2016-02-29 08:56:00

Waziri mkuu Kassim M. Majaliwa atikisa Mtwara!


Waziri mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amepokea misaada mbalimbali kwa ajili ya wakazi wa vijiji vya Mtondo na Nanjaru wilayani Ruangwa mkoani Lindi ambao nyumba zao ziliezuliwa na upepo Januari mwaka huu. Akizungumza na wananchi wa vijiji hivyo Jumapili, Februari 28, 2016, Waziri Mkuu alisema maafa huwa yanakuja bila kutarajiwa na akatumia fursa hiyo kuwashukuru wadau waliotoa misaada ya chakula, magodoro, mashuka, vitenge, mabati na mbegu za mazao. Aliwataja wadau hao kuwa ni Benki ya NMB, NSSF, wakazi wa Ruangwa na marafiki wa Ruangwa waishio Dar es Salaam ambao walifika kukabidhi misaada hiyo.

Waziri Mkuu ambaye yuko kwenye ziara ya siku mbili katika mikoa ya Mtwara na Lindi kukagua athari za mafuriko, hatua zinzochukuliwa za utoaji misaada kwa waathirika na kuwapa pole wananchi walioathirika na mafuriko hayo, alitumia fursa hiyo kuwataka wananchi waishio mabondeni wahame kwa sababu mvua kubwa bado zinakuja. "Jambo hili si mipango ya mtu binafsi na sote tunajua kwamba tunahitaji mvua kwa ajili ya mazao lakini safari hii zimekuja zaidi ya kiwango cha kawaida. Mamlaka ya hali ya hewa imeshasema kuwa mvua kubwa zaidi zinakuja ifikapo Machi mwaka huu", alisema.

Ili kuepusha maafa zaidi, kuanzia sasa, wale waliojenga mabondeni wanapaswa wahame. Pia nawasihi wananchi wachukue tahadhari wakiona mvua inakuja na upepo mkali wasikae ndani ya nyumba sababu hapa kijijini tumempoteza mzee wetu mmoja ambaye aliangukiwa na nyumba baada ya nyumba yake kuangukiwa na mti kutokana na mvua hizo," aliongeza.

Kwa mujibu taarifa ya maafa iliyotolewa na Mkuu wa wilaya ya Ruangwa, Bi. Mariam Mtima, mvua zilizonyesha kati ya Januari na Februari mwaka huu zilisababisha nyumba 393 kuezuliwa na nyingine kubomoka na kuacha wakazi wa vijiji hivyo bila makazi.  "Zahanati ya kijiji cha Mtondo iliezuliwa paa, daraja la mto Muhuru limebomoka na halipitiki kabisa na ekari 1,186 za mashamba ya wananchi zimesombwa na maji. Mazao yaliyoathirika ni mahindi, muhogo, mikorosho, mtama, ufuta, kunde, mpunga na mbaazi," alisema Mkuu huyo wa wilaya katika taarifa yake.

Alivitaja vijiji vingine ambavyo mafuriko hayo yaliharibu mashamba ya wananchi kuwa ni Nambilanje, Mkaranga, Namkatila, Chinongwe A, Likwachu, Nauname na Mbekenyera. Alisema hali hiyo imesababisha upungufu mkubwa wa chakula wilayani humo na sasa hivi wanahitaji tani 1,133 za chakula aina wanga ambazo anataraji zitatosheleza mahitaji kwa mwezi Machi 2016.

'SERIKALI YATENGA SH. BILIONI 1.6/- VYUO VYA UALIMU"

Waziri mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amesema Serikali imetenga kiasi cha sh. bilioni 1.65/- kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo kwenye vyuo vya walimu hapa nchini TanzaniaAlitoa kauli hiyo Jumamosi, Februari 27, 2016, wakati akizungumza na walimu na watumishi wa sekta ya elimu kutoka wilaya zote za Mkoa wa Mtwara uliofanyika kwenye ukumbi wa Chuo cha Ualimu Mtwara.

"Serikali inatambua uhumimu wa mafunzo kwa vitendo katika vyuo vya ualimu ni kwa sababu hiyo mwezi huu wa Februari tumetoa sh. bilioni 1.65/- kwa vyuo vya ualimu 35 vya umma nchini ili kuwezesha wakufunzi na walimu wanafunzi kushiriki kikamilifu mafunzo kwa vitendo (Block Teaching Practice)," alisema huku akishangiliwa. Alisema fedha hizo zinapaswa zitumike kulipia posho za kujikimu, nauli na ununuzi wa vifaa vya kujifunzia na kufundishia.

