2016-03-05 14:03:00

Maisha Mchanganyiko : Wanawake katika ujenzi wa amani na maridhiano


Tunapoelekea katika adhimisho la Siku ya Wanawake Duniani, Jumanne ijayo  tarehe 8 Machi, Dunia Mama anapenda kwanza kabisa,  kuwapongeza wanawake wote duniani  kwa maumbile yao asilia yaliyojazwa upendo na fadhila kwa  binadamu wengine, huduma zisizoweza lipika , iwe ndani ya familia, au katika maisha ya kijamii, na hasa familia zetu za kiafrika ambamo walau bado wengi wanazingatia uadilifu kimaumbile .Kwa hakika  si rahisi kupata maneno yanayofaa kuuenzi moyo huo wa wanawake katika majitoleo na wema wao, ukweli unaoonekana wazi wakati wanapokosekana hata kwa  muda mfupi tu ndani ya familia.  

Kwa mtazamo huo, tunaalikwa katika tafakari hii, hasa tulenga katika umuhimu wao katika masuala ya  ujenzi wa amani,  mapatano na maridhiano miongoni mwa jamii.  Kwa nini tuelekeze mawazo yetu katika hili? Ni kutokana na ukweli kwamba, mahali popote  amani inapovurugwa,  wanawake ni wa  kwanza kuteswa na hali hiyo, kama inavyoonekana  wazi wazi  sasa huko Burundi na Syria kwamba , zaidi ya robo tatu ya picha za wakimbizi zinazoonyeshwa  ni  wanawake na watoto wao. Hivyo mwanamke anakuwa ni sura inayoonyesha  mahangaiko, ni sura ya matatizo, ni sura ya udhaifu wote unoweza kuletwa na binadamu.  Ni kweli hata wanaume  huonekana katika mahangaiko hayo , lakini  idadi kubwa ya wanaume hao , au ni wagonjwa au  wazee au wale wenye kuwa na udhaifu fulani kimwili.  .

Dunia Mama , katika kuchambua hali halisi za maisha ya kijamii, anasikitika kwamba,  mwanamke huyu mwenye kuubeba msalaba wote wa familia na jamii, nafasi yake katika masuala ya kijamii bado ni finye, na hasa katika ushirikishwaji wa kutoa maamuzi juu ya maisha yao na maisha ya jamii wanamoishi. Kumbe hili linaonyesha, bado kunahitajika bidii zaidi na zaidi  katika lengo la kuhakikisha ujenzi wa haki sawa kati ya jinsia hizi mbili , wanaume na wanawake, hoja inayoturejesha  kuyatazama mafundisho ya kanisa juu ya suala hili la usawa kati  ya jinsia  ya mke na mme.      Na tutazame mafundisho ya Waraka wa Kitume wa Papa Yohane Paulo 11, juu ya hadhi ya mwanamke ( "Murielis Dignitatem” ambamo kwa kirefu ametazama Maandiko Matakatifu yanasema nini juu ya usawa huu unaodaiwa  kati ya mwanamke na mwanaume, hasa  katika wakati huu wetu,  ambamo suala la haki za wanawake limekuwa likipewa uzito zaidi na zaidi katika mtazamo wa haki za binadamu.

Waraka wa Papa unaainisha kwamba , Maandiko Matakatifu,  Agano la Kale na Agano jipya, yanadumisha ukweli juu ya Muugano uliowekwa na Mungu kati ya watu hawa wawili mwanamke na mwanamme.  Hii ikiwa na maana kwamba , heshima  na utume wa kila mmoja wao ni matokeo ya utajiri wa utofauti  wao katika asili ya utu wao, kama mwanamke na  mwanaume.

