2016-02-25 14:32:00

Papa asema ; ni baraka mtu maskini kubisha hodi mlangoni petu


Imani ya kweli  huenda sambamba na kujali mahitaji ya watu maskini walio karibu yetu, kwa kuwa katika  kumwona mtu maskini, ni kuiona sura ya  Yesu anayebisha hodi  moyoni mwetu. Baba Mtakatifu Francisko alieleza Mapema Alhamis hii wakati akiongoza Ibada ya Misa katika Kanisa dogo la Mtakatifu Marta ndani ya Vatican.

Homilia ya Papa ililenga katika Injili ya siku, ambamo  Yesu anatoa mfano wa mtu tajiri, aliyekuwa akivaa nguo za hariri za  kifahari  na kufanya karamu kifahari kila siku,  bila ya kumjali mtu maskini aliyekuwa mlango kwake kila siku aliyeitwa Lazaro, ambaye mwili wake ulifunikwa na vidonda.

Akiutafakari mfano huu,  Papa ametoa mwaliko kwa watu wote , kujihoji iwapo ni wakristo wa kweli au ni Wakristo wa jina wenye kutembea katika njia bandia za kifahali, kama ilivyokuwa kwa mtu huyo tajiri, aliyetajwa kuzijua amri zote za Mungu  kama muumini, akiishika siku ya Sabato bila kukosa kinachotakiwa kufanywa, kwenda katika Sinagogi na mara moja kwa mwaka hekaluni, nje akionekana kuwa mtu wa dini lakini maisha yake yakiwa mbali na dini ya kweli .

Papa amwelezea mtu huyo kwamba , alikuwa anaishi maisha ya kujifungia  katika dunia yake ndogo, ya kifahari,  dunia ya karamu, dunia ya mavazi ya kifahali na marafiki wa ngazi za juu, akiishi maisha batili yanayofanana na ufahali wa povu, lenye kuonekana kwa kupendeza lakini mara hutoweka.  Papa amemtaja tajiri kumezwa na mambo yake na kupuuza kinachoendelea nje ya nyumba yake, hivyo hakuwa hata na mawazo kwamba  kuna watu wngine wanaohitaji msaada wake, kukidhi mam bo muhimu katika yao, mfano  kusadia wagonjwa. Mawazo yake  yalikuwa ni juu   yeye mwenyewe tu na  mali yake, ili apate kuendelea kuishi vizuri. . Lakini kumbe vyote hivyo, utajiri na nguvu zake  havikuweza kumsaidia kitu wakati maisha ya hapa duninia yalipohitimu mwisho wake.

 Papa ameeleza na kuonya ni mara ngapi wao kama Maaskofu, huteua watu kufanya kazi za Kanisa  kwa sifa za majina na utajiri wao na kuwaweka pembeni watu maskini na wanyonge? Ameonya  Mungu Baba wa Huruma hafanyi hivyo. Yeye hana upendeleo . Lazaro mtu maskini aliyekuwa mlangoni akisubiri kula makombo ya tajiri, mtu aliyekuwa na taabu nyingi za maisha, anapokewa na katika huruma ya Mungu. .

Aidha Baba Mtakatifu Francisko amewakumbusha Wakristo hasa katika wakati huu wa Kwaresima  kwamba ni muhimu kutoka nje na kuangalia kinachoendelea katika makandokando yetu, pengine kuna maskini aliyeketi kama Lazaro,  akisubiri msaada wetu.  Ni muhimu tukaingia katika njia hii ya kutembea pamoja na Lazaro kwa kuwa Lazaro huyo, ambaye ni Yesu anayependa kusafiri pamoja nasi.  Tunapaswa kutenda kwa wema na huruma , tena tukiwa tumejawa na furaha tele, kuwapokea maskini na wahitaji wanaotuijia.  .

Papa alikamilisha kwa kumwomba Bwana, neema ya moyo mkarimu wa kumwona Lazaro anayebisha hodi mlangoni petu,ili  katika  kukutana na Maskini, huruma ya Mungu iweze kuingia na kukaa  mioyo yetu.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.