2016-03-04 15:07:00

Jumuiya ya kiekumene ya Taizè na mikakati yake!


Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 3 Machi 2016 amekutana na kuzungumza na Fra Alois, mkuu wa Jumuiya ya Kiekumene ya Taizè ambaye kwa sasa yuko mjini Roma kwa shughuli maalum. Katika mazungumzo yake na Fra Alois, wamegusia pamoja na mambo mengine: ukarimu kwa vijana wa Taizè; mikutano ya kimataifa inayoandaliwa na Jumuiya hii sehemu mbali mbali duniani pamoja na mchakato wa umoja kati ya Makanisa.

Katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, Jumuiya ya Taizè inaendelea kujikita katika sala, ili kuombea mafanikio mema katika maadhimisho haya, ili kweli yaweze kuwa ni chachu ya toba na wongofu wa ndani, tayari kuambata huruma na upendo wa Mungu unaotolewa bure kwa watu wote. Fra Alois amekuwa akifuatilia pia maisha na utume wa wanachama wa Jumuiya ya Taizè wanaoishi mjini Roma.

Jumuiya ya Taizè imekuwa pia mstari wa mbele kuwahamasisha viongozi wa Jumuiya ya Ulaya kuonesha ukarimu kwa wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta hifadhi na usalama wa maisha Barani Ulaya badala ya kugubikwa na woga na wasi wasi usiokuwa na mashiko wala mvuto. Katika maadhimisho ya Fumbo la Pasaka, vijana wa Jumuiya ya Taizè wapatao 8, 000 watakwenda mjini Bucarest, Romania ili kuungana na Wakristo wengine kusherekea Fumbo la huruma na upendo wa Mungu kwa mwanadamu. Kwa namna ya pekee, vijana wa Taizè hapo Mei, Mosi watashiriki katika maadhimisho ya Pasaka kwa Kanisa la Kiorthodox.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.