2016-03-01 14:48:00

Mshikamano wa kidugu na upendo kwa wananchi wa Fiji


Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC limetuma salam za rambi rambi kwa wananchi wote wa Kisiwa cha Fiji waliokumbwa na tufani ya Winston na kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Dr. Olav Fyske Tveit, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, wanashirikiana ili kuwasaidia wale waliokumbwa na maafa haya, kwa kuwapatia msaada wa hali na mali.

Ni matumaini ya Baraza la Makanisa Ulimwenguni kwamba, watu wataonesha umoja, udugu na mshikamano katika kuwahudumia wale waliokumbwa na maafa haya. Tufani hii imesababisha watu zaidi ya 40 kupoteza maisha na zaidi ya watu laki tatu hawana makazi baada ya makazi yao kuharibiwa vibaya na tufani ya Winston. Serikali ya Kisiwa cha Fiji imetangaza eneo hili kuwa limekumbwa na majanga asilia.

Baraza la Makanisa Ulimwenguni linasema kwamba, waamini kwa namna ya pekee wanapaswa kuonesha mshikamano wa upendo wakati wa majanga kama haya, ili kweli waweze kuwa ni sauti ya matumaini kwa wale wanaoteseka. Makanisa mbali mbali yameanza kutoa misaada kwa waathirika huko Fiji kwa kushirikiana na Chama cha Msalaba Mwekundu. Baraza la Makanisa Ulimwenguni linapenda kuwahakikishia wananchi wa Visiwa vya Fiji uwepo wake wa karibu kwa njia ya sala na sadaka. Matatizo na changamoto wanazokumbana nazo ni matatizo na changamoto za Baraza la Makanisa Ulimwenguni.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.