2016-02-26 15:40:00

Ongokeni ili kuzaa matunda ya huruma na upendo!


Katika ukumbi wa michezo, linapofunuliwa pazia, jukwaani hujitokeza waigizaji waliovalia rasmi mavazi ya kimchezo na kufanya maigizo kwa sauti na matendo kadiri ya mada ya tamthilia. Baada ya mchezo pazia linafungwa na waigizaji huonekana na nguo zao za kawaida na kuendelea na maisha yao ya kawaida. Wachezaji wakijitokeza nje ya ukumbi na kutembea mitaani na mavazi ya kuigiza wanakuwa kichekesho kisicho na kiingilio. Leo tutapewa ushauri nasaa wa kuyapa maana maisha yetu tusije tukayaishi kitamthilia, na baada ya kwisha maisha haya, tunabaki kuwa burudani la bure. 

Mazingira yaliyompeleka Yesu kutoa onyo hilo yalikuwa kule hekaluni Yerusalemu. Fasuli inaanza hivi: “Wakati huo huo,” yaani muda ule ule ambao Yesu alikuwa anazungumza juu ya kuwajibika kwa jamii mpya aliyoiunda. Yesu anatoa onyo kali kwa wanafiki wasioyapa maana ya kiutu maisha yao. Hasahasa tunaonywa vikali sisi tunaomwigiza Yesu bila ya kumuishi kidhati, pazia litakapofungwa tutabaki na kanzu za igizo na kuwa kichekesho kisicho na kiingilio.

Wakati Yesu anaongelea mada hiyo ndipo alipoletewa taarifa ya “Wagalilea ambao Pilato alichanganya damu yao na dhabihu zao.” Yesu hakukishangaa kituko hiko kwani hakikuwa cha pekee sana, kwani mara nyingi wahaji walileta vurugu mle hekaluni kwa kusukumana, au hata kujibizana vibaya na kurushiana ngumi. Pilato alikuwa makini sana na safari hii ilimlazimu kutuma askari walioingia hekaluni na kuzima fujo kwa kutumia silaha hadi wahaji kuvuja damu. Kumbe kwa Wayahudi, kitendo cha askari kuingia hekaluni ni cha unajisi mkubwa sana. Mbaya zaidi kitendo cha kumwaga damu za wahaji kilikuwa kashfa iliyopitiliza. Kwa hiyo Wayahudi wakiwa wamejaa mdadi, wakaja kwa jazba kumweleza Yesu akilaani kitendo hicho mara moja hata ikibidi kupambana na uongozi. Malalamiko yao yalikuwa ya kisiasa na ya kidini.

Kumbe, Yesu hakutaka kuingilia mambo ya kisiasa kama walivyotegemea wao. Kadhalika kidini, watu waliouawa walichukuliwa kuwa kama waliolaaniwa na kuachwa na Mungu, kwa sababu kadiri ya Biblia takatifu, jambo jema limpatalo mtu ni baraka itokayo kwa Mungu, wakati kila jambo baya alipatalo mtu ni laana ya Mungu. Iwe iweje, Yesu akaamua kutofautiana kabisa na fikra zao. Yesu anaanza kwanza kutoa maelezo:“Mnadhani kwamba watu hawa walikuwa wamekosa zaidi kuliko Wagalilea wengine,” yaani, anataka kufuta kabisa fikra za kuunganisha maafa hayo na dhambi, kwa sababu maafa yanaweza kumpata mtu au jamii yoyote ile.

Halafu anatoa onyo kwamba “kama hamjuti (hamfanyi toba) nanyi mtapotea kama wao” hapa anataka kufuta mzizi wa uovu hasa wa kujiridhisha kwa kutoa majibu mepesi kwa maswali magumu ya maisha, hivi anapendekeza kufanya mapinduzi ya kuongoka na kubadilika, hasa kwa viongozi kama Pilato aliyetoa amri ya kumwaga damu, badala ya kiongozi kutumikia yeye anatawala. Kahdalika kuhusu mnara wa Siloe ulioanguka anasema: “Mnafikiri kwamba watu hawa kumi na wanane walikuwa waovu kuliko wengine, hapana. Lakini nanyi msipotubu mtapotea kama wao.” Hapa tena Yesu anasisitiza kutohusianisha majanga na dhambi.

Ndugu zangu, tunaalikwa kutafakari maneno ya Yesu, kwamba kila yanapotokea maafa tusikimbilie kutoa majibu mepesi, bali yabidi kila mmoja kuyarekebisha maisha yake kadiri ya mapendekezo ya Yesu na kuyaishi kwa dhati na siyo kumwigiza tu. Kwa mtazamo huo wa kuishi maisha ya dhati yatoayo matunda ya kweli, na siyo kuigiza tu kwa kupendeza kwa nje kama mwigizaji, ndipo Yesu anatoa mfano ufuatao: “Mtu mmoja alikuwa na mtini umepandwa katika shamba lake la mizabibu; akaenda akitafuta matunda juu yake, asipate.” Mti huu ulikuwa na majani mazuri yanayopendeza kwa nje lakini hauna matunda.

Mhusika wa kwanza katika mfano huu ni Bwana mwenye shamba la mizabibu. Bwana anaenda kukagulia  shamba lake la mizabibu kama linazaa matunda au la, lakini hasa alienda kuangalia mtini. Kwa bahati nzuri au mbaya mtini huu umepandwa ndani ya shamba la mizabibu. Katika biblia, zabibu na tini ni alama ya taifa la Waisraeli. Kuhusu zabibu nabii Isaya alisema: “Mpenzi wangu alikuwa na shamba la mizabibu, kilimani penye kuzaa sana. Akafanya handaki kulizunguka pande zote, akatoa mawe yake, akapanda ndani yake mzabibu ulio mzuri, akajenga mnara katikati yake, akachimba shinikizo ndani yake. Akatumaini ya kuwa utazaa zabibu, nao ukazaa zabibumwitu.” (5:1-2) Kwa hiyo mhusika wa kwanza ambaye ni Bwana mwenye shamba ni Mungu mwenyewe.

