2016-03-05 12:00:00

Mashuhuda wa huruma ya Mungu


Kardinali Marc Ouellet, Rais wa Tume ya Kipapa Amerika ya Kusini anawaalika Wamissionari 9, 000 kutoka Hispania wanaotekeleza maisha na utume wao Amerika ya Kusini kutambua kwamba, wao ni walimu, mashuhuda na wamissionari wa huruma ya Mungu. Ni ukweli usioweza kufumbiwa macho kwamba, msamaha na upatanisho una nguvu zaidi kuliko hata vita, kinzani na mipasuko ya kijamii.

Hii ni sehemu ya ujumbe ambao Kardinali Ouellet anawaandikia wamissionari hawa wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wamissionari Amerika ya Kusini, inayoadhimishwa mwaka huu tarehe 6 Machi 2016 kwa kuongozwa na kauli mbiu “Mashuhuda wa huruma ya Mungu”. Wamissionari hawa ni wale waliotumwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania ili kusaidia mchakato wa Uinjilishaji huko Amerika ya Kusini.

Kauli mbiu ya mwaka huu inakwenda sanjari na changamoto zinazoendelea kutolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati huu wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Wamissionari wawe na ujasiri wa kujitoa bila ya kujibakiza kama wafuasi, mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu kati ya watu! Kardinali Marc Ouellet katika ujumbe wake anakaza kusema upendo wa huruma ya Mungu unasambaa na kuwaambata watu kwa njia neema ambayo ni msamaha, kiini cha ujumbe unaopaswa kumgusa kila mmissionari anayetekeleza dhamana na utume wake Amerika ya Kusini, ili hatimaye, Familia ya Mungu Amerika ya Kusini iweze kuguswa na upendo wa huruma ya Mungu katika hija ya maisha yake ya kila siku!

Upendo wa Mungu hauna mipaka na wala Mwenyezi Mungu hatarajii kurudishiwa chochote na binadamu baada ya kumwonjesha upendo. Mungu daima yuko tayari kusamehe na kusahau, pale waja wake wanapomwendea kwa moyo wa toba na wongofu wa ndani; na kwamba, yuko tayari kuwakumbatia na kuwaongoza kwenye uhuru wa kweli! Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ni mwaliko kwa wamissionari wote kupitia Lango la Huruma ya Mungu ambalo ni Kristo Yesu, kwa kujikita katika toba na wongofu wa ndani, tayari kujisadaka kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili ya huruma ya Mungu inayomwilishwa katika maisha na utume wa Kanisa.

Wamissionari wawe tayari kupokea upendo kamili kutoka kwa Mungu unao waganga na kuwaponya, hatimaye, kuwasamehe dhambi zao. Mang’amuzi haya ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu yanaujalia moyo amani na utulivu wa ndani; yanawawezesha wamissionari kusonga mbele kwa imani na matumaini mapya licha vizingiti na mapungufu ya kibinadamu yanayoweza kujitokeza katika mchakato wa Uinjilishaji.

Ni mang’amuzi yanayowajaza kwa namna ya pekee matumaini, nguvu na ujasiri wa kupambana na maisha pasi na kukata wala kukatishwa tamaa, ili hatimaye, waweze kuwa kweli ni mashuhuda wa huruma ya Mungu pale ambapo wanatoa huduma kwa wahitaji zaidi. Wamissionari waoneshe na kuonjesha upendo usiokuwa na mipaka kwa Mungu, Kanisa na jirani zao. Huu ni upendo unaovuka mipaka ya kijiografia, kijamii na kisiasa. Ni upendo unaokumbatia na kuwaunganisha watu. Wamissionari hawa wanapaswa kujikita katika kutangaza Neno la Mungu; kutoa Katekesi makini na huduma inayoonesha huruma ya upendo wa Mungu kwa waja wake.

Wamissionari hawa wawe wepesi kuwapokea na kuwakaribisha watu wa Mungu bila kuwawekea vikwazo wala vizingiti, ili wote waweze kuonja upendo wa Mungu unao samehe, tibu na kuokoa, ili kumpatia mwanadamu maana ya ndani kabisa ya maisha yake hapa duniani. Upendo wa Mungu uwe ni faraja kwa wale wanaoelemewa na upweke hasi; wanao ogelea katika mashaka na makwazo ya kifamilia; wanawake na wasichana wanaotumbukizwa katika biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo; watu wanaoteseka kutokana na athari za utamaduni wa kifo.

Litania hii ya mateso inawagusa pia watoto wasio onja upendo na huruma ya wazazi wao; watoto ambao hawana fursa ya kupata elimu ya msingi. Kuna kundi kubwa la wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta hifadhi na usalama wa maisha; watu wasiokuwa na fursa za ajira bila kuwasahau wanaoishi katika umaskini na magonjwa. Wote hawa wanapaswa kuonjeshwa huruma na upendo wa Mungu. Wamissionari hawa kwa mara nyingine tena wanakumbushwa kwamba, wao ni walimu wanaopaswa kuwafunda watu kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko; kwa kuwa karibu na watu, ili kuwaonjesha ukarimu na upendo.

Wawe tayari kutoa huduma ya Upatanisho kwa waamini wanaokimbilia kiti cha huruma ya Mungu, kwa kuwa ni mashuhuda na sauti ya kinabii inayosaidia kuleta marekebisho katika mafungamano ya maisha ya kijamii na kifamilia yanayoamsha ndani ya watu kiu ya kutafuta na kuambata ukweli, upendo na mahusiano bora ya kijamii. Mwishoni, wamissionari hawa wajiaminishe na kujiweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Huruma ya Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.