2016-03-05 16:14:00

Migogoro ya ardhi Tanzania kupatiwa ufumbuzi wa kudumu!


Waziri mkuu wa Tanzania Kassim M. Majaliwa amesema atawatuma mawaziri watatu waje mkoa wa Simiyu ili wakae na uongozi wa kila wilaya pamoja na wananchi ili kubaini tatizo la mipaka baina ya wilaya hizo na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.  Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo Jumamosi, Machi 5, 2016) wakati akizungumza na mamia ya wakazi wa vijiji vya Mwakaluba na Mwandoya akiwa kwenye siku ya tano ya ziara yake mkoani Simiyu.

"Tangu niingie hapa mkoani malalamiko ya mipaka nimeyapokea kila mahali nilikopita. Nimeamua kuwatuma mawaziri watatu ambao ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Bw. William Lukuvi; Waziri wa Maliasili ua Utalii, Profesa Jumanne Maghembe na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (TAMISEMI), Bw. George Simbachawene waje mkoa huu kutatua matatizo yenu," alisema.

"...Nitawatuma waje na wapite kila wilaya, wakae na kuzungumza na wakulima na wafugaji ili kubaini ni chanzo cha tatizo la migogoro hii kwenye mipaka ya vijiji na hifadhi ya Serengeti. Pia Waziri wa TAMISEMI itabidi atoe ufafanuzi kuhusu agizo lao la kutofanya shughuli yoyote mita 60 kutoka kwenye mto Simiyu ili wananchi waelewe," alisema.

Mapema, Mbunge wa Kisesa ambaye pia ni Naibu Waziri wa Nchi (OMR - Mazingira) alimweleza waziri Mkuu mbele ya wananchi hao kwamba limetolewa zuio linalowakata wakazi wa mkoa huo wasifanye shughuli zozote umbali wa mita 60 kutoka kwenye kingo za mto huo. "Limebandikwa tangazo linalokataza wananchi waishio kando ya mto Simiyu wasifanye chochote kuanzia Julai 30, 2016. Wananchi hawajashirikishwa wala kuelezwa chochote zaidi ya kuona bango la matangazo tu. Watu wananakatazwa wasichote maji wala kunywesha mifugo wakati hakuna mabwawa, itawezekanaje? Tunaomba kauli yako kuhusu jambo hili," alisema. Ili kumaliza tatizo la migogoro ya ardhi hapa nchini, Waziri Mkuu alisema Serikali ina mpango wa kuunda mabaraza ya ardhi 100 kwa nchi nzima ambayo yatakuwa na jukumu la kutatua migogoro ya ardhi kwa wakati.

Akitoa taarifa ya wilaya hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Meatu, Bw. Erasto Sima alisema wilaya hiyo iliyoanzishwa Julai mosi, 1987 ina ukubwa wa kilometa za mraba 8,835 ambapo asilimia 49 (sawa na kilometa za mraba 4,329) ya eneo lote la wilaya hiyo ni hifadhi za wanyamapori. Alilitaja eneo hilo kuwa ni pori la akiba la Maswa, sehemu ya hifadhi ya Serengeti, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na pori la hifadhi ya usimamizi wa wanyama (WMA) la Makao na kwamba asilimia 51 iliyobakia ndiyo inayotumiwa kwa makazi ya watu, kilimo na malisho ya mifugo.

MAJALIWA: MTU AKIHARIBU KAZI ASITARAJIE UHAMISHO!

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema watumishi wa umma wako huru kuhamia kokote wapendako lakini wahakikishe wanaenda huko wakiwa safi na kamwe mtu asiharibu kazi kazi akitarajia kuwa atahamishiwa sehemu nyingine. "Serikali hii haina utumishi kwa mtu aliyeharibu kazi. Usije ukaharbu hapa Itilima ukadhani utaenda Bunda kuendelea na kazi. Serikali ya awamu hii haina nafasi na watumishi wa aina hiyo," amesema.

Waziri Mkuu ametoa onyo hilo Ijumaa, Machi 4, 2016 wakati akizungumza na watumishi wa wilaya ya Itilima kwenye ukumbi wa Halmashauri ya wilaya hiyo ambao ameuzindua leo hii wilayani Itilima, mkoani Simiyu. "Watumishi wenzangu huu ni wakati wa kubadilika na kuona mwelekeo wa Serikali hii ya awamu ya tano ukoje. Jukumu letu ni kuwatumikia Watanzania wote bila kujali itikadi zao, rangi wala dini zao," alisisitiza.

Waziri Mkuu aliwahakikishia watumishi hao kwamba Serikali inatambua changamoto walizonazo kutokana na upya wa wilaya hiyo na mkoa huo na akawaahidi kuwa itaboresha mazingira yenu. "Msiwaadhibu wananchi kwa kisingizio cha mazingira magumu ya kazi zenu, tunajua mnayo madai ya nauli, posho za mafunzo, kupandishwa madaraja na malimbikizo ya likizo," alisema huku akishangiliwa. Alisema Serikali itayalipa madeni hayo japo haitamaliza yote kwa wakati mmoja ila ana uhakika wa kukamilisha walau kwa asilimia 80.

Mapema, akitoa taarifa ya wilaya hiyo, Mkuu wa wilaya hiyo, Bibi Georgina Bundala alisema wilaya hiyo iliyoanzishwa Machi 2012 na kupata Halmashauri Julai 2013 haina kituo cha Polisi cha wilaya, haina gereza, Ofisi za TAKUKURU, Mahakama ya wilaya wala Benki. Alisema wilaya hiyo haina hospitali ya wilaya ila akabainisha kuwa wamekwishatenga eneo la ekari 30 kwa ajili ya ujenzi huo. "Pia tumekwishapima viwanja 123 na eneo la kujenga taasisi lenye ekari 143.8 limefanyiwa uthamini na fidia kukamilika," alisema.








All the contents on this site are copyrighted ©.