2016-03-02 10:54:00

Huruma ya Mungu inakanya na kusahihisha!


Baba Mtakatifu Francisko wakati wa katekesi yake kwa mahujaji na wageni, Jumatano tarehe 2 Machi 2016 amegusia huruma ya Mungu inayofananishwa na Baba wa familia, anayewapenda, anayewasaidia na kuwahudumia watoto wake pamoja na kuwasamehe pale wanapokosa na kutenda dhambi. Baba wa familia anawafunda na kuwaelisha watoto wake; anawakanya na kuwasahihisha pale wanapokosea ili waweze hatimaye kukua na kukomaa katika kutenda mema.

Hivi ndivyo ambavyo Mwenyezi Mungu alivyowatendea Waisraeli waliokengeuka, wakazama na kubobea katika rushwa, ili kuwarejesha tena katika njia ya haki! Baba Mtakatifu anakaza kusema, katekesi yake inajikita kwa namna ya pekee katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu unaopania pamoja na mambo mengine, kuwaonjesha waamini upendo na huruma ya Mungu. Manabii katika Agano la Kale wanaonesha jinsi ambavyo Mwenyezi Mungu ameonesha upendo, akawataka Waisraeli kutubu na kumwongokea pale walipokengeuka na kuasi Amri, Maagizo na Agano lake.

Baba Mtakatifu anasema, hapana shaka kwamba wazazi na walezi wanatambua changamoto za malezi na makuzi ya watoto katika mchakato wa kuwasaidia kukua katika uhuru wa kweli na uwajibikaji. Mwenyezi Mungu katika Agano la Kale anaonesha masikitiko yake makubwa pale waja wake wanapotenda dhambi na kumkosea utii. Anapowaadhibu anataka kuwarejesha katika toba na wongofu wa ndani. Katika huruma na upendo wake anataka watoto wake wawe wema kwani hii ndiyo zawadi kubwa anayotaka kuwakirimia.

Baba Mtakatifu anafafanua kwamba, kadiri ya Nabii Isaya, Mwenyezi Mungu hapendezwi na sadaka za kuteketezwa, bali anataka watu watubu na kutenda haki. Hata kama dhambi zao ni nyekundu kiasi gani, atazisafisha na kuzifanya kuwa nyeupe pe, kama theluji. Waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanahamasishwa na Baba Mtakatifu kujiweka wazi mbele ya Mungu wakati huu wa Maadhimisho wa Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, kumrudia Mungu kwa njia ya toba na wongofu wa ndani, ili kuonja muujiza wa huruma na upendo.

Baba Mtakatifu anawataka waamini kuhakikisha kwamba, Mwaka wa huruma ya Mungu unakuwa kweli ni kipindi cha neema na upyaisho wa maisha ya kiroho. Ikumbukwe kwamba, huruma ya Mungu imetolewa kwa watu wote na kipindi cha Kwaresima iwe ni fursa ya kufanya majuto ya dhambi, tayari kukimbilia ili kuambata huruma ya Mungu inayofumbatwa katika Sakramenti ya Upatanisho kwa kufanya toba ya kweli, ili kuwawezesha kuishi kama watoto wapendwa wa Mungu.

Kristo ni ushuhuda wa uwepo endelevu wa Mungu kati ya watu wake, waamini waoneshe ujasiri wa kumwendea, ili kujenga urafiki na hatimaye, kujipatia maisha ya uzima wa milele. Mwenyezi Mungu anawaalika wote kutubu na kuongoka, lakini pia anasikiliza kilio cha watoto wake wanaoteseka na kunyanyasika. Hafurahii sala na sadaka inayonuka damu ya watu wasiokuwa na hatia, bali anawapokea na kuwakumbatia wale wanaotubu na watu wema wanaomkaribia wakiwa na mikono safi isiyokuwa na mawaa! Watu wanaotenda wema na haki.

Kwaresima ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu iwe ni fursa ya kumwilisha matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Anawaalika waamini kukuza na kudumisha Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu, Ijumaa ya kwanza ya mwezi, kwa kusali na kutafakari kuhusu Fumbo la Mateso, kifo na ufufuko wa Kristo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.