2016-02-29 15:47:00

Teteeni maisha, lindeni wanyonge na dumisheni amani na usalama


Baba Mtakatifu Francisko Jumatatu tarehe 29 Februari 2016 amekutana na kuzungumza na Kikosi cha Ulinzi na Usalama cha Askari wa Roma, Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, kinachotoa huduma makini na nyeti; kwa kujisadaka bila ya kujibakiza ili kuhakikisha kwamba, kunakuwepo ulinzi na usalama kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama.

Baba Mtakatifu anawashukuru kwa kuwasaidia watu kuheshimu na kufuata sheria za nchi na kwamba uwepo wao katika eneo hili ni kielelezo cha mshikamano wa Jumuiya nzima na kwamba, maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii waweze kupata msaada ili kukabiliana na ugumu wa maisha! Kikosi hiki kinashirikiana kwa karibu sana na Vatican ili kuhakikisha kuna kuwepo na amani, ulinzi na usalama katika matukio mbali mbali yanayoadhimishwa kwa nyakati mbali mbali kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican na viunga vyake.

Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza kwa huduma makini kwa mahujaji na watalii, huduma inayohitaji weledi, uwajibikaji madhubuti pamoja na kuwajali watu, wengi wao wakiwa ni wazee, huduma inayohitaji uvumilivu kwa wote; fadhila ambazo zinawataka kutumainia msaada wa Mungu. Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ni chachu ya upyaisho unaojikita katika utakaso wa maisha ya ndani unaoshuhudiwa katika matendo na maisha ya kila siku, daima kwa kujitahidi kuwa waaminifu kwa Injili ya Kristo kila mtu kadiri ya hali na wito wake.

Jubilei ya huruma ya Mungu ni fursa ya kufanya tafakari makini katika ngazi ya mtu mmoja mmoja na Jumuiya katika ujumla wake mintarafu matendo ya huruma: kiroho na kimwili; kwani kila walilomtendea mmoja wapo wa walio wadogo, wamemtendea Kristo mwenyewe. Huu ni mwongozo thabiti hata kwa wafanyakazi katika vyombo vya ulinzi na usalama, wanaotakiwa kujenga na kuimarisha mshikamano hususan na maskini na wanyonge zaidi ndani ya Jamii; kwa kusimama kidete kulinda na kutetea maisha kwa kujikita katika ulinzi na usalama, huku wakitambua kwamba, kila mtu anapendwa na kuthaminiwa na Mungu, anapaswa kukaribisha na kuheshimiwa.

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu itakuwa ni nafasi ya kupyaisha ari na mwamko wa utekelezaji wa majukumu yao kitaaluma kwa kuendelea kujisadaka kwa njia ya ukarimu. Baba Mtakatifu Francisko mwishoni, anawashukuru wote kwa huduma yao makini na ushirikiano na Vatican. Anawaweka wote hawa chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Malkia mwaminifu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.