2016-03-10 07:20:00

Ratiba elekezi: Fumbo la Pasaka: kiini cha huruma ya Mungu!


Maadhimisho ya Juma kuu ni kiini cha tafakari ya huruma ya Mungu kwa mwanadamu. Hapa Kanisa kwa namna ya pekee linakumbuka mateso, kifo na ufufuko wa Kristo. Maadhimisho haya yanapata uzito wa pekee wakati huu wa Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake kwa ajili ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu anasema, Yesu baada yak usali Zaburi ya huruma kama anavyosimulia Mwinjili Mathayo, Yesu na mitume wake walitoka kwenda kwenye Mlima wa Mizeituni. Kumbe, Juma kuu linafunguliwa kwa maadhimisho ya Jumapili ya Matawi.

Ratiba elekezi inaonesha kwamba, Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 20 Machi 2016, majira ya saa 3:30 kwa Saa za Ulaya, ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, Jumapili ya Matawi, itakayoanza kwa maandamano ya matawi, kukumbuka siku ile Yesu alipoingia mjini Yerusalemu kwa shangwe, watoto wa Wayahudi wakatandika nguo zao njiani huku wakimwimbia Yesu, Hossana mwana wa Daudi, mbarikiwa ajaye kwa jina la Bwana! Katika Ibada hii ya Misa Takatifu, waamini watatafakari Mateso ya Kristo, chemchemi ya huruma ya Mungu kwa waja wake. Hii ni Siku ya Vijana Kijimbo inayoongozwa na kauli mbiu “Heri wenye rehema maana hao watapata rehema”. Kilele cha maadhimisho haya sanjari na Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ni huko Jimbo kuu la Cracovia, Poland.

Tarehe 24 Machi 2016, Saa 3: 30 majira ya asubuhi, Baba Mtakatifu Francisko ataongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya Kubariki Mafuta ya Krisima ya Wokovu. Haya ni mafuta yatakayotumiwa na Mama Kanisa wakati wa maadhimisho ya Sakramenti mbali mbali za Kanisa. Hii ni siku ambayo Wakleri wanarudia tena ahadi zao za utii kwa Askofu mahalia. Ibada hii itaadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Alhamisi kuu ni Siku ambayo Yesu mwenyewe aliweka Sakramenti ya Daraja Takatifu na Ekaristi Takatifu; akaonesha huruma na upendo unaomwilishwa katika huduma kwa kuwaosha mitume wake miguu, changamoto kwa familia ya Mungu kuhudumiana. Kumbe, Ekaristi Takatifu ni kumbu kumbu endelevu ya huruma ya upendo wa Kristo kwa waja wake.

Ijumaa kuu tarehe 25 Machi 2016, Saa 11: 00 Jioni kwa saa za Ulaya, Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kuongoza Ibada ya Ijumaa kuu, itakayoanza kwa Liturujia ya Neno; Ibada ya Kuabudu Msalaba, kielelezo makini cha huruma ya Mungu na baadaye, waamini watashiriki Komunio Takakatifu. Katika chemchemi ya ufunuo wa huruma ya Mungu anasema Baba Mtakatifu Francisko, Yesu aliingia katika mateso na kifo chake kwa kudhamiria lile Fumbo kuu la Upendo ambalo angalikamilisha pale juu Msalabani. Akiwa pale Msalabani, Askari mmoja wapo akamchoma ubavuni kwa mkuki, mara ikatoka Damu na Maji, alama za Sakramenti za Kanisa.

Ijumaa kuu, majira ya Saa 3:15 Usiku, Baba Mtakatifu ataongoza Ibada ya Njia ya Msalaba kuzunguka Magofu ya Colosseo na baadaye atatoa baraka zake za kitume! Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko amemteua Kardinali Gualtiero Bassetti, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Perugia, Italia kuandaa tafakari ya Njia ya Msalaba kuzunguka Magofu ya Colosseo mjini Roma, Ijumaa kuu. Njia hii ya Msalaba inazingatia Vituo 14 kadiri ya Mapokeo ya Kanisa. Kwa namna ya pekee, mwaka huu, Njia ya Msalaba inapania kugusa mateso na mahangaiko ya binadamu katika ulimwengu mamboleo, ili waweze kuonja na kuguswa na huruma ya Mungu katika mahangaiko yao ya kila siku.

Tarehe 26 Machi 2016 Saa 20:30 Usiku, Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kuongoza Mkesha wa Pasaka. Huu mkesha mama wa mikesha yote ya Liturujia inayoadhimishwa na Mama Kanisa. Baba Mtakatifu atabariki moto na baadaye yatafuatia maandamano kuingia kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, wakiwa wametanguliwa na Mshumaa wa Pasaka, alama ya Kristo Mfufuka. Itafuatiwa Mbiu ya Pasaka maarufu kama “ Exsultet”. Baba Mtakatifu ataongoza Liturujia ya Neno la Mungu, Liturujia ya Ubatizo ambamo Wakristo watarudia tena ahadi zao za Ubatizo, tayari kuambata huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao. Mkesha huu utahitimishwa kwa Liturujia ya Ekaristi.

Tarehe 27 Machi 2016 ni Pasaka ya Bwana, kilele cha ufunuo wa huruma ya Mungu kwa binadamu! Baba Mtakatifu Francisko majira ya saa 4:00 asubuhi anatarajiwa kuongoza Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican na hatimaye, kutoa salam kwa mji wa Roma na Ulimwengu kwa ujumla, maarufu kama “Urbi et Orbi”. Huu ni ujumbe maalum kwa Familia ya Mungu duniani.

Kama kawaida, Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican itakushirikisha kwa kina na mapana yale yatakayojiri katika maadhimisho ya Juma kuu, Mama Kanisa anapotafakari kwa namna ya pekee, huruma ya Mungu katika maisha ya mwanadamu! Ukiwa na haraka zako, unaweza kujipatia habari kutoka kwenye mtandao wa Radio Vatican. Ukiguswa na huruma ya Mungu, mshirishe pia jirani yako kwa njia ya mitandao ya kijamii!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.