Mapema, akizungumza na mamia ya wakazi wa Mtwara kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa mashujaa, Waziri Mkuu alisema Serikali imedhamiria kuimarisha elimu na akawaonya wote wanaowaharibia elimu watoto wa kike. "Tunataka watoto wa kike wasome wa Kitanzania wasome hadi elimu ya juu waje wawe watumishi wa umma hapo baadaye. Kila mmoja awe mlinzi wa mwenzake tukikumbuka kaulimbiu ya Mama Salma Kikwete ya kwamba 'Mtoto wa Mwenzio ni wako'," alisema. "Yeyote atakayemharibia mtoto wa kike masomo kwa kumrubuni na chips au pipi ajiandae kwenda Lilungu, (gereza la mkoa wa Mtwara)", alisema.

WAZIRI MKUU ANUSA UFISADI BANDARI YA MTWARA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekagua bandari ya Mtwara na kunusa harufu ya ufisadi katika utoaji wa zabuni ya ujenzi wa gati mpya tatu. Wazi Mkuu ambaye alikagua eneo la ujenzi wa gati hizo Jumamosi, Februari 27, 2016, alisema anazo taarifa juu ya utolewaji wa zabuni hiyo na mzabuni ameshashinda lakini kuna madai kwamba watu wa manunuzi kupitia PPRA ndiyo wanakwamisha zabuni hiyo. Aliwaomba wabunge wa mkoa wa Mtwara washirikiane kusimamia suala hilo ili ujenzi wake uweze kuanza mara moja na kuleta ajira kwa wana Mtwara. "Ujenzi ukikamilika siyo tu ajira zitaongezeka bali hata meli nyingi zitaleta mizigo katika bandari hii na mapato ya mkoa yataongezeka", alisema.

"Natambua kwamba kuna mpango wa kujenga gati nne ambapo moja kati ya hizo itajengwa na TPA (Mamlaka ya Bandari) lakini hizi tatu zilitangazwa na kupata mzabuni ambaye ni kampuni ya Hyundai kutoka Japan. Lakini hii kampuni imekuwa ikizungushwa bila sababu. Tutafuatilia kubaini tatizo liko wapi," aliongeza. "Sasa hivi tuna uwezo wa kupaki meli moja tu, lakini gati zikikamilika tutaweza kuwa na meli tatu kwa mpigo, cha msingi tusimamie maamuzi yetu kwamba lazima wafanyabiashara wa korosho watumie bandari hii kusafirisha mizigo yao na si kuipeleka kwingine."

"Kwenye Bodi ya Korosho nako kuna majipu yanahitaji kutumbuliwa. RCC ilishakaa na kupitisha uamuzi kuwa mizigo yote ipitie bandari ya Mtwara lakini kuna watu ndani ya Bosi hiyo wanatoa vibali vya kusafirisha mizigo kupitia bandari ya Dar es Salaam. " Alimtaka mkuu wa bandari ya Mtwara (Port Master) Bw. Prosper Kimaro awe makini na watu wa kitengo cha manunuzi katika bandari hiyo kwani kimekuwa chanzo cha upotevu wa fedha za Serikali kutokana na ujanja wa watu wachache.

"Hapa si kuna mtu alitaka kuiba sh. milioni 300 kwa kufoji saini za wakubwa wake? alihoji Waziri Mkuu swali ambalo lilijibiwa na Bw. Kimaro kwamba ni kweli lakini uongozi uliingilia kati kabla wizi huo haujakamilishwa. Kuhusu fidia kwa wakazi wa vijiji vya Kisiwa na Mgao ambao wamekubali kuhama ili kupisha upanuzi wa bandari hiyo, Waziri Mkuu aliwahakikishia wabunge hao pamoja na uongozi wa bandari kwamba kiasi cha sh. bilioni 13.8/-kimekwishatengwa na Wizara na kitatolewa mapema mwezi ujao.

Alitumia fursa hiyo kusisitiza udhibiti wa bandari bubu ambazo zinatumiwa kuingiza sukari na mchele mchezo ambao unaikosesha Serikali mapato. "Mkuu wa Mkoa, nilikwishatoa agizo kama hilo wakati nimeenda kukagua bandari ya Tanga. Kaa na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa nanyi pia muweke mbinu za kudhibiti upenyo huu wa kuingiza bidhaa za magendo kwa sababu hawa ndiyo wanaokwepa kulipa kodi ya Serikali," alisisitiza.


Naye, Mkuu wa bandari hiyo, Bw. Kimaro wakati akitoa taarifa ya utendaji wa bandari mbele ya Waziri Mkuu, alisema bandari hiyo ilianzishwa mwaka 1950 na imekuwa inakabiliwa na ufinyu wa gati ya kuegesha meli, vifaa vya kupakulia na kupakia mizigo na kwamba hivi sasa wamekwishapata winchi ya bandarini (harbour crane) yenye uwezo wa kubeba tani 100 na tayari wako kwenye mpango wa kujenga gati moja.

Na Ofisi ya Waziri mkuu wa Tanzania.








All the contents on this site are copyrighted ©.