2016-02-27 07:56:00

Wekezeni katika elimu kwa vijana ili kuwajengea matumaini!


Kardinali Antonio Maria Vegliò, Rais wa Baraza la Kipapa la shughuli za kichungaji kwa wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum anasema kuna haja ya kuwekeza zaidi katika sekta ya elimu kwa vijana wa kizazi kipya na kuwa na mwelekeo wa pekee hasa kwa vijana wahamiaji na wakimbizi, ili kuweza kuwajengea matumaini na maisha bora zaidi.

Wakimbizi na wahamiaji wakiheshimiwa na kuthaminiwa, wakashirikishwa katika maisha ya kijamii, wanaweza kuwa utajiri mkubwa katika mchakato wa ujenzi wa jamii inayojikita katika tunu msingi za maisha. Ili kufanikisha lengo hili, kuna haja ya kuwekeza zaidi katika elimu inayowajengea vijana wa kizazi kipya uwezo wa kupenda na kuthamini tofauti zinazojikitokea katika masuala ya mahali anapotoka mtu, tamaduni na dini, ili kuondokana na misimamo mikali ya maisha inayojikita katika ubinafsi na tabia ya baadhi ya watu kuwa na maamuzi mbele.

Kardinali Antonio Maria Vegliò ameyasema haya hivi karibuni alipokuwa anachangia hoja kwenye mkutano wa kimataifa ulioandaliwa na Ubalozi wa Canada nchini Italia kwa kuongozwa na kauli mbiu “Uhamiaji na ushirikishwaji wa kijamii: Majadiliano kati ya Italia na Canada. Il kweli sekta ya elimu iweze kutekeleza utume wake barabara katika jamii haina budi kujikita katika mchakato wa kutafuta majibu muafaka ya matatizo na changamoto zinazomwandama mwanadamu kwa nyakati hizi.

Hapa jamii lazima iwezeke katika tafiti za kisayansi na kijamii mintarafu: demokrasia, haki msingi za binadamu; haki na amani; mazingira na mapambano dhidi ya umaskini wa hali na kipato; majadiliano ya kidini na kiekumene; ushirikiano na mafungamano ya kimataifa pamoja na kuangalia masuala yanayofumbata maendeleo endelevu ya binadamu! Dhamana hii ni nyeti na shirikishi, na kila mtu anaweza kuchangia kadiri ya uwezo wake kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi. Diplomasia kwa asili inajikita katika mchakato wa majadiliano kwa kutambua kwamba, utume wao mkubwa ni kujenga madaraja yanayowakutanisha watu wa mataifa.

Kardinali Antonio Maria Vegliò anaendelea kufafanua kwamba, jamii pia inapaswa kuwekeza katika uraia na ushirishwaji wake; kwa kuwaandaa walimu watakaorithisha tunu msingi za kitamaduni na kiutu; kwa kuwa na sera makini ya familia; usalama wa raia na mali zao; afya na maisha; mambo ambayo yanahitaji kimsingi kuwa na sera bora zaidi kuhusiana na changamoto ya wakimbizi na wahamiaji kwa kukazia: haki na wajibu.

Hapa Kanisa linapenda kutoa mchango wake wa kimaadili na kiutu kwa kukazia haki msingi za binadamu, utu na heshima ya binadamu bila kuingilia masuala ya ndani ya nchi husika. Kanisa katika maisha na utume wake, limejenga utamaduni wa upendo, mshikamano na ukarimu kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kumbe hata wanadiplomasia nao wanaweza kuchangia, ili kulisaidia Kanisa kutekeleza dhamana na wajibu huu ambao uneonesha upendo kwa jirani!.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.