2016-03-07 10:34:00

Benjamini William Mkapa na mchakato wa amani Burundi


Jumuiya ya Afrika Mashariki, EAC, hivi karibuni imemteua Rais mstaafu Benjamini William Mkapa wa Tanzania kuwa msuluishi mpya wa mgogoro wa kisiasa na kijamii nchini Burundi unaoendea kutokota nchini humo kwa takribani mwaka mmoja sasa. Hizi ni juhudi zinazofanywa na Jumuiya ya Kimataifa kama sehemu ya mchakato wa kutafuta suluhu ya amani ili Burundi isitumbukie tena kwenye vita ya wenyewe kwa wenyewe, tishio ambalo kwa sasa liko mbele ya macho ya wengi!

Dhamana ya Rais mstaafu Benjamini William Mkapa itakuwa na kuanzisha tena mchakato wa majadiliano ya kisiasa kati ya Serikali na Wapinzani, ili kuepuka mashambulizi, mateso na mahangaiko ya wananchi wa Burundi. Atakuwa na wajibu wa kuangalia uvunjwaji wa haki msingi za binadamu nchini Burundi. Uteuzi huu umeridhiwa na Rais John Pombe Magufuli wa Tanzania ambaye hivi karibuni ameteuliwa kuwa ni Mwenyekiti mpya wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika mkutano wake uliokuwa unafanyika Jijini Arusha, Tanzania.

Mkutano huu umehudhuriwa na viongozi wakuu wa nchi za Afrika Mashariki kutoka Uganda, Kenya, Rwanda na Mwenyeji wake Tanzania. Rais mstaafu Benjamini Mkapa atashirikiana kwa karibu na Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda, ili kuhakikisha kwamba, amani, usalama na utulivu vinarejeshwa tena nchini Burundi. Ni matumaini ya wapenda amani duniani kwamba, Serikali ya Burundi itaridhia juhudi hizi za Jumuiya ya Kimataifa za kutaka kuanzisha tena mchakato wa majadiliano na wapinzani, katika misingi ya ukweli na uwazi, ustawi na maendeleo ya wananchi wa Burundi.

Juhudi hizi zinaendelea kuhimizwa na Baraza la Makanisa Ulimwenguni pamoja na Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Ban Ki-Moon pamoja na Umoja wa Afrika. Bila utashi wa kisiasa kutoka kwa Serikali ya Burundi, juhudi zote hizi zitagonga mwamba na wananchi wataendelea kutumbukia katika maafa makubwa hatari hata kwa nchi jirani na Burundi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.