2016-03-07 12:10:00

Huruma ya Mungu katika Mafundisho ya Yesu!


Katika tafakari hii ya huruma ya Mungu tunaongozwa na Injili ya Luka 7:36-50: “Mfarisayo mmoja alimwalika Yesu kula chakula nyumbani kwake. Akaingia nyumbani mwa huyo Mfarisayo, akakaa kula chakula. Basi, katika mji ule kulikuwa na mama mmoja aliyekuwa anaishi maisha mabaya. Alipopata habari kwamba Yesu yuko nyumbani kwa huyo Mfarisayo, alichukua chupa ya alabasta yenye marashi.  Akaja, akasimama karibu na miguu yake Yesu, akilia, na machozi yake yakamdondokea Yesu miguuni. Huyo mwanamke akaipangusa miguu ya Yesu kwa nywele zake. Kisha akaibusu na kuipaka yale marashi. Yule Mfarisayo aliyemwalika Yesu alipoona hayo, akawaza moyoni mwake, "Kama mtu huyu angekuwa kweli nabii angejua huyu mwanamke ni wa namna gani, ya kwamba ni mwenye dhambi."

Yesu akamwambia huyo Mfarisayo, "Simoni, ninacho kitu cha kukwambia." Naye Simoni akamwambia, "Ndio Mwalimu, sema." Yesu akasema, Watu wawili walikuwa wamemkopa mtu fedha: mmoja alikuwa amekopa dinari mia tano, na mwingine hamsini. Waliposhindwa kulipa madeni yao, huyo mtu aliwasamehe wote wawili. Sasa ni yupi kati ya hao wawili atampenda zaidi huyo bwana?" Simoni akamjibu, "Ni dhahiri kwamba yule aliyesamehewa deni kubwa zaidi atampenda zaidi yule bwana." Yesu akamwambia, "Sawa." Halafu akamgeukia yule mwanamke na kumwambia Simoni, "Unamwona huyu mwanamke, sivyo?

Basi, mimi nilipoingia hapa nyumbani kwako hukunipa maji ya kunawa miguu yangu; lakini mwanamke huyu ameniosha miguu yangu kwa machozi yake na kunipangusa kwa nywele zake.  Wewe hukunisalimu kwa kunibusu, lakini huyu mwanamke tangu nilipoingia hapa amekuwa akiibusu miguu yangu. Wewe hukunionyesha ukarimu wako kwa kunipaka mafuta kichwani, lakini huyu mwanamke amefanya hivyo kwa kunipaka mafuta miguu yangu. Kwa hiyo nakwambia amesamehewa dhambi zake nyingi kwa kuwa ameonyesha upendo mkubwa. Mwenye kusamehe kidogo, hupenda kidogo." Basi, Yesu akamwambia yule mwanamke, "Umesamehewa dhambi zako." Na hapo wale waliokuwa pamoja naye mezani wakaulizana, "Ni mtu wa namna gani huyu awezaye kusamehe dhambi?" Naye Yesu akamwambia yule mwanamke, "Imani yako imekuokoa; nenda kwa amani.”

II – TAFAKARI

Simulizi la Bwana na wadeni wake wawili linatokea wakati Yesu alipokuwa amekaa mezani kwa Mfarisayo Simoni, wakati wa hafla iliyoandaliwa na Simoni kwa heshima ya Yesu. Mazingira haya yenyewe ya hafla hiyo ni kwazo kubwa kwa Wayahudi wa wakati ule. Yesu Myahudi alikuwa anawatembelea na kuchanganyikana na wanaume na wanawake wadhambi. Tena anajitwalia madaraka na mamlaka ya kuwaondolea dhambi, uwezo ambao alikuwa nao Mungu Mwenyezi peke yake! Tena uwezo huo ulikuwa unaratibiwa na makuhani wa Hekalu la Yerusalemu waliokuwa wanaweka taratibu za toba na matendo ya kiibada yaliyokuwa yanahitajika ili mdhambi apate kuondolewa dhambi zake na Mungu.

