2016-02-29 09:51:00

Damu ya mashuhuda wa imani ni mbegu ya Ukristo mpya na Umoja wa Wakristo!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 29 Februari 2016 amekutana na kuzungumza na Patriaki Abuna Matthias wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox  Tewahedo la Ethiopia kwa kumtakia amani, ustawi na maendeleo ya familia ya Mungu nchini Ethiopia. Baba Mtakatifu anasema, uwepo wake mjini Vatican ni sehemu ya mchakato wa kuimarisha mahusiano ya Makanisa haya mawili, kama ilivyokuwa kwa Patriaki Abuna Paulos alipomtembelea Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 1993 na mwaka 2009 alipokutana na kuzungumza na Papa mstaafu Benedikto XVI pamoja na kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya awamu ya Pili ya Sinodi ya Maaskofu Barani Afrika mwendelezo wa mapokeo kutoka katika Kanisa la mwanzo.

Baba Mtakatifu ameendelea kufafanua kwamba, kunako mwaka 2012, ujumbe wa Vatican ulishiriki katika mazishi ya Patriaki Abuna Paulos, ili kuendelea kuimarisha mahusiano ya Makanisa haya wakati wa raha na shida. Kuanzia mwaka 2004 Kanisa Katoliki na Kanisa la Kiorthodox la Mashariki wamejikita katika mchakato wa kukuza na kudumisha majadiliano ya kiekumene kupitia Tume ya Pamoja ya Kitaalimungu na kwamba, Kanisa la Kiorthodox Tewahedo la Ethiopia limeshiriki kikamilifu.

Katika kipindi hiki chote majadiliano ya kiekumene yamejikita zaidi katika Umoja wa Kanisa unaoyashirikisha Makanisa haya umoja unaofumbatwa katika Fumbo la Utatu Mtakatifu; kielelezo cha: Imani, Ubatizo, Bwana na Yesu Kristo Mkombozi wa Ulimwengu. Makanisa haya yanaunganishwa na fadhila ya Sakramenti ya Ubatizo, inayowawezesha kuwa ni sehemu ya Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Waamini wanaunganishwa pia katika utajiri wa Mapokeo ya Kimonastiki na Liturujia; mambo yanayowafanya wote kujisikia kuwa ni ndugu wamoja katika Kristo. Kumbe, kuna mambo mengi yanayowaunganisha, ikilinganishwa na yale yanayowagawa!

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, mateso na mahangaiko ya Wakristo wa Makanisa haya mawili yanawaunganisha na kuwaimarisha katika mchakato wa majadiliano ya Uekumene wa damu, ambao umekuwa ni mbegu ya Ukristo mpya katika Kanisa la mwanzo na kwamba, damu ya mashuhuda wa imani kwa nyakati hizi inakuwa ni mbegu ya umoja wa Wakristo na kwamba, majina yao yameandikwa kwenye kitabu cha mashuhuda wa imani ya Kanisa la Mungu. Uekumene wa mashuhuda wa imani ni mwaliko kwa Wakristo kutembea kwa pamoja ili kufanikisha umoja mkamilifu wa Kanisa.

Baba Mtakatifu anatambua kwamba, Kanisa la Kiorthodox la Ethiopia tangu mwanzo limekuwa ni Kanisa la mashahidi wa imani na kwamba, hadi leo hii, wanaendelea kushuhudia chuki za kidini dhidi ya Wakristo na waamini wa dini nyingine huko Mashariki ya Kati na baadhi ya nchi za Bara la Afrika, changamoto kwa viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kisiasa na kiuchumi kuhakikisha kwamba, wanajifunga kibwebwe ili kujenga jamii inayojikita katika misingi ya: haki, amani, upatanisho, msamaha na mshikamano. Ethiopia inaendelea kujipambanua katika mchakato wa maboresho wa maisha ya watu wake kwa kujikita katika haki, utawala wa sheria pamoja na kuheshimu mchango wa wanawake katika jamii.

Baba Mtakatifu anatambua tatizo la ukosefu wa maji safi na salama na athari zake katika masuala ya kijamii na kiuchumi. Hapa Makanisa hayana budi kushirikiana kwa karibu zaidi ili kudumisha mafao ya wengi na utunzaji bora wa mazingira. NI matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, mazungumzo kati yake na Patriaki Abuna Matthias wa kwanza yatasaidia kuimarisha urafiki wa kidugu kati ya Makanisa haya mawili, tayari kufungua ukurasa mpya wa msamaha na uponyaji kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Baba Mtakatifu anamwomba Patriaki Abuna Matthias wa kwanza kuendelea kusali kwa ajili ya kuombea umoja wa Wakristo kutoka katika ulinzi na tunza ya mashuhuda wa imani na watakatifu kwa ajili ya familia ya Mungu. Roho Mtakatifu aendelee kuwasaidia, kuwaangazia na kuwaongoza katika njia ya maridhiano, amani na matumaini, ili siku moja waweze kuadhimisha Sadaka ya Kristo Altareni wakiwa wameungana kikamilifu katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.