2016-03-04 06:41:00

Kanisa lina mchango mkubwa katika maendeleo ya watu Timor ya Mashariki


Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 3 Machi 2016 amekutana na kuzungumza na Bwana Rui Maria de Araùjo, Waziri mkuuwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Timor ya Mashariki ambaye baadaye amekutana pia na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameandamana na Monsinyo Antoine Camilleri; Katibu mkuu msaidizi wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican.

Baba Mtakatifu na mgeni wake katika mazungumzo yao, wameridhika na mahusiano mazuri yaliyopo kati ya pande hizi mbili sanjari na mchango wa Kanisa katika ujenzi wa Timor ya Mashariki, hususan katika sekta ya  elimu, afya na mapambano dhidi ya umaskini. Baada ya mazungumzo haya, ujumbe wa Vatican na Timor ya Mashariki ulibadilishana nyaraka za kuridhia itifaki ya makubaliano iliyotiwa sahihi huko Dìli tarehe 14 Agosti 2015.

Itifaki hii ina utangulizi pamoja na vipengele 26 vinavyotambua kisheria viongozi wa Kanisa na taasisi zake pamoja na kutoa uhuru kamili kwa Kanisa kuweza kutekeleza utume wake kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi wa Timor ya Mashariki kiroho na kimwili.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.