2016-03-07 10:14:00

Kanisa na huruma ya Mungu!


Kanisa kama Taifa na Familia ya Mungu ni wakala pia wa upendo na huruma ya Mungu. Huruma sio tu namna ya kutenda ya Mungu bali ni kigezo cha kutambua nani ni wana wa Mungu kweli. Sura ya Mungu anayehurumia inapaswa kuwa ndiyosura halisi ya Kanisa linaloendeleza fumbo la Pasaka la Kristo. “Kanisa linakiri huruma ya Mungu, Kanisa linaiishi katika mang’amuzi yake, na tena katika mafundisho yake, likimtafakari Kristo daima, likijikusanya kwake, katika maisha yake na Injili yake, katika msalaba wake na ufufuko wake, na katika fumbo lake zima…Kanisa huwaleta watu karibu na kiini cha huruma ya Mwokozi, ambaye ndiye mdhamini na mgawaji wa huruma hiyo.”

Aidha Kanisa linapokiri juu ya huruma ya Mungu linatangaza pia kuongoka na kumgeukia Mungu. Kumgeukia Mungu ni matunda ya kujitambua na kung’amua huruma ya Mungu.“Yesu Kristo ametufundisha kwamba mtu hapokei tu na kuizoea huruma ya Mungu, bali anaitwa pia kuwatendea wengine huruma.” Kristo ametufundisha hilo katika hotuba yake ya mlimani (Rej. Mt 5:1-12), mfano wa mwana mpotevu (Rej. Lk 15:11-32) na zaidi ya yote kwa mateso na kifo chake msalabani. Kristo anatufundisha kuwa yale tunayowatendea wengine hasa waliowanyonge, tunamtendea yeye mwenyewe (Rej. Mt 25:31- 40) na tunayoacha kuwatendea wengine tunaacha kumtendea yeye mwenyewe (Mt 25:41-46). Sisi Maaskofu wenu tunapenda kuwakumbusha tena mambo yafuatayo, ili kwa pamoja tuweze kutangaza huruma ya Mungu na kujipatia sisi wenyewe huruma yake.

Wajibu wakutangaza Habari Njema

Kwa ubatizo wetu, sisi sote tunashiriki kazi ya unabii ya Kristo. Wajibu wetu ni kumtangaza Kristo popote katika mazingira yetu ili afahamike, apendwe na kufuatwa. Tunawatia shime wale wengi wenu ambao mnaonyesha juhudi kubwa ya kujifunza imani yetu na kuwashirikisha wengine. Wahudumu wa Daraja Takatifu, Watawa na Makatekista wanafanya jitihada kubwa ili kumpeleka Kristo na ujumbe wake wa huruma kwa watu. Hata hivyo bado inaonekana kuwa jitihada hizo si kubwa katika ngazi ya familia. Bado watoto na vijana wengi hawapati mafundisho ya msingi na ya kawaida toka kwa wazazi au walezi wao. Wazazi na walezi hawakai na watoto wao na kuwaeleza habari njema ya Kristo Bwana wetu. Tujue kuwa Mapadre, Watawa na Makatekista wetu bado ni wachache, hawawezi kumfikia kila mmoja kwa wakati na kwa kina.

Tunapenda kuwaalika waamini wote; wazazi na walezi kutumia muda wenu nyumbani kuuishi na kuwafundisha watoto ujumbe wa Kristo. Tukumbuke kuwa familia ni jumuiya na kanisa la kwanza ambamo misingi ya imani na ya utu inajengwa. Hali ya jumuiya hiyo, huathiri jumuiya zingine kubwa. Tabia za mwanzo za wanadamu zinajengwa katika familia,maana “mtoto umleavyo ndivyo akuavyo”. Wazazi na walezi wanawajibu wa kuwapatia watoto wao elimu na kuwarithisha imani na maadili (Rej. Kumb 6:20-25). Watoto wanawajibu wa kuwaheshimu wazazi wao, kuwatunza wazazi wao, hasa uzeeni, katika ugonjwa na ulemavu, kuwatii na kuwaombea wazazi, na kuwazika wakifa (Rej. Ybs 3:1-6). Wazazi jengeni mahusiano bora ili kuimarisha familia zenu. Salini pamoja, mfanye kazi pamoja kwa juhudi na kwa maarifa,mkipendana na kuheshimiana(Rej. Efe 5:22-25). Jitahidini kuishi maagano ya ubatizo wenu ili kutoa mfano bora wa maisha ya kikristo kwa watoto na wale ambao bado hawajamfahamu Kristo ili wapate kumfahamu. Tukiyaishi haya tunakuwa tunadhihirisha huruma na upendo wa Mungu unaoendelezwa katika maisha yetu ya kila siku. Huruma na upendo huenda pamoja.

