2016-02-25 07:03:00

Italia na Vatican kuendelea kushirikiana kwa karibu zaidi!


Rais Sergio Mattarella wa Italia tarehe 23 Februari 2016 Jumanne tarehe 23 Februari 2016 ameongoza ujumbe wa Serikali ya Italia uliokutana na ujumbe wa Vatican uliokuwa unaongozwa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, kama sehemu ya mapokeo ya maadhimisho ya kumbu kumbu ya Mkataba wa Laterano uliotiwa sahihi kunako tarehe 11 Februari 1929 na kufanyiwa marekebisho kunako tarehe 18 Februari 1984.

Viongozi hawa pamoja na mambo mengine wamejadili kuhusu: vita huko Mashariki ya Kati na maeneo mengine ambako kuna kinzani na mipasuko ya kijamii, kisiasa na kidini; changamoto ya wahamiaji na mchango wa Kanisa katika kuwapokea na kuwakarimu wahamiaji na wakimbizi katika ngazi ya Kanisa mahalia sanjari na ushirikiano katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Kardinali Pietro Parolin akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya mkutano huu, amekiri kwamba, maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu yanaendelea vyema hadi wakati huu na kwamba, kuna mwelekeo na mwitiko chanya kutoka kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema. Serikali ya Italia imeonesha utashi wa kisiasa wa kuendelea kushirikiana kwa karibu zaidi na Vatican ili kuvuka vikwazo na changamoto zilizojitokeza kabla ya uzinduzi wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Kardinali Parolin anakaza kusema, katika mazungumzo yao na Serikali ya Italia wamegusia mambo msingi katika Mkataba wa Laterano na changamoto za nyakati hizi kwa mfano suala zima la itifaki ya kodi ambayo hivi karibuni imeridhiwa kati ya Serikali ya Italia na Vatican. Bado majadiliano yanaendelea kati ya Kanisa na Serikali ya Italia kuhusu dhamana ya Viongozi wa maisha ya kiroho kwa vikosi vya ulinzi na usalama vya Italia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.