2016-03-01 10:14:00

Someni alama za nyakati; toeni kipaumbele cha kwanza kwa utume wa Kanisa!


Askofu mkuu Angelo Becciu, Katibu mkuu msaidizi wa Vatican katika hotuba yake ya shukrani kwa Padre Federico Lombardi aliyekuwa Mkurugenzi mkuu wa Radio Vatican pamoja na Dr. Alberto Gasbarri aliyekuwa Mkurugenzi wa utawala, wakati wa kung’atuka kwao kutoka madarakani hapo tarehe 29 Februari 2016 amesema, Radio Vatican ni muhimu sana mbele ya Mungu na macho ya waamini na watu wenye mapenzi mema.

Kipindi hiki cha mageuzi kitasaidia kuleta matumaini na dhamana mpya katika mchakato wa Uinjilishaji mpya, ili kuweza kufikisha ujumbe wa Neno la Mungu katika mioyo ya watu wengi. Vyombo vya habari vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Vatican vinapaswa kuangalia matukio mbali mbali ya dunia kwa jicho la Kanisa na kwa mwanga wa mafundisho ya Mababa wa Kanisa.

Vyombo vya habari za Kanisa havina budi kujishughulisha kwa namna ya pekee na mambo yanayomgusa mwanadamu kwa nyakati hizi: vita, umaskini, magonjwa, mazingira; wahamiaji na wakimbizi bila kusahau changamoto ya ukanimungu pamoja na kuwaimarisha waamini katika imani na Injili ya Kristo! Vatican inawashukuru na kuwapongeza kwa namna ya pekee, Padre Federico Lombardi na Dr. Alberto Gasbarri kwa sadaka na majitoleo yao kwa Radio Vatican. Ni Radio ambayo imekuwa kweli ni sauati ya kinabii, katika kutetea haki za maskini na wanyonge; utu na heshima ya binadamu, lakini zaidi kwa kutangaza Injili ya furaha na matumaini kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko.

Padre Lombardi ni kiongozi aliyeipenda Radio Vatican; akaitetea kwa ari, ujasiri na moyo mkuu pasi na makuu pamoja na kuhakikisha kwamba, haki na mahitaji yake msingi yanapatikana ili iweze kusonga mbele. Aliwapenda na kuwathamini wafanyakazi wa Radio Vatican ambao wamekuwa kweli ni Jumuiya yake katika maisha na utume wa Kanisa kwa kipindi cha miaka 25.

Ameona na kushuhudia mabadiliko ya teknolojia ya mawasiliano ya jamii na kuhakikisha kwamba, ujumbe wa Vatican na Kanisa unawafikia wengi, hasa wale ambao bado wanasuasua katika maendeleo ya sayansi na teknolojia ya habari. Padre Federico Lombardi amekuwa kweli changamoto katika mang’amuzi na maendeleo ya mawasiliano ndani ya jamii. Padre Lombardi anaendelea kuwa msemaji mkuu wa Vatican kwa sasa! Uwepo wa Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican ni juhudi binafsi za Padre Lombardi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.