2016-02-27 09:32:00

Papa Francisko "kujichimbia" Mlimani kwa mafungo!


Baba Mtakatifu Francisko pamoja na wasaidizi wake wa karibu kuanzia tarehe 6 – 11 Machi 2016 watapanda kwenda Jangwani ili kusali, kutafakari na kujiwekea mikakati ya maisha na shughuli za kichungaji. Tafakari wakati wa mafungo haya ya maisha ya kiroho itaongozwa na Padre Ermes Ronchi na itafanyika huko Ariccia, nje kidogo ya mji wa Roma. Tafakari hizi ni maswali kumi yanayobubujika kutoka katika Injili yatakayomsaidia Baba Mtakatifu na wasaidizi wake kujiandaa kikamilifu kwa ajili ya kuadhimisha Fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Kristo.

Ratiba elekezi inaonesha kwamba, wakati wote wa mafungo kutakuwepo na Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu ili kutoa nafasi kwa wahusika kwenye mafungo kuweza kuzungumza na Kristo wa Ekaristi. Masifu ya Asubuhi, Tafakari, Ibada ya Misa Takatifu na Masifu ya Jioni. Maswali ya msingi: Je, mnatafuta nini? Mbona mmekuwa na woga? Hamna imani ndani mwenu? Ninyi ni chumvi na nuru ya ulimwengu.

Ninyi mnasema kuwa mimi ni nani? Yesu akamwambia Petro, umemwona huyu mwanamke? Yesu akawauliza, Je, mna mikate mingapi? Yesu akamuuliza yule mwanamke, Je, washitaki wako wa wepi? Hakuna aliyekuhukumu? Mwanamke mbona unalia? Unamtafuta nani? Simone wa Yohane, Je, wanipenda? Bikira Maria akamuuliza Malaika, Je, litakuaje neno hili? Yote haya ni maswali msingi yanayobubujika kutoka katika Injili. Itakumbukwa kwamba, wakati wote wa kipindi cha mafungo, hakutakuwepo na katekesi siku za jumatano, mikutano ya hadhara na binafsi, ili kutoa nafasi kwa Baba Mtakatifu na wasaidizi wake wa karibu, kuzama zaidi katika sala na tafakari, ili kujichotea tena nguvu ya kusonga mbele kwa imani na matumaini, tayari kukabiliana na changamoto za maisha na utume wa Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.