2016-03-01 09:39:00

Mshikamano na wagonjwa wenye magonjwa adimu


Askofu mkuu Zygmund Zimowski, Rais wa Baraza la Kipapa la wahudumu katika sekta ya afya katika ujumbe wake kwa maadhimisho ya Siku ya IX ya Magonjwa Adimu Duniani ambayo imeadhimishwa hapo tarehe 29 Februari 2016 kwa kuongozwa na dhamiri “Kiini kiwe ni sauti ya mgonjwa: Jiungeni nasi ili kupaaza sauti kwa magonjwa adimu” anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuendelea kushikamana na kuwasaidia wagonjwa. Tema iliyochaguliwa kwa maadhimisho ya Mwaka huu inatoa pia changamoto kwa Mama Kanisa, ili kuendelea kufanya tafiti na hatimaye tiba kwa magonjwa haya yanayoendelea kusababisha mateso na mahangaiko makubwa kwa wagonjwa na familia zao.

Askofu mkuu Zimowski anaiomba Jumuiya ya Kimataifa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa wagonjwa hawa ambao kimsingi wanapaswa kuwa ni wadau na walengwa wa kwanza katika huduma na tiba. Wadau mbali mbali waendelee kuhamasishwa kufanya tafiti mbali mbali ili kuweza kupata tiba muafaka ya magonjwa haya. Lengo ni kuvunja ukimya unaoambata wagonjwa hawa, kwani hii ni changamoto ya Jamii nzima.

Kanisa linasikia kuwa na wajibu mzito katika mahangaiko ya wagonjwa hawa ili kuwaonjesha huruma na mshikamano kama sehemu ya utekelezaji wa mafao ya wengi na haki katika sekta ya afya ya jamii. Baraza la Kipapa la wahudumu katika sekta ya afya linapenda kuendeleza changamoto hii katika ngazi na kwa wadau mbali mbali wa tafiti za kisayansi; kwa kukuza na kudumisha sera na mikakati endelevu ya huduma za kichungaji kwa wagonjwa hawa kama ushuhuda wa mshikamano wa upendo.

Askofu mkuu Zimowski anasema kwamba, magonjwa adimu itakuwa ni mada itakayofanyiwa kazi na Baraza lake wakati wa mkutano wake mkuu utakaofanyika mjini Vatican kuanzia tarehe 10 – 12 Novemba 2016. Katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, Kanisa linapenda kuwahamasisha waamini na wadau mbali mbali kutoa kipaumbele cha kwanza katika utekelezaji wa matendo ya huruma: kiroho na kimwili kwa wagonjwa; maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.