2016-03-08 14:01:00

Kumbu kumbu ya Miaka 3 ya Uongozi wa Papa Francisko!


Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma, Jumapili tarehe 13 Machi 2016 ataadhimisha kumbu kumbu ya miaka mitatu tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki. Hiki ni kipindi ambacho kimekuwa na matukio pamoja na changamoto nyingi katika maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko. Padre Federico Lombardi, msemaji mkuu wa Vatican anasema, Baba Mtakatifu anaendelea kujipambanua kama mwalimu wa Kanisa na binadamu katika ujumla wake. Katika kipindi cha miaka mitatu ya utume wake, amejitahidi kutembelea mabara yote, isipokuwa Oceania.

Huko amegusa na kushuhudia furaha, matumaini na mahangaiko ya familia ya Mungu katika ujumla wake. Amekuwa mstari wa mbele kuzungumzia: haki na amani; dhidi ya vita vinavyoendelea kusababisha majanga makubwa katika maisha ya watu. Amegusia kuhusu utandawazi wa mshikamano unaojikita katika kanuni auni badala ya kuendekeza utamaduni usioguswa na mahangaiko ya watu wengine. Waraka wa Baba Mtakatifu Francisko “Sifa kwako, juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” Laudato si unagusa masuala nyeti yanayotishia ustawi, usalama na maendeleo ya binadamu katika ulimwengu mamboleo.

Jumuiya ya Kimataifa inamwangalia Baba Mtakatifu kama dira na mwongozo wa maisha, kielelezo kwamba, kwa hakika ni Mwalimu mahiri, makini na anayeaminika katika huduma na utume wake unaojikita katika maisha ya kiroho na kimaadili. Padre Lombardi anakaza kusema, wakuu wa dunia hii ni watu muhimu sana katika mchakato wa maendeleo ya binadamu kama ilivyo pia kwa maskini, ili kuwa na matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi!

Baba Mtakatifu katika kipindi hiki cha miaka mitatu, kwa hakika amekuwa ni shuhuda na chombo cha huruma ya Mungu; tema ambayo ameivalia njuga katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Ni muasisi wa maadhimisho ya Jubilei yenye mwelekeo mpana katika maisha na vipaumbele vya watu, ili kila mtu mahali alipo, aweze kuguswa, na hatimaye, kuambata huruma na upendo wa Mungu unaomwilishwa katika ushuhuda wa imani tendaji!

Matendo ya huruma: kiroho na kimwili, iwe ni chachu ya Uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wa upendo, hasa miongoni mwa maskini ambao kimsingi ni walengwa wakuu wa Habari Njema ya Wokovu. Baba Mtakatifu anaendelea kutoa mwaliko kwa waamini kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Kristo na Kanisa lake, Neno la Mungu na Maisha ya Kisakramenti; kielelezo makini cha tasaufi na maisha ya kiroho. Haya ni maisha yanayopaswa kumwilishwa katika matendo ya huruma!

Padre Lombardi anasema, Baba Mtakatifu amedhamiria kuendeleza mchakato wa mageuzi yaliyodokezwa na Makardinali wakati wa vikao vyao elekezi. Anafanya mageuzi haya kwa kuzingatia Injili, Mapokeo na Mafundisho ya Kanisa, ili kweli miundo mbinu inayomilikiwa na kusimamiwa na Kanisa, iweze kukidhi mahitaji ya Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo! Tangu mwanzo, Makardinali walionesha imani na matumaini yao kwa Baba Mtakatifu Francisko; kazi anayoendelea kuivalia njuga hatua kwa hatua, akiwa mwaminifu kwa Injili ya Kristo na uhuru kamili.

Baba Mtakatifu ametoa kipaumbele cha pekee katika dhana ya umoja na ushirikishwaji wa familia ya Mungu katika maisha na utume wa Kanisa kwa njia ya maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu, dhana inayopaswa kufanyiwa kazi katika ngazi mbali mbali za maisha na utume wa Kanisa mahalia. Lengo ni kuwa na msimamo wa pamoja katika kukabiliana na changamoto, fursa na matatizo yanayolikabili Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo, daima, wakiongozwa na Injili ya Kristo!

Licha ya umaarufu na unyenyekevu unaoshuhudiwa na Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake, anasema Padre Lombardi, bado kuna watu “wanamrushia madongo”! Hili ni jambo la kawaida katika maisha ya binadamu kwani watu wanaogopa yale wasioyafahamu; watu wana wasiwasi na mambo ya mbeleni; jambo ambalo Baba Mtakatifu anapaswa kulitekeleza kwa kujizatiti, kwa ujasiri, huku akijikita katika imani na matumaini kwamba, anaongozwa na Roho Mtakatifu katika kutekeleza mapenzi ya Mungu kwa Kanisa lake. Baba Mtakatifu ni nahodha anayeliongoza Kanisa, katika ukweli na uwazi, ili liweze kufikia malengo yake.

Padre Lombardi anahitimisha mahojiano maalum na Radio Vatican mintarafu miaka mitatu tangu Baba Mtakatifu Francisko alipochaguliwa kuliongoza Kanisa kwa kusema kwamba, amekuwa kweli ni shuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa maskini, wagonjwa na wale wanaoteseka: kiroho na kimwili. Kwa njia hii, wengi wameguswa na kuonja huruma ya Mungu katika maisha yao. Kwa hakika hili ni jambo la kumshukuru Mungu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.