1. Upendo unaoaibisha:

Makaribisho aliyopata Yesu nyumbani kwa Simoni yanadhihirisha ukaribu wa pekee usio wa kawaida, ukaribu unaleta aibu. Wakati wa hafla iliyoandaliwa na Simoni kwa heshima ya Yesu, ghafula tunamwona mwanamke mwenye sifa mbaya katika mji ule, alijulikana kwa wote kwa ajili ya matendo yake. Bila kupiga hodi, bila kukaribishwa anaingia, anamwendea Yesu moja kwa moja, anamwangukia miguuni pake, anaiosha

kwa machozi yake, anafuta kwa nywele zake, anabusu miguu yake na kuirashia manukato. Vitendo vyake vinashangaza washiriki wote wa hafla hiyo na kuwakwaza. Wote wanamjua mwanamke huyo, na Simoni moyoni mwake humhukumu kuwa mdhambi. Lakini Simoni haelekezi mawazo yake kwa mwanamke huyo hasa, maana tayari amemhukumu kuwa mdhambi na anamfahamu kuwa mdhambi siku zote. Simoni  anamhukumu Yesu moyoni mwake. Inawezekanaje kwa mtu huyu ambaye watu humwona na kumheshimu kama nabii, inawezekanaje kwa Yesu huyo kumruhusu mwanamke mdhambi kumtia unajisi kwa kumshika na kumgusa? Kumbe, Yesu katika hekima yake na Maongozi ya Kimungu aliruhusu tukio hili litokee. Anataka kulitumia kama fundisho na mfano katika simulizi la bwana na wadeni wawili analotaka kuwashirikisha wasikilizaji wake, na kwa namna ya pekee kumpa mwenyeji wake - Simoni - fundisho zuri.

2. Bwana na wadeni wawili

Huruma ya Yesu kwa wadhambi ni wazi na ina maonjo yote ya huruma ya kibinadamu, tena huruma isiyotafuta sifa wala pongezi wala shukrani. Linalotokea baada ya mwanamke mdhambi kusamehemewa na Yesu dhambi zake kwa ajili ya kitendo chake hicho cha kuosha miguu yake kwa machozi na kufuta kwa nywele zake kilichoashiria toba yake na huzuni kwa ajili ya maisha yake ya dhambi - ni simulizi au mfano ambao Yesu anamua kuwashirikisha wote waliopo katika hafla bila kuashiria kwamba simulizi hili analilenga kwao moja kwa moja kama fundisho.

Kama ilivyo kawaida yake, Yesu hataji majina ya wale watu anaowasimulia. Badala yake anataka wasikilizaji walenge kiini cha simulizi au ujumbe wake. Mdeni wa kwanza anadaiwa dinari mia tano. Wa pili hamsini. Wa kwanza anadaiwa kiasi cha fedha mara kumi zaidi kuliko wa pili. Kwa thamani ya fedha za wakati ule wa Yesu, dinari mia tano ni sawa na mshahara wa kibarua kwa muda wa miaka miwili na nusu. Dinari hamsini ni kama mshahara wa miezi miwili na nusu. Wadeni wote wawili hawana uwezo wa kulipa deni kwa yule bwana anayewadai. Hivyo, bwana huyo anaamua kuwasamehe, wote wawili.

Katika simulizi la Yesu hakuna mazungumzo ya bwana na wadeni wake. Hawaongei kabisa. Bwana kwa hiari yake mwenyewe anaamua kuonyesha huruma yake na kuwasamehe madeni yao yote. Kiini cha simulizi hili ni neno - aliwasamehe. Na neno hili linakuwa msingi wa swali wa Yesu kwa Simoni - ni yupi kati ya wadaiwa hao wawili ambaye alimpenda bwana wake zaidi? Simoni lakini hajaelewa bado kwamba yeye ni sehemu ya simulizi hili. Anamjibu Yesu kwamba yule aliyesamehewa zaidi atampenda bwana wake zaidi. Simoni hajaelewa kwamba dhambi ya mwanadamu ni deni kwa Mungu. Tena ni deni ambalo Mungu mwenyewe anaweza kusamehe. Ni kwa neema ya Mungu tu tunasamehemwa dhambi zetu. Ni wazi kwamba Simoni hawezi kukubaliana nafsini mwake na tendo la Yesu la kumsamehe mwanamke mzinzi.

3. “Mwenye kusamehe kidogo, hupenda kidogo” (Lk 7:47​)

Hapo Yesu anafunua maana halisi ya simulizi lake. Simoni ndiye mdeni mwenye kudaiwa dinari hamsini. Ndiyo maana alimpenda Yesu kidogo tu. Hakumpa maji ya kuosha miguu alipofika nyumbani kwake, hakumkumbatia wala hakumbusu Yesu. Mwanamke mzinzi ni mdeni mwenye kudaiwa dinari mia tano. Ndiyo maana aliangukia miguu yake Yesu, akiibusu na kuosha kwa machozi yake na kufuta kwa nywele zake. Kwa nguvu zake mwenyewe asingeliweza kulipa deni la dhambi zake kwa Mungu. Ni kwa neema tu ya Mungu mwenye Huruma wote wawili - mwanamke na Simoni walisamehewa dhambi zao. Tafsiri ya kiswahili ya sentensi hii - “Kwa hiyo nakwambia amesamehewa dhambi zake nyingi kwa kuwa ameonyesha upendo mkubwa.” (mstari wa 48) - si sahihi. Inaleta hisia kwamba mwanamke amesamehewa dhambi zake kwa sababu alipenda sana.

