2016-03-08 07:37:00

Changamoto ya wahamiaji Barani Ulaya!


Mashirika mbali mbali ya kitawa na kazi za kitume, yamekuwa mstari wa mbele katika kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta hifadhi na usalama wa maisha sehemu mbali mbali za dunia. Mashirika haya yanajitahidi kujibu kilio cha wahamiaji na wakimbizi wanaoendelea kulichangamotisha Kanisa katika maisha na utume wake, ili liweze kujibu kilio hiki mintarafu Injili ya huruma ya Mungu. Hii ni changamoto inayotolewa na Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Maadhimisho ya Siku ya Wakimbizi Duniani kwa mwaka 2016. Hii ni changamoto pevu pia kwa Jumuiya ya Kimataifa.

Padre Gabriele Bentoglio Katibu mkuu msaidizi wa Baraza la Kipapa la shughuli za kichungaji kwa wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum hivi karibuni akichangia mada katika kongamano lililoandaliwa na Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume mjini Roma lililoongozwa na dhamira: “watawa na wahamiaji katika karne ya ishirini na moja: matumaini, majibu na changamoto”. Amesema, Baraza hili la kipapa ni chombo makini cha utekelezaji wa mikakati ya kichungaji kwa ajili ya wahamiaji, wakimbizi na watu wasiokuwa na makazi maalum sehemu mbali mbali za dunia.

Huu ni utume unaolisukuma Kanisa kutoa majibu muafaka yanayojikita katika Injili ya huruma ya Mungu, hususan wakati huu, Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, haki msingi za wakimbizi na wahamiaji zinalindwa na kuheshimiwa pamoja na kuwaendeleza wahamiaji na wakimbizi kama sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Changamoto ya wahamiaji na wakimbizi kwa mwaka 2016 ni kubwa kuwahi kutokea katika historia ya Jumuiya ya Kimataifa. Si jambo la kushangaza tena kuona makundi makubwa ya wahamiaji na wakimbizi yakitafuta usalama na hifadhi ya maisha sehemu mbali mbali za dunia. Takwimu zinaonesha kwamba, Bara la Ulaya lina idadi kubwa ya wahamiaji na wakimbizi, ikifuatiwa na Bara la Asia, Amerika ya Kaskazini, Afrika, Amerika ya Kusini na hatimaye, Oceania.

Wanawake na watoto ndio wanaounda kundi kubwa la wahamiaji na wakimbizi, kiasi kwamba wamegeuzwa kuwa ni wahanga wa biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo pamoja na uhalifu wa magenge. Wanawake na watoto wakishapokonywa hati na nyaraka zao za kusafiria wanageuzwa kuwa ni watumwa wa ngono, biashara haramu ya binadamu na viungo vyake. Ni kundi linalofanyishwa kazi za suluba na ndoa za shuruti. Haya ni mambo ambayo Baba Mtakatifu Francisko ameyazungumzia katika ujumbe wake kwa Siku ya Wakimbizi Duniani kwa mwaka 2016.

Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kutekeleza dhamana na wajibu wake, lakini pia waamini na watu wenye mapenzi mema, wanaguswa kwa namna ya pekee na changamoto ya Injili ya huruma ya Mungu kwa watu hawa wanaoendelea kunyanyasika. Watu wana haki ya kutohama wala kukimbia nchi zao, ikiwa kama watapata uhakika wa usalama wa maisha na utu wao. Kwa vile kuna watu wanaolazimika kukimbia au kuzihama nchi zao, basi, iwe ni fursa kwa Jumuiya ya Kimataifa na wadau mbali mbali kushirikiana kwa dhati ili kuisaidia Jamii kukua na kukomaa: kiutu, kijamii na kiroho, tayari kuchangia katika mchakato wa ustawi na maendeleo ya wengi.

Ukarimu kwa wageni ni changamoto ya Injili ya huruma ya Mungu na mwaliko wa kujenga na kudumisha madaraja yanayowakutanisha watu badala ya kujenga kuta zinazowabagua na kuwanyanyasa watu katika Jamii kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko. Jamii zijifunze kutoa na kupokea kwani hata wakimbizi na wahamiaji wanao mchango mkubwa, ikiwa kama watapewa fursa ya kushirikisha utajiri wao kwa Jamii inayowapatia hifadhi. Baba Mtakatifu anakazia kwa namna ya pekee: utu na heshima ya binadamu; upendo, umoja na mshikamano; chachu muhimu ya mabadiliko katika jamii.

Jumuiya ya Kimataifa haina budi kusimama kidete ili kuyatafutia ufumbuzi wa kudumu mambo yanayosababisha makundi makubwa ya watu kuhama na kuzikimbia nchi zao! Vita, dhuluma na nyanyaso; umaskini na hali ngumu ya maisha ni katiya mambo ambayo yanasababisha makundi makubwa ya wahamiaji na wakimbizi, changamoto inayowagusa watu wote, kila mtu kadiri ya nafasi na dhamana yake ndani ya jamii. Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu iwe ni fursa kwa Familia ya Mungu kutoa majibu muafaka kwa wakimbizi na wahamiaji mintarafu Injili ya huruma ya Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.