2016-03-04 14:32:00

Wasindikizeni waamini kukimbilia huruma ya Mungu!


Baba Mtakatifu Francisko anaipongeza Idara ya Toba ya Kitume kwa kazi kubwa inayofanya kwa ajili ya kuwasaidia Mapadre kutekeleza vyema utume wao wa kuwaonjesha waamini huruma ya Mungu hususan wakati huu Kanisa linapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Idara hii imekamilisha kozi ya ishirini na saba inayopania kuwasaidia Mapadre wapya kuadhimisha vyema Sakramenti ya Upatanisho inyomfanya mtu aguse kwa mkono wake ukubwa wa huruma ya Mungu, chimbuko la amani ya ndani.

Baba Mtakatifu ameyasema haya Ijumaa, tarehe 4 Machi 2016 alipokutana na washiriki wa kozi maalum kuhusu Sakramenti ya Upatanisho iliyoandaliwa na Idara ya Toba ya Kitume kwa Mapadre waungamishaji. Imani ya Kikristo inapata muhtasari wake katika huruma ya Mungu ambayo ni hai, inaonekana na imefikia hitimisho lake kwa Kristo Yesu, kielelezo cha upendo wa Mungu anayetaka kila mwanadamu akombolewe, agano ambalo limefungwa kwa njia ya Damu Azizi ya Yesu na kwamba, huruma ya Mungu inaweza kuwafikia watu wote wanaoikimbilia.

Huruma ya Mungu anakaza kusema Baba Mtakatifu iko wazi kama malango matakatifu yanayogusa moyo wa Mungu anayependa na kufanya subira ili kuwapokea na kuwakumbatia tena wale waliotenda dhambi na kukimbia mbali na uwepo wake. Huruma ya Baba inaweza kuwafikia watu kwa kuwa na dhamiri nyofu; kusikiliza Neno la Mungu linaloongoa moyo wa mtu; kwa kukutana na watu wenye huruma; kwa kuguswa na mang’amuzi ya maisha yanayosimulia kuhusu madonda ya ndani; dhambi, msamaha na huruma ya Mungu.

Baba Mtakatifu anafafanua zaidi kwamba, njia ya wazi na iliyonyooka inayomhakikishia mwamini maondoleo na msamaha wa dhambi ni Yesu Kristo mwenye mamlaka ya kusamehe dhambi; utume ambao amelikabidhi Kanisa. Kumbe, Sakramenti ya Upatanisho ni mahali muafaka pa kuonja huruma ya Mungu na kuadhimisha sherehe ya kukutana na Baba wa milele. Mapadre waungamishaji wanapaswa kukumbuka kwamba, wao daima ni vyombo vya huruma ya Mungu, hivyo wanapaswa kuwa makini ili kamwe wasiwe ni vikwazo vya zawadi ya wokovu.

Waungamishaji watambue kwamba hata wao pia ni wadhambi na wanahamasishwa kukimbilia huruma ya Mungu; kwa kuonesha unyenyekevu wa imani na ukarimu, ili kweli mwamini anayekimbilia huruma ya Mungu aweze kugusa upendo wa Baba wa milele. Hapa waungamishaji wanakumbushwa kwamba, kuna watakatifu kama Leopoldo Mandic na Padre Pio wa Pierelcina waliojisadaka bila ya kujibakiza ili kuwagawia watu huruma na msamaha wa Mungu.

Mwamini baada ya kutubu na kupata maondoleo ya dhambi kwa njia ya imani anapaswa kuwa na uhakika kwamba, dhambi zake zimesamehewa kwa njia ya huruma ya Mungu, kielelezo cha Jubilei ya moyo inayowafurahisha waamini, Kanisa  lakini hata kwa Mwenyezi Mungu mwenyewe, kwani Maandiko Matakatifu yanasema kwamba, kuna furaha kubwa mbinguni kwa ajili ya mwenye dhambi mmoja atubuye, kuliko kwa ajili ya wenye haki tisini na kenda ambao hawana haja ya kutubu. Kumbe, waungamishaji wanapaswa kuwa njia ya furaha ili mwamini baada ya kupata ondoleo la dhambi aweze kufurahia matendo ya Mungu yaliyomwokoa, kwa kuishi katika hali ya shukrani, tayari kutimiza malipizi ya dhambi alizotenda na kuwaendea ndugu zake kwa moyo mwema unaowajibika.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, ulimwengu mamboleo umegubikwa kwa kiasi kikubwa na ubinafsi, madonda pamoja na kishawishi cha watu kutaka kujifungia katika undani wao, hivyo ni muhimu sana kuwasindikiza waamini wanaokimbilia kiti cha huruma ya Mungu, changamoto na mwaliko kwa waungamishaji kuwa mashuhuda amini wa Injili; watu wenye upendo wa kibaba kwani wao kimsingi ni walinzi wa Kondoo wa Kristo na wala si wamiliki wa kondoo wala neema ya Mungu.

Sakramenti ya Upatanisho inapaswa kupewa kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wa Kanisa si tu wakati huu wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, ili waamini na waungamishi waweze kweli kuonja upendo aminifu wa Mungu usiodanganya kamwe. Huu ni upendo unaovuka matarajio ya kibinadamu na kwamba, mbinguni kuna moyo mwema wa Mama Bikira Maria, ambaye alipokuwa chini ya Msalaba alionja mateso ya binadamu, kumbe, anaweza kuwafariji. Bikira Maria ni kimbilio la wakosefu, Mama wa huruma ya Mungu, awaongoze na kuwaimarisha katika utume wa Upatanisho ambao kimsingi ni njia ya huruma ya Mungu na kwa namna ya pekee katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.