2016-03-01 10:28:00

Wanawake simameni kidete kulinda, kutetea na kudumisha haki na amani!


Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Kusini mwa Afrika, IMBISA, hivi karibuni, liliandaa mafunzo kwa wanawake kutoka katika nchi za IMBISA huko Maseru, Lesotho; kuhusu: wanawake na maendeleo; haki msingi za wakimbizi na wahamiaji. Hizi ni changamoto zinazoendelea kuibuliwa kila siku kutokana na ongezeko la wimbi la wakimbizi na wahamiaji Kusini mwa Afrika, wengi wao ni wale wanaotafuta fursa za ajira na maisha bora, lakini wanajikuta wakiteseka na kunyanyasika ugenini kama ilivyojitokeza hivi karibuni kwa baadhi ya Nchi zilizoko Kusini mwa Afrika.

Wanawake Wakatoliki IMBISA wanahamasishwa na Kanisa kuhakikisha kwamba, wanatambua haki msingi za binadamu, tayari kuzisimamia katika utekelezaji wa shughuli, mikakati na utume wao ndani na nje ya Kanisa. Wanawake Wakatoliki wanapaswa kuwa ni sauti ya wanyonge, hasa miongoni mwa wanawake ambao wamekuwa ni wahanga wa biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo; mambo yanayodhalilisha utu na heshima yao kama binadamu.

Wanawake wametakiwa kusimama kidete kuhimiza utawala bora unaojikita katika sheria, ili kuwashughulia wale wote wanaojihusisha na uvunjaji wa sheria hasa dhidi ya wanawake wahamiaji na wakimbizi. Semina hii ni mwendelezo wa utekelezaji wa changamoto zilizotolewa na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI katika Waraka wake wa kitume, Dhamana ya Afrika, “Africae munus” mwongozo makini katika maisha na utume wa Kanisa Barani Afrika.

Hapa wanawake Barani Afrika wanakumbushwa kwamba, wao ni vyombo na mashuhuda wa misingi ya haki, amani na upatanisho katika jamii. Wanawake walipata fursa ya kushirikishana uzoefu na mang’amuzi yao katika ujenzi wa misingi ya haki, amani na upatanisho, ili kweli Bara la Afrika liweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

IMBISA: Inter-regional Meeting of the Bishops of Southern Africa.








All the contents on this site are copyrighted ©.