2016-03-02 15:02:00

Nyanyaso za kijinsia kushughulikiwa haraka sana!


Askofu mkuu Angelo Becciu, Katibu mkuu msaidizi wa Vatican anasema kuhusu kashfa ya nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo, viongozi wa Kanisa wanapaswa kutoa maamuzi haraka iwezekanavyo ili kuepuka shutuma zisizokuwa na msingi, ili kuhakikisha kwamba, haki inatendeka mara moja. Kanisa linatambua na kukiri mapungufu yaliyojitokeza kwa baadhi ya viongozi wa Kanisa ambao walificha kwa makusudi kashfa ya za nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo ili  kuliepusha Kanisa na aibu kama hii.

Askofu mkuu Becciu anakaza kusema, hakuna taasisi yoyote duniani: kisiasa na kijamii ambayo imesimama kidete katika miaka ya hivi karibuni kulinda na kuwatetea watoto wadogo dhidi ya nyanyaso za kijinsia kama ambavyo Kanisa linafanya. Kanisa linaendelea kuweka sera na mikakati madhubuti ili kuwalinda na kuwatetea watoto dhidi ya uwezekano wa uwepo wa nyanyaso za kijinsia kwa watoto wadogo.  Askofu mkuu Becciu ameyasema haya katika mahojiano maalum na Bwana Gian Guido Vecchi yaliyochapishwa kwenye Gazeti la “Corriere della Sera, toleo la tarehe 1 Machi 2016.

Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI na baadaye Papa Francisko ni kati ya viongozi wa Kanisa ambao wamesimama kidete kuhakikisha kwamba, watoto wanalindwa dhidi ya nyanyaso za kijinsia kwa kuondokana na tabia ya kutaka kuficha au kuhalalisha maamuzi yaliyochukuliwa na viongozi. Kanisa liko macho kwa sasa, ingawa pengine limechelewa kufanya maamuzi mazito ili kulinda na kuwatetea watoto wadogo dhidi ya nyanyaso za kijinsia, lakini kwa hakika Kanisa limejifunza kutokana na makosa haya ya kihistoria, kwa sasa linataka kuwa makini zaidi ili mambo haya yasijirudie tena.

Askofu mkuu Becciu anafafanua kwamba, Kanisa lilipogundua kuhusu nyanyaso hizi, lilianza mchakato wa kujisafisha kwa kuweka sera na mikakati makini inayotekelezwa kwa wakati huu na kwamba, Mabaraza ya Maaskofu Katoliki sehemu mbali mbali za dunia yamepewa mwongozo wa kufuatwa ili kukabiliana na tatizo hili, sanjari na kushirikiana na vyombo vya sheria ili kuhakikisha kwamba, haki inatendeka na sheria ina chukua mkondo wake.

Nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo zinaacha majeraha makubwa katika maisha ya watoto na kwamba, hii ni dhambi kwa Mungu na Kanisa na hapa hakuna tena mchezo, mtu akipatikana, sheria inachukua mkondo wake. Kanisa litaendelea kutoa malezi makini kwa majandokasisi wake, ili kweli waweze kuwa ni mfano bora wa kuigwa katika maneno na matendo yao na kamwe wasiwe ni vichokoo vya kashfa zinazo lidhalilisha Kanisa. Maaskofu wawe makini katika kuwachagua wale wanaodhani kwamba, wana wito wa kuwa Mapadre.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.