2016-03-03 14:42:00

Tumieni sayansi na teknolojia kudumisha maisha ya watu!


Fadhila na maadili katika maisha ni tema muhimu sana katika utamaduni mamboleo kwani mafao ya binadamu ni matunda ya ukarimu na uchaguzi huru unaotarajia jema. Sayansi na teknolojia haiwezi kufua dafu ili kumwezesha mtu kutenda jema, bali hekima inayobubujika kutoka katika sakafu ya moyo wa binadamu. Maandiko Matakatifu yanakaza kusema, nia njema au mbaya inapata chimbuko lake katika moyo wa mwanadamu.

Moyo kadiri ya Maandiko Matakatifu una maana pana zaidi kwani unagusa maisha ya kiroho, akili, utashi na hapa ni maskani ya maamuzi yanayoapswa kufanywa na mtu katika kufikiri na kutenda kadiri ya mwanga wa Roho Mtakatifu na kwamba, moyo unahusika. Hapa ni chimbuko la matendo mema na mabaya, pale ambapo ukweli na ushauri kutoka kwa Roho Mtakatifu unapowekwa kando. Moyo ni muhtasari wa ubinadamu ulioumbwa kwa mikono ya Mungu mwenyewe na katika moyo huu, Mungu anaweka hekima yake.

Hii ni tafakari ya kina iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko siku ya Alhamisi, tarehe 3 Machi 2016 alipokutana na wajumbe wa Taasisi ya Kipapa ya maisha wanaofanya mkutano wao wa mwaka mjini Vatican. Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, kutokana na baadhi ya mitazamo ya kitamaduni, wengi wanashindwa kutambua hekima ya Mungu inayofumbatwa katika maisha ya binadamu, lakini ikumbukwe kwamba, ubinadamu ni kito cha thamani sana mbele ya Mwenyezi Mungu kinachopaswa kulindwa na kudumishwa, ili uweze kuzaa matunda yanayokusudiwa.

Ili kutekeleza dhamana hii kuna haja ya kuupatia: uhuru na ukweli kwa kuulinda dhidi ya sumu ya uchoyo, ubinafsi na uwongo, ili kuzaa fadhila mbali mbali katika ubinadamu. Baba Mtakatifu anasema, fadhila ni tabia ya kawaida na imara ya kutenda mema; kutoa kilicho chema kabisa kutoka nafsini mwake na kwamba, fadhila humsaidia mtu kuchagua na kutenda mema. Fadhila ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha uhuru wa binadamu unaoweza kutolewa na moyo wa mtu. Moyo unapojikuta uko mbali na wema na ukweli unaofumbatwa katika Neno la Mungu, hapo kuna hatari ya kuchanganya mambo na matokeo yake ni mtu kuteleza na kuanguka katika masuala ya kimaadili.

Neno la Mungu linawakanya watu kutokuwa na mioyo migumu inayijikita katika ubinafsi na uovu; mambo ambayo ni vigumu kuweza kubadilika. Kila mtu anayetenda dhambi huyo ni mtumwa wa dhambi. Toba na wongofu wa ndani ni dawa madhubuti kabisa inayoweza kumsaidia mtu kubadili mwelekeo wa maisha yake. Baba Mtakatifu anatambua taasisi mbali mbali ambazo zinajielekeza katika huduma kwa maisha ya watu kwa njia ya tafiti sanjari na huduma kwa kusaidia kutenda mema na kuhamasisha kutafuta mema kwa ajili ya binadamu.

Lakini pia kuna taasisi ambazo zinatafuta kwa udi na uvumba mafao ya kiuchumi kuliko hata ustawi na maendeleo ya binadamu, changamoto ya kuwa kweli waaminifu kwa kutafuta mema kwa moyo mnyofu na ukweli. Kanuni maadili zinaonesha umuhimu wa kutafuta na kudumisha mema kwa binadamu; mambo yanayodhihirisha fadhila kwa ajili ya kuendeleza maisha ya binadamu.

Leo hii kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia kuna vifaa tiba vinavyoweza kusaidia kudumisha maisha ya binadamu, lakini kinachokosekana hapa ni utu, utambuzi wa kimaadili na mafao ya binadamu. Ni wajibu wa wafanyakazi katika sekta ya afya kuzingatia sayansi, teknolojia na utu. Haya ni mambo muhimu yanayopaswa kumwilishwa katika mafunzo na majiundo ya wanafunzi katika sekta ya afya ili kweli waweze kusimama kidete kupokea na kuhudumia maisha mintarafu utu wa mwanadamu bila kujali hali yake.

Viongozi wa sekta ya afya wawasaidie wafanyakazi wao kuzingatia huduma bora za kibinadamu, tayari kulinda na kudumisha maisha ya binadamu, sumaku inayovuta uzuri wa maisha kwa kuzingatia fadhila, ili kweli waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Baba kwa ajili ya maisha. Utamaduni mamboleo ukuze na kudumisha maisha ya binadamu kwa kujikita katika fadhila zinazomjenga mtu katika mchakato wa kufikiri na kutenda kwa kumtumainia Mungu ambaye ni kiini cha fadhila zote. Watu wasimame kidete kuondokana na ubinafsi na ujinga, ili kutenda kadiri ya moyo wa Mungu kwa kuonesha huruma ya Mungu. Majiundo yao iwe ni fursa ya kukua na kukomaa katika fadhila.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.