2016-03-03 09:05:00

Shirika la Kipapa kwa ajili ya Makanisa hitaji lapongezwa na Papa!


Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni amelishukuru Shirika la Kipapa kwa ajili ya Makanisa hitaji kutokana na mchango wake wa hali na mali kwa Makanisa hitaji sehemu mbali mbali za dunia. Baba Mtakatifu ameyasema haya wakati alipokutana na viongozi wa Shirika la Kipapa kwa ajili ya Makanisa hitaji baada ya maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican. Ibada hii imehudhuriwa pia na Askofu mkuu Joseph Couts, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Pakistan.

Katika maadhimisho ya kumbu kumbu ya miaka mitatu tangu Baba Mtakatifu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki, yaani tarehe 13 Machi 2016, Shirika la Kipapa kwa ajili ya Makanisa hitaji limemzawadia Baba Mtakatifu nakala ya Biblia ya watoto kutoka katika lugha ya mataifa ambayo Baba Mtakatifu katika kipindi cha miaka mitatu ameweza kuyatembelea.

Nakala ya kwanza ya Biblia kwa ajili ya watoto ilichapishwa kunako mwaka 1979 na tangu wakati huo zaidi ya nakala millioni 51 zimechapishwa katika lugha 178. Kutokana na mradi huu, mamillioni ya watoto yameweza kusoma na kutafakari Maandiko Matakatifu. Baba Mtakatifu anasema msaada kwa Makanisa hitaji ni kielelezo makini cha umoja na udugu kwa Makanisa yanayoendelea kuteseka kutokana na sababu mbali mbali duniani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.