mambo msingi yanayomwezesha mwamini kuonja huruma na upendo wa Mungu katika maisha yake. Huu ndio mwaliko wa Kristo Yesu kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Waamini wanaalikwa kuwapokea na kuwaonjesha huruma na upendo maskini wa kiroho na kimwili; mdhambi aliyejeruhiwa kutoka katika undani wa maisha yake na kwamba, hapa ndipo Wakristo wanapotakiwa kuonesha ushuhuda wa huruma ya Mungu. Waamini wakumbuke kwamba, mwisho wa siku, wote watahukumiwa kutokana na huruma na upendo kwa jirani zao kama anavyosema Mtakatifu Yohane wa Msalaba.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.