Kupokea Sakramenti za Kanisa

Kristo Bwana wetu, ametuachia sakramenti ili tukizipokea vema tujipatie neema zake. Sakramenti ni kielelzo kingine cha upendo na huruma ya Mungu inayobubujika kutoka katika Fumbo la mateso, kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo. Kanisa, ambalo ni mama na mwalimu, linawapokea katika familia ya wanakanisa watu wote kwa njia ya Ubatizo, Kipaimara na Ekaristi Takatifu. Kwa njia ya Kanisa na Sakramenti za Kitubio na mpako mtakatifu Kristo ananyoosha mkono wake wa uponyaji kwa wagonjwa wa mwili na roho. Kristo ameweka pia Sakramenti za Ndoa na Daraja Takatifu kwa ajili ya kutoa huduma. Tunawahimiza wapendwa wakristo kuzishiriki kwa ari kubwa Sakramenti hizi za Kanisa inavyostahili ili kujipatia neema za Mungu. Huruma ya Mungu inajidhihirisha katika Sakramenti za Kristo katika Kanisa.

Tukumbuke kuwa, “mwaliko wa Kristo wa wongofu unaendelea kusikika katika maisha ya wakristo. Wongofu wa pili ni kazi ya kudumu ya Kanisa lote linalowakumbatia wakosefu kifuani mwake, nalo ni takatifu na papo hapo linaitwa kujitakasa na kufuata daima njia ya toba na kujifanya upya. Bidii hii ya kuongoka si kazi ya kibinadamu tu. Ni msukumo wa moyo uliovunjika, unaovutwa na neema, kuitikia mapendo yenye huruma ya Mungu aliyetupenda sisi kwanza.”14 Ubatizo, Kipaimara na Ekaristi Takatifu hutuwekea misingi yote ya maisha ya kikristo.

Tukiwa bado katika safari hapa duniani tunaelemewa na mateso, magonjwa, na dhambi. Kristo Mganga wetu hutusamehe dhambi na kuturudishia afya kwa sakramenti za Kitubio na Mpako Mtakatifu wa wagonjwa. Hatimaye sakramenti za Daraja takatifu na Ndoa zinatupatia nafasi ya kutoa utume wakuhudumia ujenzi wa Taifa la Mungu.Tukiziishi Sakramenti hizi tunakuwa tunadhihirisha huruma na upendo wa Mungu unaoendelezwa katika maisha yetu ya kila siku kupitia Sakramenti za Kanisa. Huruma na upendo huenda pamoja.

Matendo ya huruma

“Iweni na huruma, kama Baba yenu alivyo na huruma”. Kristo Bwana wetu anatufundisha na kututaka kuwatendea wanadamu wote kwa mapendo na huruma. “Kama Baba yenu”. Hiki ndicho kipimo. Mungu ndiye kipimo cha upendo na huruma ambao wanadamu wanaalikwa kuudhihirisha katika maisha yako. Tunapowatendea wenzetu matendo ya huruma tunamtendea Kristo mwenyewe anayetueleza uwepo wake kwao. “Kadiri mlivyomtendea mmojawapo wa hao ndugu zangu walio wadogo, mlinitenda mimi (Rej. Mt 25:40). Mapendo na huruma yakikristo si ya vionjo bali ya hitaji. Mungu anatupenda sisi sikwasababu tunavutia, bali tunavutia kwasababu anatupenda nakutuhurumia daima (Rej. Kum 6:5, Law 19:8). Hivi tunapopendana kuhurumia jirani zetu, tunawafanya wavutie na kupendeza natunaufanya uumbaji uvikwe kwa sura yake ya uhalisia wa awali inayovutia.

