2016-02-27 09:08:00

Ijumaa ya huruma ya Mungu!


Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu amejipangia walau kila Ijumaa kutekeleza tendo moja la huruma, ili kuhakikisha kwamba, huruma ya Mungu inagusa na kuacha chapa ya kudumu katika mioyo ya watu! Ijumaa tarehe 26 Februari 2016, Baba Mtakatifu Francisko ametembelea Jumuiya ya San Carlo iliyoko Castel gandolfo, nje kidogo ya mji wa Roma. Hiki ni kituo cha mshikamano nchini Italia, kinachotoa huduma kwa watu wanaotengwa na kusukumizwa pembezoni mwa jamii, hususan waathirika wa matumizi haramu ya dawa za kulevya.

Askofu mkuu Salvatore Rino Fisichella, Rais wa Baraza la Kipapa la Uhamasishaji wa Uinjilishaji Mpya anasema, Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kuwashangaza wengi katika maisha na utume wake. Wakati wa hija yake ya kitume nchini Mexico alikemea vikali biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya na wale wote wanaojihusha na biashara hii kwani wanapandikiza mbegu ya kifo katika maisha ya watu. Baba Mtakatifu aliwataka wadau mbali mbali kuhakikisha kwamba, wanajikita katika mchakato wa kumwilisha kanuni maadili na tunu msingi za maisha ya kiutu na kijamii. Alikumbusha kwamba, vijana ni jeuri na matumaini ya Kanisa na Jamii katika ujumla wake.

Baba Mtakatifu akiwa nchini Mexico aliwaambia Maaskofu kwamba, haitoshi kwa viongozi wa Kanisa kukemea na kulaani mmong’onyoko wa maadili na utu wema ndani ya jamii, lakini, wanapaswa kuwa na sera na mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji unaonesha ujasiri wa kichungaji ili kusaidia mchakato wa maboresho ya jamii kwa kuwa karibu na familia; kwa kusaidia kuganga na kuponya madonda ya mwanadamu; pamoja na kuendeleza malezi na majiundo makini katika medani mbali mbali za maisha ili kudumisha misingi ya haki, amani, usalama, ustawi na maendeleo ya wengi sanjari na kukuza Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo.

Kwa mkakati huu wa kichungaji unaopania kudumisha na kumwilisha huruma ya Mungu kwa maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, Ijumaa, Baba Mtakatifu alitembelea na kuzungumza na Jumuiya ya San Carlo, iliyoanzishwa na Don Mario Picchi kunako mwaka 1979 inayotoa huduma kwa waathirika wa dawa za kulevya 60 wanaohudumiwa na Jumuiya hii ambayo ni kielelezo cha ushuhuda wa huruma ya Mungu. Watu wengi wameguswa na uwepo pamoja na ushuhuda wa Baba Mtakatifu Francisko kati yao. Kwa ukimya mkuu, amesikiliza historia ya maisha yao na kuonesha uwepo wake wa kibaba kwa kila kijana.

Baba Mtakatifu amewahamasisha vijana hawa kutojikatia tamaa ya maisha na hatimaye, kumezwa tena na matumizi haramu ya dawa za kulevya kwani mbele yao kuna fursa ya kuweza kuanza tena upya na kuwa watu wema zaidi. Baba Mtakatifu amekazia umuhimu wa kutumainia na kuambata huruma ya Mungu katika maisha hasa huku bondeni kwenye machozi, lakini uwepo wa huruma ya Mungu, unawafariji na kuwapatia tena matumaini mapya katika maisha, tayari kusonga mbele kwa imani na matumaini zaidi.

Kituo cha mshikamano cha Don Mario Picchi katika utume wake kwa kipindi cha miaka 45 iliyopita kimewahi pia kuwapokea na kuwakaribisha Mtakatifu Yohane Paulo II na Mwenye heri Paulo VI. Kituo hiki kinaendelea kupanua wigo wa utume wake kwa ajili ya kuwasaidia vijana wanaotumbukia katika matumizi haramu ya dawa za kulevya, ili kuwasaidia kutoka katika shimo la kifo na kuwapatia tiba muafaka. Janga la matumizi haramu ya dawa za kulevya ni kati ya changamoto zilizofanyiwa kazi na Mtakatifu Yohane Paulo II katika maisha na utume wake, kwa kuwataka viongozi wa Kanisa kuhakikisha kwamba, wanawarejeshea tena vijana utu na heshima yao, kwani wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Sadaka wanayoifanya wale wote wanaohudumia vijana hawa ni utajiri unaobubujika kutoka moyoni.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.