Mtakatifu Yohane Paulo 11, anaendelea kuutazama usawa  kati ya mwanamke na mwanaume, akitazama kwa kina pia maneno na utendaji wa Yesu Kristo kwa wanawake  akisema, inathibitisha na kutoa ufafanua wazi na ukweli , kuhusu usawa wa mwanamke na mwanaume, kwamba mbele ya Mungu wote ni sawa tangu awali ,  mwanamke aliumbwa na Mungu kama ilivyokuwa kwa mwanamme,  wote waliumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Wote wawili wakiwa sawa katika kupokea  zawadi ya ukombozi uliotoka kwa Mungu kupitia mwanae Yesu Kristo na huimarisha katika  mwanga wa maisha ya  upendo na  Roho Mtakatifu. Na wote hutakatifushwa na kukamilishwa na upendo wa Mungu wa kuokoa unaotolewa bure kwa  jamii yote ya binadamu bila kujali mke au mme.  

Waraka wa Yohana Papa Paulo II, unaendelea kutuasa kwamba,  hata zile aya ambazo zimeandikwa katika Biblia kama  mwanamme atamtawala mwanamke , katika hali yoyote isitafasiriwe kama sharti la mwanamme kumgandamiza mwanamke.  Pia amewaonya wanawake wasitumie jina la kutafuta uhuru wao kwa  ubabe na majigamb o ya kijinga,  kwa kuwa kufanya hivyo ni kuwa  nje na mpango wa Mungu aliyewaumba  kwa  maumbile tofauti lakini katika usawa wa kiutu. Waraka huo unaendelea kututaka sisi binadamu  wa  nyakati hizi kuhifadhi ukweli  huo halisi wa utu sawa kati ya mwanamke au mwanaume.

Tunapaswa sote,  wake kwa waume, kusikiliza maneno ya Yesu na kutazama matendo yake , kwenye mahusiano haya ya kati ya  wanawake na wanaume  kama  msingi wa wazi zaidi, wenye kutuonyesha  usawa katika mahusiano,  hadhi na wito wa wanawake katika Kanisa na katika ulimwengu. Waraka unataja kila wito una maana  kubwa kibinafsi na kinabii. . Katika  kuitikia wito,  njia ya maisha binafsi ya mtu hujulikana  iwe kwa mwanamke au mwanamke , mwelekeo wa mtu katika kutimiza  Mapenzi ya Mungu.

Kwa sababu hiyo, kwa niaba ya  Kanisa, Papa Yohane Paulo 11, alitoa shukutani za dhati kwa kila mwanamke, katika hali yao tofauti na wanaume, kwa  wito na utume wao mbalimbali,  iwe kama mama wa familia, au  wale  walioyaweka maisha yao wakfu kwa Mungu katika ubikira;  pia kwa wanawake wanaofanya kazi za kitaaluma, nawale  ambao kwa wakati mwingine hulazimika kubeba mzigo mzito wa uwajibikaji  kijamii.  Kanisa linatambua wanawake kama ilivyo kwa wanaume , wote  wako katika hija ya maisha  hapa duniani, katika vyote mazuri na huzuni zote za dunia hii.

Aidha tunashukuru Mungu kwa juhudi zilizofanyika  katika kuelimisha umma juu ya usawa huu,   kwa kuwa  si tu kanisa lenye kutambua tunu za mwanamke katika maisha ya binadamu duniani  lakini hata vyombo vingine vya kijamii vinaendelea kukuza  utambuzi  kwamba tofauti za kimaumbile si sababu za mmoja kumnyanyasa au kumbagua mwingine kimaisha. Lakini tofauti hizo zinapaswa  kutajirisha  na kuyafanya maisha yawe na mvuto na kupendeza zaidi na zaidi  kwa kila mtu. 

Tafakari hii pia  inatukumbusha  kikao cha ngazi ya juu cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa , kilichofanyika Mwezi Octoba mwaka jana , ambacho kilitathimini utendaji wa azimio  namba 1325, katika kutimiza miaka kumi na mitano, ambayo ni  ajenda ya wajibu wa  wanawake katika udumishaji wa amani na usalama.  Kwa mara ya kwanza ajenda hiyo ilizungumzia kwa makini zaidi katika ngazi hiyo ya kimataifa kunako mwaka  2000, ambamo mlionyesha kutambuliwa kwa  nguvu zaidi ,  wajibu wa usawa wa kijinsia katika ajenda na uongozi  na hasa katika udumishaji wa amani na usalama hata katika  ngazi ya kimataifa. Mkutano wa mwezi Oktoba 2015, uliofanyika ikiwa imepita wiki chache tu kwa Umoja wa Mataifa kuadhimisha miaka 70 ya uwepo wake ,ambamo   Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, liliahidi kuwajibika na ujenzi wa usawa wa kijinsia kama kiini cha mikakati yote  ya kutengeneza ramani mpya , kwa ajili ya maendeleo duniani.

