2016-02-29 08:06:00

Miaka 125 ya upendo na huruma ya Mungu Zambia


Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu nchini Zambia yanakwenda sanjari na Jubilei ya miaka 125 tangu Familia ya Mungu nchini Zambia ilipopokea imani ya Kikristo. Maadhimisho haya yatazinduliwa rasmi  mwezi Agosti 2016 na kuhitimishwa hapo Agosti 2017. “Miaka 125 ya upendo na huruma ya Mungu” ndiyo kauli mbiu inayoongoza maadhimisho ya Jubilei ya miaka 125 ya Ukristo nchini Zambia.

Haya yameelezwa na Padre Justine Matepa, Mratibu mkuu wa shughuli za kichungaji, Baraza la Maaskofu Katoliki Zambia. Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu yameunganishwa na Jubilei ya miaka 125 ya Ukristo Zambia, ili kumshukuru Mungu kwa wema na ukarimu wake kwa Familia ya Mungu nchini Zambia. Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu yalizunduliwa na kila Jimbo kadiri ya maelekezo yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko ili kutoa fursa kwa waamini wengi kushiriki maadhimisho haya kadiri ya uwezo na nafasi zao.

Maandalizi ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu nchini Zambia yalianza kushika kasi kunako mwezi Aprili 2015 kwa kuwakutanisha wakurugenzi wakuu wa shughuli za kichungaji majimboni, Makatibu wa Katekesi na Waratibu wa Utume wa Biblia. Mapendekezo yaliyotolewa katika mkutano huu, yaliridhiwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Zambia. Huu ni mwendelezo wa maadhimisho ya Mwaka wa Imani ili kweli Familia ya Mungu nchini Zambia iweze kuambata na kushuhudia huruma ya Mungu katika uhalisia wa maisha yake.

Katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, watoto na vijana kutoka Zambia watapewa kipaumbele cha pekee, ili waweze kunolewa vyema katika katekesi makini, tayari kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu kwa jirani zao. Familia ya Mungu nchini Zambia inataka kuwasha  moto wa upendo na huruma ya Mungu kwa watu wake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.