Lakini dhana hii si sahihi. Katika lugha ya asili ya Injili ya Luka - kigiriki - imeandikwa hivi - “Kwa hiyo nakwambia amesamehewa dhambi zake nyingi na kwa sababu hiyo ameonyesha upendo mkubwa”. Mnaona utofauti wa maana ya sentensi hii? Kwa sababu ya kusamehewa dhambi zake nyingi akawa na upendo mwingi kwa Mungu. Neema isiyo na masharti ya Mungu mwenye Huruma ya kumsamehe kila dhambi ilimfanya mwanamke huyo ampende sana. Kisha Yesu anasema - “mwenye kusamehe kidogo, hupenda kidogo’. Yeyote ambaye hajaonja, hajafikiwa na Upendo huru wa Mungu hawezi kumpenda Mungu.

4. Ondoleo la dhambi na Imani inayookoa

Katika hafla nyumbani kwa Mfarisayo Simoni Yesu aliwakwaza wengi waliosemezana mioyoni mwao - "Ni mtu wa namna gani huyu awezaye kusamehe dhambi?” Swali hili linahitaji jibu ambalo linatokana na imani ya Wayahudi wa wakati ule kwamba ndiye Mungu aondoaye na kusamehe dhambi (taz. Lk 5:21). Na hata kama Mungu anasamehe dhambi, lakini bado dhambi hiyo inahitaji malipizi kadiri ya Sheria ya Dini ya Kiyahudi. Katika mtazamo wa washiriki wengi wa hafla Yesu amejitwalia mamlaka ya Mungu mwenyewe ya kusamehe dhambi. Kwao tendo hili ni kufuru kubwa sana. Lakini Yesu kwa kujitwalia madaraka ya kusamehe dhambi ya mwanamke mzingi anatenda kama Mungu anavyotenda - anamsamehe kwa sababu ya imani yake katika uwezo wa Yesu wa kuondoa na kusamehe dhambi.

Asingelikuwa na imani hiyo, asingelihangaikia kumfikia Yesu, na kabla ya hapo kwenda kununua manukato kwa gharama kubwa na kupita vikwazo vyote hadi alipomfikia Yesu na kumwangukia miguuni pake. Kwa sababu ya imani yake hiyo kubwa sana, Yesu aliweza kumsamehe dhambi zake zote. Imani ni sharti la pekee linalodaiwa na Yesu kwa mtu yeyote aweze kuponywa na kusamehewa dhambi zake. Katika miujiza yote ya Yesu, imani ni msingi na ufunguo wa miujiza hiyo. "Imani yako imekuokoa; nenda kwa amani.”

Yatokanayo ya simulizi kwa ajili yetu ni yapi? Tusome na kutafakari simulizi jingine la mfalme wa watumishi wawe wawili – wadeni wake. Tusome Injili ya Mathayo, sura ya 18, mstari wa 23 hadi wa 35. “23 Ndiyo maana Ufalme wa mbinguni umefanana na mfalme mmoja aliyeamua kukagua hesabu za watumishi wake. Ukaguzi ulipoanza, akaletewa mtu mmoja  aliyekuwa na deni la fedha talanta elfu kumi. Mtu huyo hakuwa na chochote cha kulipa; hivyo bwana wake aliamuru wauzwe, yeye, mke wake, watoto wake na vitu vyote alivyokuwa navyo, ili deni lilipwe. Basi, huyo mtumishi akapiga magoti mbele yake, akasema, Unisubiri nami nitakulipa deni lote.

Yule bwana alimwonea huruma, akamsamehe lile deni, akamwacha aende zake. Lakini huyo mtumishi akaondoka, akamkuta mmoja wa watumishi wenzake aliyekuwa na deni lake fedha denari mia moja. Akamkamata, akamkaba koo akisema, Lipa deni lako! Huyo mtumishi mwenzake akapiga magoti, akamwomba, Unisubiri nami nitalipa deni langu lote. Lakini yeye hakutaka, bali alimtia gerezani mpaka hapo atakapolipa lile deni. Basi, watumishi wenzake walipoona jambo hilo walisikitika sana, wakaenda kumpasha habari bwana wao juu ya mambo hayo yaliyotukia.  Hapo yule bwana alimwita huyo mtumishi, akamwambia, Wewe ni mtumishi mbaya sana! Uliniomba, nami nikakusamehe deni lako lote.  