Wahusika wa pili ni shamba la mizabibu ambalo ni Waisraeli. Mungu alitegemea zabibu zingezaa matunda matamu, yaani Wisraeli wangekuwa wema kumbe wamegeuka kuwa zabibumwitu. Hapo Mungu amedanganyika juu ya maisha ya wahusika hawa wa pili kwani wamekuwa waigizaji tu. Kadhalika nabii Hosea anawalinganisha Waisraeli na mtini, ambao ni mhusika wa tatu. Mtini huu umepandwa ndani ya shamba la mizabibu ili kuonesha kuwa ndani ya taifa la Waisraeli (mizabibu) kuna mtini unaotakiwa kukuzwa. Kwa hiyo mtini hapa unalinganishwa na mtu binafsi katika jamii au jumuia, kwamba kila mmoja anao wito wa pekee na anawajibika kutoa matunda. Kwa bahati mbaya mtini huo mmoja nao hauzai matunda. Hapo ndipo anapoingia mhusika wa nne ambaye ni, mtunzaji wa shamba la mizabibu. Mtunzaji huyo ni Yesu Kristo aliyefika kuchapa kazi shambani mwa Bwana.

Mwenye shamba anakasirika na kusema kwa ghadhabu: “Tazama miaka mitatu hii naja nikitafuta matunda juu ya mtini huu, nisipate kitu.” Ni kweli mtunza shamba amefanya kazi miaka mitatu lakini hakuna matunda. Miaka hiyo mitatu ni maisha ya Yesu hadharani na ile miaka ya mahubiri ya Yohane mbatizaji aliyehubiri kuongoka na kuzaa matunda ya wema. Mwenye shamba anaamua bila kigugumizi kupitisha maamuzi mazito: “Uukate mbona hata nchi unaiharibu?”

Tamko hili linaibua majadiliano na lugha gongana kati ya mwenye shamba (Mungu) na mtunzaji (Yesu). Hebu yafuatilie mabishano hayo. Mwenye shamba anasema: “Uukate.” Mtunzaji wa shamba anapinga “haukatwi mti hapa” badala yake“uuache mwaka huu nao, hata niupalilie niutilie samadi; nao ukizaa matunda baadaye, vema! La, usipozaa, ndipo uukate.” Hapa yaonekana mwenye shamba ni mkali, hana huruma, wakati mtunzaji wa shamba ni mwema, na mwenye huruma. Huyo ndiye Mungu tuliye naye sisi katika fikra zetu. Mungu yule anayetoa hukumu ya kukata mtini ni matokeo ya hukumu na mitazamo yetu tunayofikiri kuwa ndiyo haki ya Mungu. Kumbe, Yesu anatukosoa na kutuonesha Mungu halisi ambaye uso wake unaakisiwa katika Yesu mwenyewe wa Nazareti. Mungu wa kweli ni yule anayewakilishwa na Yesu, yaani Mungu mwema, mwenye huruma, mvumilivu mwenye subira, huyo ndiye tunayetakiwa kumwaminia na kumwishi daima.

Angalia Mtunzaji wa shamba anamwomba Bwana mwenye shamba aongezewe mwaka mmoja tu ili kuushughulikia mtini: “Bwana uuache mwaka huu,”  huo sasa utakuwa ni mwaka wa nne toka mtini ulipotegemewa kutoa matunda. Mwaka huo wa nne siyo wa kihistoria, bali toka pale ambapo Yesu alitoa sera zake katika sinagogi ya Nazareti: “Leo Maandiko haya yametimia masikio mwenu,…..na kutangaza mwaka wa neema uliokubaliwa,” yaani mwaka wa jubilei. Mwaka wa jubilei ni wa maisha yanayodumu daima hadi mwisho wa historia. Huo ndiyo mwaka wa nne, ambao mfanyakazi, mtunza shamba la mizabibu anaendelea kufanya kazi katika shamba la mizabibu akiupalilia mtini, akiutilia mbole, na kuuchengelea hadi kieleweke. Kisha anasema: “Usipozaa, ndipo uukate” maneno hayo yanaonekana kuwa kama laana na tishio, kumbe ni mwaliko kwetu kutilia maanani maisha yetu hapa duniani. Tusiwe waigizaji wa maisha, bali tuongoke na kutoa matunda ya upendo na huruma. Tukifanya vinginevyo imekula kwetu.

Ndugu zangu, shamba la mizabu ni jumuiya ya Kanisa, na mtini ni Mkristo mmoja binafsi, yaani wewe na mimi ambao ni sehemu ya jumuiya na taifa hili la Mungu. Leo kila mmoja anaalikwa kutambua kwamba maisha yetu hayana budi yatoe matunda anayoyategemea Mungu. Na matunda yanayotegemewa siyo yale ya mchezo wa kuigiza, bali daima tuzae matunda yanayodumu daima. Matunda anayoyategemea Bwana unayakuta katika waraka kwa Wagalatia, nayo ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi Wagalatia 5:22-23). Hivi jiangalie sana, kama maisha yako hayatoi matunda, basi geuka, ongoka na ukumbuke kwamba mwishoni Bwana anategemea matunda kutoka kwenye maisha aliyokupa.

 

Na Padre Alcuin Nyirend, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.