2016-02-29 08:18:00

Fadhila na maadili katika huduma kwa wagonjwa!


Taasisi ya Kipapa ya maisha, kuanzia tarehe 3-5 Machi 2016 itafanya mkutano wake mkuu utakaojihusisha zaidi na masuala ya fadhila na maadili katika maisha ya binadamu. Katika mkutano huu, hapo tarehe 4 Machi 2016, kutafanyika warsha ya hadhara itakaowahusisha kwa namna ya pekee: wasomi, watafiti, wafanyakazi katika sekta ya afya na wanafunzi wanaotaka kujinoa katika uwanja wa fadhila na maadili, ili kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya uhai. Warsha hii itakuwa na mwelekeo wa kitaalimungu na kifalsafa; kimaadili na kihuduma; kijamii na kitamaduni.

Lengo la Warsha hii ni kuwasaidia wadau mbali mbali kujipatia fadhila zitakazowasaidia kufanya maamuzi thabiti mintarafu kanuni maadili na utu wema; mafao ya wengi; kanuni za kimataifa kuhusu maisha ya binadamu; maadili kanuni maadili ya wahudumu katika sekta ya afya. Itakumbukwa kwamba, sekta ya afya ni kati ya changamoto kubwa za kimaadili kwa nyakati hizi, kumbe, washiriki watafundwa namna ya kutekeleza mchakato wa maamuzi ya kitabibu, tafiti za kitabibu na huduma ya wauguzi hospitalini.

Hii itakuwa ni nifursa pia kwa washiriki kuelekezwa namna ya kugundua fadhila, ili kuwawezesha kusimama kidete, kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya uhai. Ikumbukwe kwamba, fadhila zinazozungumziwa hapa ni imani, matumaini na mapendo na nyingine ni busara, haki, nguvu na kiasi. Hizi ni fadhila ambazo ni muhimu sana katika kulinda zawadi ya maisha ya binadamu mintarafu nidhamu ya shughuli za kitabibu. Wawezeshaji wa warsha hii ni wataalam wa kimataifa, wenye ujuzi na mang’amuzi makubwa katika masuala haya.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.