2016-03-05 15:21:00

Padre Wojciech: Mmissionari wa huruma ya Mungu nchini Tanzania!


Katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa huruma ya Mungu, Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano ya majivu aliwapatia wamissionari wa huruma ya Mungu dhamana na wajibu wa kwenda sehemu mbali mbali za dunia ili kuwashirisha watu Fumbo la huruma ya Mungu, kiini cha maisha na utume wa Kanisa kwa kuwaondolea watu dhambi ambazo kimsingi zinaondlewa tu na Kiti cha kitume pekee, ili upana wa utume wao uweze kuonekana wazi zaidi.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, hawa ni Wamissionari wa huruma kwani watakuwa ni ishala wazi ya huruma ya Baba wa milele kwa binadamu anayetafuta msamaha. Ni Wamissionari wa huruma kwa sababu ni wawezeshaji na wahamasishaji wa mkutano uliojaa ubinadamu, chimbuko la wokovu, changamoto ya kuanza upya pamoja na Kristo kwa kuambata neema ya Sakramenti ya Ubatizo.

Katika mahojiano maalum na Radio Vatican, Padre Wojciech Adam Koscielniak, mmissionari wa huruma ya Mungu anayefanya kazi na utume wake Parokia ya Kiabakari, Jimbo Katoliki la Musoma anaelezea historia fupi ya maisha na utume wake Jimboni Musoma. Lakini anafafanua zaidi umuhimu wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa kutambua kwamba, Mapadre ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu, waliokabidhiwa dhamana ya kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa yanayowakirimia waamini huruma ya Mungu. Hizi ni Sakramenti za Ekaristi Takatifu, lakini kwa namna ya pekee kabisa Sakramenti ya Upatanisho.

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, Wamissionari wa huruma ya Mungu watawapatia waamini matumaini mapya kwa kuwaondolea dhambi zao; kwa kuhubiri kuhusu wema, upendo, huruma na msamaha wa Mungu usiokuwa na kifani. Waamini wanakumbushwa kwamba, upendo wa Mungu ni mkubwa kuliko hata dhambi na mapungufu ya binadamu.

Huu ni ujumbe wa matumaini unaopaswa kumwilishwa katika huduma za maisha ya kiroho, kwa njia ya maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa; Semina, Warsha na Mafungo pamoja na mialiko kutoka kwa Maaskofu wa Makanisa mahalia ambao wanahimizwa kwa namna ya pekee na Baba Mtakatifu Francisko kutoa mwaliko kwa Wamissionari wa huruma ili kwanza kabisa wawe ni wahubiri na washawishi wa huruma. Wamissionari hawa wanapswa kuwa kweli ni watangazaji na mashuhuda wa furaha ya msamaha.

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kutoa wito na mwaliko kwa Kanisa ili kueneza huruma ya Mungu. Wamissionari wa huruma ya Mungu kwanza kabisa wanapaswa kutambua kwamba, wanapaswa kutafuta na kuambata huruma katika maisha yao, ili waweze kuzama katika bahari ya huruma ya Mungu inayoshuhudiwa katika maisha yao ya kila siku. Padre Wojciech Adam Koscielniak anamshukuru Mungu pamoja na shughuli za kusimamia  Kituo cha Hija Kiabakari, Jimbo Katoliki Musoma, lakini amekwisha pata mialiko kutoka kwa Maaskofu na makundi kadhaa ya familia ya Mungu nchini Tanzania, wanaotaka kufahamua zaidi kuhusu huruma ya Mungu, ili hatimaye, waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu katika maisha yao ya kila siku!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.