2016-03-02 12:04:00

DR. Jakaya Mrisho Kikwete ateuliwa kuwa balozi wa heshima wa chanjo duniani


Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepokea kwa furaha uteuzi uliofanywa na Shirika la Global Alliance for Vaccines and Immunizations (GAVI) kwa kumteua Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais Mstaafu wa awamu ya nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Balozi wa Heshima wa Chanjo Duniani. Kwa niaba ya Serikali, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na kwa niaba yangu binafsi napenda kuchukua fursa hii kumpongeza kwa dhati Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwa uteuzi huu.

Ndugu wananchi,  Kama mlivyosikia kwenye vyombo vya habari Rais wetu mstaafu wa awamu ya nne (4) Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete ameteuliwa kuwa BALOZI WA HESHIMA WA CHANJO DUNIANI kupitia shirikia la Global Alliance for Vaccines and Immunizations (GAVI) mnamo tarehe 31 Januari, 2016 nchini Ethiopia. Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inapenda kuchukua fursa hiikuungana na shirika la GAVI pamoja na wananchi wote wa Tanzaniakumpongeza Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwa uteuzi huo. Kuteuliwa kwake kuwa Balozi wa heshima kwenye masuala ya chanjo, kuna maana ya kuwa,atakuwa mhamasishaji wa wakuu wote wa nchi za Afrika na dunia kwa ujumla kuhakikisha wanaweka kipaumbele katika upatikanaji wa huduma za afya hususan masuala ya chanjo.

Katika muda wote wa uongozi wake Mheshimiwa Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete alitoa kipaumbele katika masuala ya afya ya uzazi na mtoto likiwemo suala la chanjo na kuhakikisha wanawake na watoto wanapata huduma ipasavyo. Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto pamoja na Watanzania wote tumefarijika sana kwa uteuzi huo, kwani pamoja na juhudi hizo, amekuwa ni Mwenyekiti mwenza wa Jopo la watu mashuhuri la kumshauri Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa juu ya uboreshaji wa malengo ya Maendeleo endelevu.(Sustainable Development Goals)

Aidha,Mheshimiwa Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete alishiriki katika mkutano mkubwa wa GAVI uliofanyika mnamo tarehe 26 hadi 27Januari 2015 nchini Ujerumani na kueleza dhamira yake na ya nchi kwa ujumla katika kushiriki kikamilifu kupunguza kiwango kikubwa cha maradhi na vifo vitokanavyo na magonjwa yanayozuilika kwa chanjo. Ikumbukwe kuwa katika kipindi cha uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete,Tanzania iliweza kuongeza kiwango cha utoaji wa huduma za chanjo hadi kufikia wastani wa zaidi ya asilimia 95 ikiwa ni zaidi ya lengo la Kimataifa la asilimia 90.Tunaami kuwa mafanikio haya yamechangia Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kupewa heshima hiyo.

Historia inaonyesha kuwa kwenye miaka ya sabini watoto wengi walipoteza maisha yao kutokana na magonjwa yanayozuilika kwa chanjo. Wengi wetu ni mashahidi wa milipuko na vifo vilivyotokana na ugonjwa wa surua kipindi hicho. Wodi nyingi katika Hospitali zetu zilitengwa na zilijaa watoto waliougua surua na ugonjwa wa pepo punda. Aidha, watoto wengi walibakia na ulemavu wa viungo, ulemavu wa kutoona, ulemavu wa kutosikia, na mtindio wa ubongo kutokana na athari za magonjwa ya polio na surua. Juhudi za Serikali katika kukabiliana na magonjwa yanayozuilika kwa chanjo zimeleta mafanikio makubwa. Kwa mfano, magonjwa ya ndui na pepopunda kwa watoto wachanga yametoweka,pia tumeshuhudia wodi za surua zikifungwa, na vifo vitokanavyo na surua kupungua kwa kiasi kikubwa.Aidha Tanzania imekwisha thibitishwa kuwa ni miongoni mwa nchi zilizotokomeza ugonjwa wa Polio duniani. Mafanikio haya ni matokeo ya juhudi za Serikali kuwekeza katika chanjo.

Imethibitika kuwa chanjo ni mkakati muafaka katika kutokomeza magonjwa na kupunguza vifo vya watoto, hivyo kupunguza gharama kubwa ambazo familia zetu na Taifa kwa ujumla lingetumia katika kutibu maradhi yatokanayo na magonjwa yanayozuilika kwa chanjo. Rejea za kitaaluma zimethibitisha kuwa chanjo huzuia takribani vifo Milioni 2 hadi 3 kila mwaka kutokana na maradhi yanayozuilika kwa chanjo duniani. Nchini Tanzania, mwaka 2004, vifo vya watoto chini ya miaka mitano vilikuwa 112 kati ya vizazi hai 1,000 na viliendelea kupungua hadi vifo 81 kwa kila vizazi hai 1,000 mwaka 2010.

Mojawapo ya mikakati ya Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete katika kipindi chake cha uongozi ilikuwa ni kufikia malengo ya maendeleo ya Milenia. Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa (UN Inter Agency Report for child mortality estimates), Tanzania ilifanikiwa kufikia lengo la Millenia namba 4 la kupunguza vifo vya watoto walio na umri chini ya miaka 5 kutoka vifo 81 hadi vifo 54 kwa kila vizazi hai 1,000 mwaka 2013.

Tunafahamu kuwa Mheshimiwa Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete ana kazi kubwa mbele yake ya kuhakikisha nchi zote za Afrika na Dunia kwa ujumla zinafikia kiwango cha wastani wa asilimia 90 wa chanjo kwani, hadi sasa, bado kuna nchi ambazo bado zina kiwango cha wastani wa asilimia 50. Ni faraja yetu kubwa kuwa Mheshimiwa Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete ataendelea kuwa mstari wa mbele kuhakikisha upatikanaji wa huduma za chanjo barani Afrika na dunia kwa ujumla na hivyo kuokoa maisha ya watoto. Tunamtakia mafanikio mema katika utekelezaji wa majukumu hayo makubwa kidunia,na kumuahidi ushirikiano wetu.

 

Imetolewa na ;

Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

1.3.2016

 








All the contents on this site are copyrighted ©.