Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili iliyopita, tarehe 21 Februari 2016 aliwakumbuka kwa namna ya pekee, wanachama wa Jumuiya ya Papa Yohane XXII, iliyoanzishwa na Mtumishi wa Mungu Don Oreste Benzi ambayo, Siku ya Ijumaa jioni tarehe 26 Februari 2016 inaendesha Njia ya Msalaba kielelezo cha mshikamano na sala kwa ajili ya wanawake na wasichana wanaoendelea kuathirika kwa biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo sehemu mbali mbali za dunia.
Jumuiya ya Papa Yohane XXIII inashirikiana na Idara ya utume wa miito Jimbo kuu la Roma katika kuadhimisha Njia hii ya Msalaba kuzunguka viunga vya mji wa Roma. Huu ni muda wa sala, tafakari na shuhuda mbali mbali kutoka kwa wahanga wa biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo; mambo ambayo yanaathari kubwa kwa utu na heshima ya binadamu. Utumwa mamboleo na biashara haramu ya binadamu ni mambo ambayo hata leo hii yanaendelea kufanyika katika miji mbali mbali duniani na wala si dhana ya mambo yaliyopitwa na wakati.
Jumuiya ya Papa Yohane XXIII katika kipindi cha miaka ishirini na mitano imekuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya utumwa mamboleo na biashara ya ukahaba. Zaidi ya wanawake na wasichana 7, 000 wamekombolewa kutoka katika utumwa mamboleo, leo ni watu huru na wanaendelea na maisha yao kama kawaida. Hadi wakati huu, kuna zaidi ya wasichana na wanawake 200 wanaohudumiwa n ana Jumuiya ya Papa Yohane XXIII. Kila juma, wanachama hawa wanakutana ili kuweka sera na mikakati ya kuwasaidia wanawake na wasichana wanaoendelea kutumbukizwa katika biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo. Takwimu zinaonesha kwamba nchini Italia kuna wasichana kati ya 75, 000 hadi 120, 000 wanaojishughulisha na biashara ya ngono mitaani. Idadi ya wateja wao inakadiriwa kuwa ni millioni tisa inayoingiza kiasi cha Euro millioni 90 kwa mwezi.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
All the contents on this site are copyrighted ©. |