Mapendo kwa jirani yana msingi wake katika kumpenda Mungu. Ndiyo maana Yesu anasisitiza kuwa, kumpenda Mungu kuende sambamba na kumpenda jirani (Rej. Mt 22:39). Jirani ni mtu yeyote, mhitaji. Mfano wa Msamaria mwema unasisitiza fundisho hilo (Rej. Lk 10:25-37). Na sheria yote na manabii inategemea amri hiyo ya Mapendo (Rej. Mt 22:40). Kumpenda Mungu ina maana pia kupenda vyote vinavyopendwa na Mungu. “Kwahiyo, huruma kwa masikini na wagonjwa, vilevile matendo ya huruma ya ujima, yenye lengo la kupunguza kila aina ya dhiki za wanadamu, yanaheshimiwa na Kanisa kwa namna ya pekee… Utendaji wa huruma leo waweza kuwaelekea watu wote kabisa na mahitaji yao, na lazima uwe wa namna hiyo.

Kila mahali wapo watu wenye kukosa chakula, na kinywaji, mavazi, makao, madawa, kazi na elimu, na vifaa vinavyohitajika ili kuweza kuishi maisha yaliyo kweli ya kiutu. Wapo wanaohangaika katika dhiki au kwa sababu ya kukosa afya, wanaoteseka mbali na makwao au walio kifungoni, na hapo mapendo ya Kikristo lazima yawatafute na kuwapata, kuwaliwaza kwa uangalizi mkarimu na kuwainua kwa kuwapatia msaada.” Tunapenda basi kuwakumbusha tena mafundisho ya Kanisa letu juu ya matendo ya huruma ya mwili na ya roho. Mapokeo ya Kanisa letu yanatufundisha juu ya matendo saba ya mwili, ambayo Kanisa limechota toka maandiko Matakatifu (Rej. Mt 25:36; Tobit 1:17).

(i) Kuwalisha wenye njaa

(ii) Kuwanywesha wenye kiu

(iii) Kuwavika wasio na nguo

(iv) Kuwakaribisha wasio na makazi

(v) Kuwatembelea wagonjwa

(vi) Kuwatembelea wafungwa

(vii) Kuwazika wafu.

Tukifanya hivyo, huruma ya Mungu itakuwa wazi kwetu na kwao. “Katika parokia zetu, jumuiya zetu, vyama vyetu vya Kitume na vikundi, katika maana kwamba popote alipo Mkristo; kila mmoja apate chemchemi ya huruma.”16 Kusoma, kutafakari na kusikiliza Neno la Mungu ni msaada mkubwa katika kutembea kwenye njia ya huruma. Pamoja na matendo hayo ya huruma ya mwili mapokeo ya Kanisa yanatufundisha pia kutenda matendo ya huruma ya roho yanayotupeleka kuwajibika katika:

(i) Kuwashauri wenye mashaka

(ii) Kuwafundisha wasiojua

(iii) Kuwafariji wenye huzuni

(iv) Kuonya wakosefu

(v) Kusamehe makosa

(vi) Kuvumilia wasumbufu

(vii) Kuombea wazima na wafu

Jamii yetu inajumuisha watu wenye uwezo mkubwa na wenye uwezo mdogo. Wengine ni wazee, watoto, wagonjwa na walemavu, n.k. Tunawahimiza walio na uwezo kuwasaidia wasio na uwezo. Haya ni makundi ya watu wanaotuzunguka kila siku na huu ni uhalisia wa maisha. Tujifunze kumwona Yesu katika wahitaji hawa na tutambue kuwa kila tunapowahudumia tunakuwa tunaliboresha hekalu la Roho Mtakatifu. Tukitumie kipindi cha Kwaresima mwaka huu kama fursa ya kujikumbusha mapokeo haya ya Kanisa na kiwe kipindi cha kuadhimisha na kung’amua huruma ya Mungu. Tukiyatenda matendo haya ya huruma tutakuwa tunadhihirisha huruma na upendo wa Mungu unaoendelezwa katika maisha yetu ya kila siku kupitia ukarimu wa kikristo. Huruma na upendo huenda pamoja.

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.