2016-02-29 15:39:00

Wokovu wa Mungu unajionesha katika mambo ya kawaida!


Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Ibada ya Misa Takatifu aliyoiadhimisha kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, kilichoko mjini Vatican , Jumatatu tarehe 29 Februari 2016 amewakumbusha waamini kwamba,  wokovu wa Mungu haujikiti katika mambo makubwa yanayotetemesha dunia, nguvu au fedha bali katika maisha na matukio ya kawaida ambayo wakati mwingine hayapewi uzito unaostahili kama ilivyotokea kwa Jemedari Naaman aliyeambiwa na Nabii Elisha kwenda kujitakasa kwenye Mto Yordani mara saba, akaona kwamba, Nabii wa Mungu alikuwa amemdharau kwa kwani hakutoka nje ili kumpoea na kumtibu na badala yake akamwelekeza kwenda kujitakasa mtoni, alipotekeleza agizo la Nabii Elisha akapona na kumwamini Mungu wa Israeli.

Hivi ndivyo ilivyokuwa hata kwa Yesu wakati alipokuwa anahubiri, wengi hawakuamini maneno yake, akabezwa na wakuu wa Makuhani, waandishi na wanasheria, waliokuwa wanatafuta wokovu kwa kujificha katika maadili, lakini watu wengi hawakuwa na imani nao kwani matendo yao yalisigana na kile walichokuwa wanasema na kutenda! Masadukayo waliamini zaidi katika nguvu za watawala wa ulimwengu huu, wakaonesha shingo ngumu kwa watenda dhambi, lakini hata hawa hawakumwamini Yesu, kwani walitegemea kuona mambo makubwa yanayotisha!

Yesu katika maisha na utume wake anasema Baba Mtakatifu alizungumza na kuwaonesha watu wokovu unaofumbatwa katika maisha na mambo ya kawaida kabisa, yaani Heri za Mlimani na Matendo ya huruma yanayomwilishwa katika maisha ya watu! Hiki ndicho kipimo cha hukumu itakayotolewa na Kristo, mwisho wa nyakati, atakapokuja kuwahukumu wazima na wafu na wala Ufalme wake hautakuwa na mwisho.

Heri za Mlimani, muhtasari wa mafundisho makuu ya Yesu iwe ni dira na mwongozo thabiti kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanapojiandaa kwa ajili ya kuadhimisha Fumbo la Pasaka katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Msalaba wa Kristo ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha huruma ya Mungu kwa binadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.