2016-03-01 09:49:00

Mshikamano katika kutetea utu na heshima ya binadamu!


Patriaki Abuna Matthias wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox  Tewahedo la Ethiopia wakati wa hija yake ya kitume mjini Vatican amepata nafasi ya kutembelea Kanisa kuu la Mtakatifu Petro pamoja na kuadhimisha Ibada Takatifu na Familia ya Mungu kutoka Ethiopia inaoishi hapa mjini Roma. Patriaki Abuna Matthias wa kwanza, Jumatatu tarehe 29 Februari 2016 amekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican.

Katika hotuba yake amekazia umuhimu wa Makanisa haya kuendeleza mahusiano ya kiekumene katika maisha na utume wao na kwamba, wataendeleza pia majadiliano ya kiekumene yanayotekelezwa na Tume ya pamoja ya Kitaalimungu kimataifa, ili kujenga umoja wa Kanisa unaoonekana. Amemshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa moyo wake wa upendo na mshikamano na Familia ya Mungu nchini Ethiopia, hususan kwa ushuhuda wa imani unaoendelea kutolewa na wafiadini kutoka Ethiopia.

Patriaki Abuna Matthias wa kwanza amemwelezea Baba Mtakatifu Francisko kwamba, Kanisa lao ni kati ya Makanisa ya zamani yanayoendelea kuhifadhi amana ya Mababa wa Kanisa inayofumbatwa katika Biblia, Mapokeo ya Kanisa, Liturujia, Sala, Sakramenti na Mafungo. Wanayo ibada kwa Bikira Maria Mama wa Mungu, watakatifu na mashuhuda wa imani; mambo yanayowaunganisha kama Wakristo na kwamba, bado kuna nafasi ya kuendelea kushirikiana kwa karibu zaidi kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa.

Patriaki Abuna Matthias wa kwanza anakaza kusema, ulimwengu mamboleo unaendelea kukabiliana na changamoto nyingi zinazojikita katika: vita, misimamo mikali ya kidini; utamaduni wa kifo pamoja na athari kubwa za mabadiliko ya tabianchi. Mambo yote haya yanahitaji kwa namna ya pekee umoja na mshikamano katika kulinda na kutetea haki, amani, ustawi na maendeleo ya wengi; utu na heshima ya binadamu; ili kweli dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.