2016-03-03 09:20:00

Mshikamano wa Makanisa na Burundi


Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC linasikitika kuona hali ya machafuko na ukosefu wa amani, usalama na utulivu vikiendelea kushika kasi nchini Burundi, hali ambayo inahatarisha mafungamano na umoja wa kitaifa. Kutokana na changamoto hii, Baraza la Makanisa Ulimwenguni kwa kushirikiana na Baraza la Makanisa Yote Barani Afrika, AACC kuanzia tarehe 1- 4 Machi yanatembelea Burundi ili kuonesha mshikamano wa dhati katika mchakato wa kutafuta suluhu ya amani kwa wananchi wa Burundi ambao wamejaribiwa na kutikiswa sana na machafuko ya kisiasa nchini humo.

Dr. Olav Fykse Tveit, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni anasema, wako nchini Burundi iliĀ  kusaidia mchakato wa kutafuta suluhu ya amani nchini Burundi, baada ya machafuko ya kisiasa kuikumba Burundi kutokana na kasoro za uchaguzi muu uliopita. Wakiwa nchini Burundi, viongozi hawa wa Makanisa wanakutana na viongozi wa Kanisa na Serikali pamoja na mashirika ya misaada ya kimataifa. Ujumbe wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni unaongozwa na Dr. Olav Fykse Tveit.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.