2016-03-03 14:53:00

Onesheni toba ili kuambata huruma ya Mungu!


Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Ibada ya Misa aliyoadhimisha kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, Alhamisi, tarehe 3 Machi 2016 amesema, moyo ulio wazi na kiu ya toba, unaweza kukutana na kuambata huruma ya Mungu, tofauti kabisa na ukosefu wa uaminifu uliooneshwa na Waisraeli katika Agano la Kale. Kwa mwamini kujitambua kuwa ni mdhambi, huu ni mwanzo wa hija ya toba na wongofu wa ndani.

Mwenyezi Mungu alikuwa mwaminifu kwa ahadi zake, lakini Waisraeli wakamwangusha kwa kutokuwa waaminifu, wakashindwa kusikiliza mausia ya Neno lake; akawatendea miujiza mingi, lakini bado wakaonesha shingo ngumu. Ukosefu wa uaminifu ulioneshwa na Watu wa Mungu, uliwafanya kufunga mioyo yao kwa huruma na upendo wa Mungu.

Lakini, Mungu aliendelea kuwaalika kumfungulia mioyo yao, akiwataka kutokuwa na shingo ngumu, bali wepesi kusikiliza mausia yake. Mwenyezi Mungu anaendelea kuwaalika watoto wake ili waweze kumrudia tena kwa toba na wongofu wa ndani, kwani Yeye ni mwingi wa huruma na mapendo, lakini maneno haya yote yanagonga mwamba! Hakuna anayesikiliza.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, hivi ndivyo ilivyojitokeza kwa Yesu wakati wa maisha na utume wake. Viongozi wakuu wa dini waliokuwa na ujuzi na maarifa ya mambo ya Mungu, hawakumsikiliza Yesu, badala yake, watu wa kawaida waliguswa na kushangazwa na hekima iliyokuwa inabubujika kutoka kwa Yesu, wakawa na imani naye. Hawa ni watu waliokuwa na mioyo wazi; walielemewa na dhambi, lakini bado waliweza kuacha nafasi kwa Neno la Mungu kuingia na kuzama katika maisha yao.

Baba Mtakatifu anasema, kwa watu wenye mioyo migumu walitafuta visingizio vingi ili kumweka Yesu majaribuni: walitaka kumwona akitenda miujiza ili kushuhudia kile alichokuwa anatenda. Hii ndiyo historia ya watu wasiokuwa waaminifu kwa Mungu; watu wenye shingo ngumu wasioweza kukubali na kupokea huruma ya Mungu inayofumbatwa katika msamaha. Mungu anawasamehe waja wake, pale wanapotambua kwamba, wametenda dhambi. Yesu anakaza kusema, yule ambaye hayuko pamoja naye, ni kinyume chake.

Baba Mtakatifu anasema, huruma ya Mungu inaanza kutenda kazi pale mwamini anapojisikia kuwa ni mdhambi, tayari kutubu na kumwongokea Mungu na hapo Mungu anaonesha uaminifu wake. Waamini wawe na ujasiri wa kumwomba Mungu neema ya uaminifu, kwa kujisikia kuwa ni wadhambi, tayari kupokea na kuambata huruma na msamaha wa Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.