2016-03-04 07:47:00

Sakramenti ya Upatanisho ni dawa tosha ya magonjwa ya kiroho na kimwili


Baraza la Maaskofu Katoliki Malta katika ujumbe wake kwa Kipindi cha Kwaresima sanjari na maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu linakumbusha kwamba, hakuna ugonjwa usioweza kutibiwa na Kristo Yesu, jambo la msingi ni waamini kujiweka wazi mbele ya Kristo kwani Yeye analo Neno la uzima. “Kristo ni dawa ya magonjwa yetu” ndiyo kauli inayoongoza ujumbe wa Kwaresima kutoka kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Malta.

Magonjwa haya ni yale yanayomsibu mwanadamu kiroho na kimwili; magonjwa ambayo wakati mwingine yanasababisha mahusiano ya watu kulega lega kwa kuanzia katika familia ambalo ni Kanisa dogo la nyumbani, shule ya upendo, haki, amani na ukarimu. Haya ni magonjwa yanayojikita pia katika mmong’onyoko wa kimaadili na utu wema; magonjwa ambayo kwa sasa yamekuwa na athari kubwa katika ustawi na maendeleo ya wengi, kiasi hata cha kuwafanya watu kuwa mbali na Mwenyezi Mungu.

Magonjwa haya ya kiroho na kimwili yanayojaza mioyo ya watu uchungu na masikitiko makubwa, kiasi hata cha kuwafanya watu wengi kutumbukia katika ubinafsi ambao ni hatari kubwa zaidi kwani watu wengine wanawakimbia na kuwakwepa wanapowaona wakiwa katika mazingira kama haya! Baraza la Maaskofu Katoliki Malta linakumbusha kwamba, Wakristo hawana kinga thabiti juu ya magonjwa haya ya kijamii.

Kumbe, wanaalikwa kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Paulo aliyekirimiwa na waamini wa Malta akiwa njiani kuelekea Roma, akaonesha umahiri wa kuganga na kuponya roho za watu, anaendelea kuwahamasisha waamini kumkimbilia Kristo kwa moyo wa imani na matumaini, ili aweze kuwaganga na kuwaponya kutokana na magonjwa yanayoendelea kuwaandama katika maisha ya kiroho na kimwili!

Maaskofu Katoliki Malta wanafafanua umuhimu wa utume wa Mapadre katika Sakramenti ya Upatanisho, inayomwonjesha mwamini huruma, upendo na msamaha wa Mungu. Si kazi ya Mapadre kulaani wala kuhukumu, bali kutoa msamaha na huruma ya Mungu kwa niaba ya Kanisa, wakitambua kwamba, mhusika mkuu ni Kristo mwenyewe. Mapadre wawanyooshee mikono na kuwaombea wagonjwa, ili Mungu aweze kuwasamehe dhambi zao.

Mapadre wanakumbushwa kwamba, Kanisa ni kama hospitali iliyoko kwenye uwanja wa vita inayowapokea majeruhi na wagonjwa wa kila aina. Hii ndiyo dhana ya Kanisa analopendekeza Baba Mtakatifu Francisko wakati huu wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, Kanisa ambalo lina uwezo wa kuwakumbatia wote, ili kuwaonjesha huruma na upendo wa Mungu. Waamini kwa upande wao pia waoneshe ari na moyo wa unyenyekevu wa kutaka kukimbilia kwenye kiti cha huruma ya Mungu.

Kanisa lioneshe upendo na huruma kwa waamini wanaoogelea katika kinzani na misigano ya maisha ya ndoa na familia, ili wasikate tamaa katika maisha na utume wa Kanisa, daima wawe na ujasiri wa kumkimbilia Kristo, ili awajalie neema na baraka ya kuanza tena upya katika maisha yao ya kiroho na kimwili. Waamini wanakumbushwa kwamba, ni kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho wanaweza kuonja na kuambata huruma, msamaha na upendo wa Mungu. Maondoleo ya dhambi ni dawa makini inayomwezesha mwamini kuanza tena mchakato wa uponyaji wa ndani. Kwaresima iwe ni fursa ya kukimbilia na kuambata huruma, msamaha na uponyaji wa Mungu katika magonjwa sugu yanayomwandama mwanadamu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.