Je, haikukupasa nawe kumhurumia mtumishi mwenzako kama nilivyokuhurumia? Basi, huyo bwana alikasirika sana, akamtoa huyo mtumishi aadhibiwe mpaka hapo atakapolipa deni lote. 35 Na baba yangu aliye mbinguni atawafanyieni vivyo hivyo kama kila mmoja wenu hatamsamehe ndugu yake kwa moyo wake wote." Tunamwona hapa mfalme na wadeni wawili. Sawa sawa na simulizi la bwana na wadeni wawili tunalotafakari leo. Mdeni wa kwanza anadaiwa talanta elfu kumi. Mdeni wa pili anadaiwa na mdeni wa kwanza dinari mia moja tu. Mfalme kwa huruma yake anamsamehe mdeni wa kwanza deni lake lote ambalo kwa vyovyote vile asingeliweza kulilipa maana lilikuwa kubwa mno.

Kwa hesabu za sasa, talanta elfu kumi ni sawa na dinari milioni kumi (talanta moja ni dinari elfu kumi) - ni kiasi ambacho haiwezekani kulipa katika maisha ya kibinadamu! Mdeni wa kwanza aliposamehewa deni kubwa hili hakuwa tayari kumsamehe mdeni wake dinari mia moja tu - kiasi ambacho angeweza kulipa kwa kazi ya miezi sita tu. Mfalme aliposikia hayo, alishikwa na hasira na kumwita mdeni wake aliyesamehewa talanta hizo zote elfu kumi. Akamwambia - “Wewe ni mtumishi mbaya sana! Uliniomba, nami nikakusamehe deni lako lote. Je, haikukupasa nawe kumhurumia mtumishi mwenzako kama nilivyokuhurumia?” (Mt 18:33) Mtumishi aliyesamehewa deni lake lote likarudishwa, mwenyewe katupwa jela hadi alipe deni lote, jambo ambalo haliwezekani. Hivyo - kwa kifupi - mtumishi huyo alihukumiwa maisha, au zaidi - umilele wote. Hitimisho la simulizi hili linatisha - “Na baba yangu aliye mbinguni atawafanyieni vivyo hivyo kama kila mmoja wenu hatamsamehe ndugu yake kwa moyo wake wote.” (Mt.18:35) Sisi ni Kanisa ambalo limejaa watumishi wa Mungu ambao wamesamehewa wingi wa dhambi zao zisizohesabika. Na kwa sababu Huruma hiyo ya Mungu tunapaswa kusameheana sisi wenyewe makosa yetu yote.

Je, inawezekana basi kuweka mipaka kwa Huruma ya Mungu wakati tumeambiwa kuwasamehe waliotukosa saba mara sabini au bora - kila wakati? Ni lini tutakapoelewa kwamba Huruma ya Mungu si haki yetu bali ni neema huru tunayopewa na Mungu katika uhuru wake wote nasi tunapaswa kuwahurumia wengine si kwa sababu ni haki yetu - hivyo tunaweza kuwanyima wengine au kuwapa masharti au kuwasumbua – bali kwa ni kwamba ni zawadi tunayopewa bure na Mungu na tunapaswa kuwapasha wengine bure? Katika nafsi ya Yesu, Huruma ya Mungu hukubali kuchafuliwa, kunajisiwa na hali yetu duni. Yesu huokoa hali hiyo duni ya maisha yetu ya dhambi kwa upendo wake usio na masharti wala mipaka.

Katika Injili zote hakuna sehemu nyingine kama tukio hili tunalilotafakari leo - la ukaribu wa kimwili wa pekee wa mdhambi na Yesu. Mwanamke mdhambi na mzinifu anaruhusiwa na Yesu kumgusa, kumbusu miguu yake, kuosha kwa machozi yake, kufuta kwa nywele zake. Hakuna mtu mwingine katika Injili zote aliyeruhusiwa kuwa karibu na Yesu kiasi hicho. Hata Mama yake mwenyewe! Huruma ya Yesu huokoa si kwa kupishana na taabu na dhiki na hali yetu duni ya dhambi, kwa kutazama kwa mbali au kutuhurumia kwa maneno tu, ama kwa kuguswa tu kidogo -bali kwa kukubali kunajisiwa kabisa kwa karibu sana na hali yetu ya dhambi.

Na Padre Wojciech Adam Koscielniak.

Kituo cha Hija Kiabakari, Jimbo Katoliki Musoma.








All the contents on this site are copyrighted ©.