2016-03-04 14:44:00

Uinjilishaji ujikite katika ushuhuda wa Neno la Mungu!


Mama Kanisa anatambua kwamba, mhusika mkuu katika mchakato wa Uinjilishaji ni Roho Mtakatifu; dhamana ambayo inapaswa kutekelezwa kwa njia ya ushuhuda wa maneno na matendo, kielelezo makini cha imani tendaji. Wainjilishaji watambue kwamba, wameitwa na Mwenyezi Mungu ili kushiriki kikamilifu katika azma ya Uinjilishaji inayopaswa kutekelezwa kwa upendo mkuu. Haya ndiyo mawazo makuu yaliyofafanuliwa na Padre Raniero Cantalamessa, Ijumaa tarehe 4 Machi 2016 wakati wa mahubiri yake ya tatu kwa Baba Mtakatifu na wasaidizi wake wa karibu kama sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Fumbo la Pasaka, kielelezo cha huruma ya Mungu.

Itakumbukwa kwamba, kipindi hiki Padre Cantalamessa anatafakari kuhusu umuhimu wa maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican katika maisha ya kiroho, kwa kuchambua baadhi ya nyaraka zilizotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Akizungumzia juu ya Waraka wa Ufunuo wa Kimungu, Dei Verbum, maarufu kama Neno la Mungu anasema, huu ni mwaliko wa kulipokea, kulitafakari na kulimwilisha katika uhalisia wa maisha ya watu. Mwenyeheri Paulo VI akauboresha Waraka huu kwa kukazia umuhimu wa “Kutangaza Injili” “Evangelii nuntiandi”, Mtakatifu Yohane Paulo II akakazia kuhusu “Utume wa Ukombozi” “Redemptoris missio” na sasa Papa Francisko anakazia umuhimu wa kushuhudia Injili ya furaha, “Evangelii gaudium”.

Padre Cantalamessa anasema kwamba, mhusika mkuu wa utume wa Uinjilishaji ni Roho Mtakatifu na ujumbe ni Neno la Mungu linalopaswa kutangazwa na kushuhudiwa kwa njia mbali mbali za vyombo vya mawasiliano ya jamii kwa kutambua kwamba, Neno la Mungu ni roho na uzima. Mitume wa Yesu waliagizwa kwenda duniani kote ili kutangaza na kushuhudia Neno la Mungu kwa watu wa mataifa baada ya kumpokea Roho Mtakatifu.

Mpango huu wa ufunuo hutimizwa kwa matukio na maneno ambayo yameunganishwa kwa ndani kabisa, kiasi kwamba kazi zilizotimizwa na Mungu katika historia ya wokovu zinaonesha na kuthibitisha mafundisho na yale yote yaliyomo katika maneno; na maneno yanatangaza kazi na kuliangaza Fumbo lililomo ndani yake. Hapa waamini wanaalikwa kuwa ni mashuhuda wa Neno la Mungu linalomwilishwa katika uhalisia wa maisha, kwani matendo yana mvuto na mashiko kuliko maneno matupu! Bikira Maria ni nyota ya Uinjilishaji kwani alimbeba Neno wa Mungu aliyefanyika mwili na kukaa kati ya watu wake, akawa ni chachu ya Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia.

Wainjilishaji watambue kwamba, wanateuliwa na kutumwa na Mungu ili kutangaza na kushuhudia Neno lake kwa watu wa mataifa kama ilivyokuwa kwa Abrahamu, Manabii, Mitume na sasa dhamana hii inawawajibisha Wakristo wote waliompokea Roho Mtakatifu kwa njia ya Ubatizo, ili wasiishi tena kwa ajili yao wenyewe, bali kwa ajili yake yeye aliyekufa na kufufuka kwa wafu. Wakristo waondokane na kishawishi cha uvivu kwa kudhani kwamba kuna wengine watawafanyia kazi hii, bali wao ni kuendelea “kula bata” kama wanavyosema Waswahili. Wakristo washiriki kwa hali na mali; kwa sala na sadaka zao ili kufanikisha mchakato wa Uinjilishaji unaopaswa kuwa ni matunda ya tafakari ya kina na sala inayomwilishwa katika ushuhuda wa Uinjilishaji.

Padre Cantalamessa anakaza kusema, mchakato wa Uinjilishaji unajikita katika ushuhuda wa upendo, kielelezo makini cha imani tendaji. Kuna vikwazo na vizingiti kama ilivyokuwa kwa Yona alipotumwa kwenda kuhubiri Ninawi. Upendo ushuhudiwe kwa wale wanaotangaziwa Habari Njema ya Wokovu na kwa Kristo na Kanisa lake.

Kwa ufupi, Injili inapaswa kutangazwa kwa njia ya ushuhuda wa maisha yenye mvuto na mashiko kwa watu, ili wale wanaotangaziwa Injili waone na kuonja utukufu wa Kristo unaojaza nyoyo zao. Wainjilishaji watekeleze dhamana hii kwa unyenyekevu kwa kutambua kwamba, Roho Mtakatifu ndiye mhusika mkuu wa utume wa Uinjilishaji unaopaswa kujikita katika ushuhuda wa maisha, chemchemi ya furaha na utukufu wa Kristo katika mioyo ya watu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.