2016-03-07 06:59:00

Iweni na huruma kama Baba wa mbinguni!


Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la  Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 6 Machi 2016 amewaalika waamini kutafakari kwa kina mafundisho ya huruma ya Mungu yanayosimuliwa na Mwinjili Luka, katika sura 15: Kondoo aliyepotea, shilingi iliyopatikana na Baba mwenye huruma ambayo ndiyo Injili ya Jumapili ya nne ya Kipindi cha Kwaresima. Hapa mhusika mkuu ni Baba mwenye huruma akiwa na watoto wake wawili. Daima yuko tayari kusamehe na kusahau; ni Baba mwenye matumaini makubwa, mvumilivu na anayewapatia watoto wake uhuru hata kama anatambua madhara yake.

Baba mwenye huruma alithubutu kutoa urithi kwa mtoto wake mdogo, akitambua fika kwamba, huko njiani mambo si rahisi sana kama anavyodhani kijana huyu mdogo, huko atakiona che mtema kuni! Hivi ndivyo anavyotenda Mwenyezi Mungu kwa kumwachia mwanadamu uhuru wake kamili, zawadi ambayo anapaswa kutumia vyema. Kijana aliondoka machoni pa Baba yake kimwili, lakini bado moyoni mwake aliendelea kumsubiri ili aweze kurejea tena nyumbani. Siku moja akamwona akiwa mbali, akamkimbilia, akamkumbatia, akambusu na kumwonesha upendo wake.

Hivi ndivyo Baba mwenye huruma anavyotenda hata kwa kijana wake mkubwa, aliyebaki daima nyumbani kwa Baba, lakini sasa anasikitika na kupinga kitendo cha Baba yake kumfanyia sherehe mdogo wake aliyekosa na kutenda dhambi. Baba mwenye huruma anatambua na kumwambia kijana wake mkubwa kwamba, ilibidi kufanya sherehe kwani hatimaye, mdogo wake amerejea tena nyumbani. Pale mwamini anapojisikia kuwa si mali kitu mbele ya Mungu hapo ni mwanzo wa mchakato wa kukimbilia na kuambata huruma ya Mungu. Kwa yule anayejisikia kuwa ni mwema na mkamilifu, hapo ajue kwamba, hii ni tabia inayotoka kwa shetani na ni hatari kwa maisha ya kiroho.

Mwenyezi Mungu yuko tayari kuwahurumia na kuwasamehe wale wote wanaojisikia kuwa ni wadhambi. Katika mfano wa Baba mwenye huruma, kuna kijana wa tatu aliyeona kuwa sawa na Mungu si kitu cha kung’angania sana, akajinyenyekesha na kuwa sawa na mtumwa! Huyu ndiye Kristo Yesu kielelezo cha huruma, msamaha na upendo wa Mungu. Huyu ndiye aliyempokea, akamwosha mwana mpotevu na hatimaye kumfanyia sherehe ya msamaha. Yesu anawafundisha wafuasi wake kuwa na huruma kama Baba wa mbinguni!

Baba mwenye huruma anajifunua kwa namna ya pekee kwa njia ya Yesu Kristo anayeonesha upendo usiokuwa na mipaka; mwenye subira isiyokuwa na kifani, daima anasubiri kuwaona waja wake wakitubu na kumwongokea, tayari kuwakumbatia na kuwaonjesha huruma na upendo. Mwenyezi Mungu anaendelea kuwaona binadamu kuwa ni watoto wake hata pale wanakosa na kukengeuka; wanapokimbia na kutoweka mbele ya uso wake; anazungumza kwa upendo mkuu, hata pale ambapo waamini wanadhani kwamba ni wenye haki na watakatifu. Daima Mwenyezi Mungu ni mwaminifu na mwingi wa upendo. Kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho, mwamini anaweza kurudishiwa tena utu wake wa kuitwa mwana mpendwa wa Mungu, tayari kusimama na kuendelea tena na safari. Kipindi cha Kwaresima iwe ni fursa ya kuchuchumilia toba na wongofu wa ndani, ili kuona uso wa huruma ya Mungu na hatimaye kurejea kwake kwa mioyo yote bila kutumbukia tena kwenye dhambi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.