2016-02-29 16:24:00

Ufunuo wa huruma ya Mungu kwa mwanadamu!


Mungu alimuumba mwanadamu katika hali ya neema ya utakaso. Hata hivyo mwanadamu hakubaki katika hali hiyo, alivunja amri aliyopewa na Mungu na kutaka kufanya alichotaka na siyo alivyotaka Mungu. Ingawa Mungu alimwadhibu mwanadamu kwa kosa lake, bado alimhurumia. Kwanza alimwahidi mwanadamu kumletea mkombozi. Mungu anamwambia adui wa mwanadamu, shetani, akisema “Nitaweka uadui kati yako na huyo mwanamke, na kati ya uzao wako na uzao wake; huo utakuponda kichwa na wewe utamponda kisigino” (Mwa 3:15).

Kwa maneno hayo Mungu aliahidi kuwaletea wanadamu Mwanae ili awakomboe na dhambi zao. “Hatua hiyo ya kitabu cha “Mwanzo” imeitwa “Injili ya kwanza” kwa sababu inatangaza kwa mara ya kwanza Masiha na Mkombozi, mapambano kati ya shetani na mwanamke na ushindi wa mwisho wa mzao wake.” Utekelezaji wa ahadi hiyo ya Mungu umedhihilika katika nafsi ya Yesu Kristo, Mwana pekee wa Mungu, aliye Mungu nafsi ya pili ya Utatu Mtakatifu. Katika masimulizi ya historia ya wokovu, Agano la Kale linatusimulia jinsi Mungu alivyojifunua kwa mwanadamu hatua kwa hatua kuwa ni mwenye huruma.

Kwanza Mungu aliandaa taifa la Israeli kwa njia ya mababu wa taifa hilo, ili toka taifa la Israeli Mungu afahamike kwa mataifa yote, na toka taifa hilo atokee mkombozi. Alimwita Ibrahimu na kwa ahadi zake kwa Isaka na Yakobo aliweka Agano na taifa la wana wa Yakobo mlimani Sinai baada ya kuwatoa utumwani Misri akijitambulisha kuwa yeye ni “Mungu mwingi wa huruma mwenye fadhili, si mwepesi wa hasira, mwingi wa rehema na kweli” (Kut 34:6). Kwa njia ya vivywa vya manabii wake, Mungu alinena na watu wake akijifunua kwao. Aliwapa ujumbe wake, na mwongozo wa maisha. “Maana unabii haukuletwa popote kwa mapenzi ya mwanadamu bali wanadamu walinena yaliyotoka kwaMungu, wakiongozwa na Roho Mtakatifu”(2Pt 1:21).

Hivyo “matokeo (Kujifunua kwa Mungu) yanaangaza njia ya ahadi, kutoka mababu hadi Musa na kutoka Yoshua mpaka maono yanayoanzisha utume wa manabii wakubwa”. Ingawa mwanadamu alionekana kumkosea Mungu tena na tena; bado Mungu aliendelea kumhurumia. Mara nyingi mwanadamu alimuasi Mungu na kuvunja uaminifu wa Agano alilofanya na Mungu. “Maana historia yote ya binadamu imejaa mapambano magumu dhidi ya nguvu za giza. Mapambano haya yalianza tangu mwanzo wa dunia, nayo yataendelea, asemavyo Bwana, mpaka siku ya mwisho. Binadamu akiwa katika vita hivi, lazima apambane bila kukoma, ili aweze kuambatana na mema; wala hataweza kuufi kia umoja wake wa ndani, bila juhudi kubwa, pamoja na msaada wa neema ya Mungu.”

Kristo Mwana wa Mungu alizindua nyakati za Agano jipya. Kwa tendo la umwilisho wake, Mwana wa Mungu alifanyika mtu kwaajili ya kuifi kisha kwa wanadamu huruma ya Mungu katika ukamilifu wake na kumpatanisha mwanadamu na Mungu. Kwa njia hii ya huruma kuu ya Mungu mwanadamu anaalikwa kuutambua na kuupokea upendo huu mkuu wa Mungu, kupitia Kristo aliye kielelezo chetu cha utakatifu na anayetufanya washiriki wa tabia ya uungu. Kristo, akifungua utume wake,ananukuu kitabu cha nabii Isaya akisema, “Roho wa Bwana yu juu yangu, kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri masikini habari njema, amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, na vipofu kupata kuona tena, kuwaacha huru waliosetwa na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa” (Lk 4:18-19/Isa 61:1-3). 

Tangazo hilo liliambatana na mafundisho, matendo yake na miujiza mbalimbali,jambo lililofanya sura ya huruma Mungu ijidhihirishe na upendo wa Mungu ushikike. Hali inayofanya kila mtu, katika kila hali na nafasi, aonje kukubalika na kupendwa na Mungu ambaye upendo na huruma yake havifungwi na hali zetu. Huo unabaki kuwa utume wa Kanisa, utume wa kueneza huruma na upendo wa Mungu: “Yesu aliwaita watu kumi na wawili wamfuate kwa karibu zaidi na washiriki katika kazi yake. Yesu aliwapa watu hao jina mitume. Walishuhudia huduma mbalimbali zilizofanywa na Yesu, walihifadhi akilini mwao yale waliyoona na kuyasikia.

Katika mafundisho yake Yesu akifuatwa na makundi kwa makundi, aliwalisha wenye njaa, aliwaponya wagonjwa, aliwafukuza pepo na kuwafufua wafu”. Huu unaendelea kuwa utume wa kila mwanakanisa, maana, kama anavyofundisha Baba Mtakatifu Francisko, “Yesu anathibitisha kwamba huruma siyo tendo la Baba tu, bali ni kigezo cha hakikisho la wana wake kweli. Kwa kifupi tunaitwa kuonesha huruma kwasababu tumeonewa huruma kwanza”. Huruma ya Mungu kwetu inaonekana pia katika tunza yake kwetu, akitulinda na kutuneemesha, ili tuishi kwa furaha na amani.

Kilele cha ufunuo wa huruma ya Mungu kwa mwanadamu ni tukio kuu la fumbo la Pasaka. Tukio la mateso, kifo na ufufuko wa Kristo ni kilele cha tendo la huruma na upendo wa Mungu kwetu. Yesu Kristo alitoa nafsi yake iwe fi dia ya dhambi. Kwa sababu hiyo kila mkosefu amechangia katika mateso na kifo cha Yesu Kristo, na mateso, kifo na ufufuko wa Kristo ndio sababu ya wokovu wa kila mkosefu. Hivyo sura halisi ya upendo wa Mungu ni huruma yake, na huruma “ni jina la pili la upendo.”

Na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania








All the contents on this site are copyrighted ©.