2016-02-29 07:54:00

Huduma ya afya kwa maskini wa Roma!


Dr. Lucia Ercoli, Mkurugenzi mkuu wa Chama cha Madaktari wa Mshikamano nchini Italia anamshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kuanzisha kituo cha afya kwa maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kwenye eneo la Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Madaktari na wauguzi kutoka Vatican watakuwa wanashirikiana na madaktari wenzao kutoka Hospitali ya Policlinico Tor Vergata iliyoko mjini Roma, ili kutoa huduma ya tiba kwa maskini na wahitaji zaidi.

Dr. Ercoli katika taarifa yake kwa vyombo vya habari anakaza kusema baada ya kuanza kutoa huduma ya afya katika maeneo yaliyoko pembezoni mwa Mji wa Roma, wamekubali pia mwaliko wa kutoa huduma hii kwa maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii mjini Roma hususan kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Anakiri kwamba, bado kuna mambo mengi ya kufanya hasa maeneo yaliyoko nje ya kidogo ya mji wa Roma, lakini kituo cha tiba kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican ni alama ya matumaini na huruma ya Mungu hasa wakati huu Mama Kanisa anapoadhimish Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, mwaliko wa kumwilisha matendo ya huruma kiroho na kimwili katika uhalisia wa maisha ya watu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.