Tunashukuru Mungu kwamba, walau kumekuwa na mwamko kidogo , katika kuwahusisha wanawake kwenye utendaji  na maamuzi ya kijamii, kama ilivyoonyesha mwaka juzi 2014 kwamba ,  kwa karibia asilimia 88 ya taratibu zote za Umoja wa Mataifa  katika kujenga amani duniani , ziliweza washirikisha wanawake , ikionyesha ongezeko la  asimia 50 ikilinganishwa na mwaka 2011. Na  kabla ya kupitishwa kwa azimio namba 1325 , ushiriki wa wanawake katika kutoa maamuzi kwa hoja zilizohusiana na masuala ya amani ilikuwa ni asilimia 11tu.

Kwa sasa inajionyesha wazi kwamba, wanawake wanahitajika  kuwa wajumbe kamili katika hatua zote za majadiliano yanayolenga  kuleta amani na utulivu , pia katika juhudi za upatanishi. Aidha kuna umuhimu wa wanawake kupata haki ya kuwa wadhibiti wa rasilimali katika maeneo yao na hasa aridhi kwa kuwa wengi hujishughulisha na aridhi kwa manufaa ya familia nzima. Aidha ushiriki wao ni muhimu katika mazungumzo yanayotafuta kushinda matatizo na uchungu wa mizozo yenye kuzaa vita  au katika utendaji wotewote unaolenga kutoa ukarabati kwa mioyo iliyoumizwa, kwa kuwa suala hili hugusa maisha yao moja kwa moja.   

Aidha wito unatolewa wa kuunga mkono, Kitengo cha Wanawake katika Ofisi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Matafa, amb acho kinatoa  kilio kinachotafuta kuharakishwa  hatua zinazoweza fanikisha  wanawake kujiunga katika juhudi  zote zinazotafuta kujenga amani na usalama,  kwa moyo ulio thabiti zaidi kisiasa , na kwa ajili ya kuhimiza msaada wa kifedha na uwepo wa matumizi mazuri ya fedha zinazotolewa kama msaada kwa wahitaji.  

Tukumbuke,   kwa mwaka huu, adhimisho la Siku ya Kimataifa ya  wanawake , linaongozwa na Mada Mbiu : "Dunia ya  50-50 ifikapo 2030: harakisha usawa wa kijinsia.  Dunia Mama , inatualika wote kushiriki katika jitihada hizi za kuwa na usawa katika utendaji wote.  Lakini hii haina maana ya kutoheshimu tofauti za  kimaumbile kati ya mwanamme na mwanamke,  lakini usawa wenye kukamilisha mpango wa Mungu aliyeumba jinsia zote mbili kike na kiume kwa sura na mfano wake.

 Na tuyakumbuke  mafundisho ya Kanisa juu ya usawa katika utofauti wa kijinsia , tukiwa tumejawa na utambuzi kwamba,  sote wake kwa waume ni muhimu katika kuijenga dunia ya amani na salama mahali popote duniani.  Tunaalikwa  kuiadhimisha siku hii ya wanawake, kama  fursa  nyingine ya kuthibitisha umuhimu na ulazima wa uwepo  jinisia zote katika ya kila aina ya maisha ya  binadamu, bila ya mojakuigandamiza nyingine.  Na tuyakumbuke maneno ya Papa Francisko, ya  mwaka jana alimosema, dunia bila mwanamke ni  dunia tasa, si tu kwa sababu wanawake huleta maisha lakini kwa huduma yao na uwezo wao wa  kuona mbali , uwezo katika uelewa kupitia macho tofauti, moyo wao makini na bunifu zaidi katika kumhudumia binadamu mteswa na mnyonge . Mungu wabariki wanawake wote.

Imeandaliwa nami Tj Mhella
 








All the contents on this site are copyrighted ©.